NA SOSTHENES NYONI-DAR ES SALAAM
KIUNGO wa kimataifa wa Kenya , Victor Wanyama amemkaribisha mshambuliaji Mbwana Samatta kukipiga LigI Kuu ya England msimu ujao.
Samatta ambaye ni mshambuliaji wa timu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza nchini Uholanzi, ameingia kwenye rada ya timu saba zinazoshiriki Ligi Kuu ya England zikiwania saini yake ili azitumikie msimu ujao.
Timu hizo ni pamoja na Leicester City, Cardiff, Westham United, Brighton, Aston Villa, Watford na Burnley ambazo kama ofa zao zitakubaliwa na Genk, moja wapo itamsajili Samatta.
Mbali ya timu hizo za England, Lazio ya Italia na Lyon ya Ufaransa pia zipo katika mbio za kumwania mshambuliaji huyo wa zamani wa TP Mazembe ya DRC na Simba ya hapa nchini.
Samatta na Wanyama walikutana katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika(Afcon)inayoendelea kushika kasi nchini Misri huku kila mmoja akilipigania taifa lake.
Kwa upand wa Samatta alikuwa nahodha wa kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyoshiriki fainali za Afcon kabla ya kutupwa nje hatua ya makundi.
Kama ilivyo kwa Samatta, ambaye anakipiga Tottenham inayoshiriki Ligi Kuu ya England, alikuwa nahodha wa kikosi cha Kenya(Harambee Stars), kilichoshiriki fainali za mataifa ya Afrika(Afcon)zinazoendelea nchini Misri kabla ya kuondolewa hatua ya makundi.
Mara baada ya Taifa Stars kuondolewa katika michuano ya Afcon, Samatta aliandika maneno haya kupitia akaunti yake ya instagram; “Ilikuwa ni nafasi nzuri kucheza na mmoja wa wachezaji Bora na wa mfano wa kuigwa katika ukanda huu wa Africa mashariki, tunajivunia uwepo wako ndani ya East Africa.”
Maneno ya Samatta yalionekana kumgusa Wanyama ambaye naye kupitia akaunti yake ya instagram jana aliandika;”Nashukuru Sana Kaka yangu,na ni matarajio yangu kukuona premierleague (Ligi Kuu England) msimu ujao tuendelee kupeperusha bendera ya East Africa(Afrika Mashariki).