Derick Milton, Bariadi
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Festo Kiswaga ametoa siku 14 kwa kampuni 13 zinazonunua pamba wilayani humo, kuwalipa wakulima wa zao hilo Sh bilioni 12 wanazowadai.
Kiswaga amesema hayo leo Jumanne Novemba 5, wakati akizungumza na waandishi wa habari ambapo amezitaka kampuni hizo kuhakikisha zinalipa madeni hayo ya wakulima, ikiwamo ushuru wa halmashuari na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).
Amesema wilaya hiyo imezalisha pamba kilo milioni 41.3 yenye thamani ya Sh bilioni 50, ambayo tayari imechukuliwa na wanunuzi hao ambapo wamelipa Sh bilioni 37.2 na bado wanadaiwa Sh bilioni 12.73 fedha za wakulima.
“Ndani ya wiki hizo mbili, kuanzia leo hadi Novemba 20, nawataka wawe wamelipa deni hilo mara moja, baada ya muda huo kama kutakuwa na mnunuzi ambaye atakaidi tutamfuata uko alipo na tutamchukulia hatua kali ikiwamo kumshitaki,” amesema Kiswaga.