25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Wanne wakataa uwaziri wa Magufuli

John+Magufuli+PHOTO*Wahofia kwenda na kasi ya Hapa Kazi Tu!

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

WABUNGE wanne wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametajwa kukataa uteuzi wa nafasi ya uwaziri ili kujaza nafasi za wizara nne zilizokuwa wazi, MTANZANIA imebaini.

Hatua hiyo imetokana na kile kilichoelezwa kuwa ni hofu ya wabunge hao kushindwa kwenda na kasi ya Rais Dk. John Magufuli, ambaye aliwaapisha mawaziri wapya Desemba 12, mwaka huu.

Wakizungumza na MTANZANIA wabunge hao ambao hawakupenda kutajwa majina yao gazetini walidai kuwa kasi ya Rais Magufuli inawatia hofu.

“Kasi ya Rais Dk. John Magufuli ni nzito na kwangu ni ngumu na nilifikiri niko mimi peke yangu kumbe baada ya taarifa hizi nasikia na wenzangu wawili nao walikataa uteuzi.

“Niliarifiwa juu ya uteuzi lakini baada ya kupima nikaona hapana siwezi kazi ya uwaziri, bora ni baki na ubunge wangu,” alisema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe.

WIZARA NNE ZILIZOKOSA MAWAZIRI

Wakati akitangaza Baraza la Mawaziri, Desemba 10, mwaka huu, Rais Magufuli alisema kuna baadhi ya wizara hazina mawaziri kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo unyeti wa wizara hizo na kwamba anaendelea kuwatafuta.

Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli aliteua manaibu waziri wa wizara hizo, huku akitoa ahadi kuwa atawatangaza mawaziri wake baadaye atakapomaliza mchakato.

Wizara hizo ni pamoja na Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu ambayo naibu wake ni Mhandisi Edwin Ngonyani na Wizara ya Fedha na Mipango, ambayo naibu wake ni Dk. Ashatu Kijaji.

Wizara nyingine ni Maliasili na Utalii, ambayo naibu wake ni Mhandisi Ramo Makani, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi ambayo naibu wake ni Mbunge wa Jimbo la Nyasa mkoani Ruvuma, Stella Manyanya.

KINANA ATOBOA SIRI

Mwishoni mwa wiki akiwa mkoani Arusha, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, alitoa siri ya wabunge wanne ambao walipigiwa simu za uteuzi wa uwaziri, lakini walikataa kwa hofu ya kushindwa kwenda na kasi ya Rais Magufuli.

Alisema anachoamini ni kwamba Rais John Magufuli, atakuwa aliwaeleza baadhi ya wabunge kuhusu nia yake ya kuwateua katika nafasi hizo, lakini wao wakamwomba asiwape majukumu hayo kwa kuwa hawana uhakika wa kwenda na kasi anayohitaji katika Serikali yake.

Kinana alisema kinachojitokeza sasa ni kama alivyoshauri Rais Magufuli kuwa si vema kwa waziri aliyeteuliwa kufanya sherehe nyumbani kwake na kuita marafiki kwa kuwa wana mzigo mzito katika kuwatumikia wananchi.

“Ni vema mawaziri hawa wakafanya maombi kwa kuwaita au kuwafuata viongozi wa dini kwani wana kazi ngumu kulingana na nia njema aliyonayo Rais Magufuli katika kupambana na masuala ya ufisadi.

“… kazi ya kupambana na ufisadi kamwe si rahisi hadi kushangilia uteuzi, lengo kubwa ni kuwaletea wananchi maendeleo kupitia ubinafsishaji wa viwanda kutoka kwa watu waliomilikishwa na kuviua,” alisema Kinana.

Katibu mkuu huyo wa CCM, alisema anaunga mkono uamuzi wa Rais Magufuli wa kufuta maadhimisho ya Siku ya Ukimwi dunaini, hali ya kuwa wagonjwa hawana dawa.

“Nyingine ni Wiki ya Maji, mnafanya maadhimisho huku watu hawana maji, Wiki ya Maziwa wakati wafugaji wamekonda na mifugo imekonda haitoi maziwa, fedha hizo zitumike kwa mambo mengine,” alisema Kinana.

MIKATABA KWA MAWAZIRI

Wakati wa kampeni za kuwania urais, Dk. Magufuli, aliahidi kama atafanikiwa kuingia madarakani, atawasainisha mikataba maalumu ya kazi mawaziri wake kabla ya uteuzi.

Alisema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha anakuwa na mawaziri wanaokwenda kwa wananchi badala ya kukaa ofisini wakiandika madokezo.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, atafanya hivyo kwa kuwa anahitaji kuunda Serikali itakayokuwa na mawaziri waliotayari kulitumikia taifa kwa uadilifu.

Kutokana na ahadi hiyo MTANZANIA ilimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa, ili kujua iwapo mawaziri walioteuliwa wamesainishwa mikataba au laa.

Katika majibu yake Msigwa alisema asingeweza kuzungumza kwani yupo katika kikao na kuahidi kuwa atalitolea ufafanuzi suala hilo baada ya muda.

Desemba 10, mwaka huu Rais Magufuli alitangaza Baraza la Mawaziri lenye jumla ya wizara 18 zenye mawaziri 19, huku wizara moja ikiwa na mawaziri wawili.

Katika uteuzi huo, mawaziri 13 walikuwamo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, huku wapya wakiwa wawili ambao ni Balozi Dk. Augustine Mahiga na Nape Nnauye.

Kwa upande wa manaibu waziri, wengi ni sura mpya ambazo hazikuwamo katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya awamu ya nne.

Uamuzi wa kutangaza baraza hilo unavunja ukimya na maswali ya muda mrefu kuhusu uundwaji wa baraza hilo.

Rais Magufuli, alisema pamoja na hali hiyo hata akikamilisha uteuzi wa wizara nne zilizobaki, baraza lake la mawaziri litakuwa na mawaziri 34 tu tofauti na Serikali ya awamu ya nne chini ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, iliyokuwa na mawaziri 60 pamoja na manaibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles