Na Brighiter Masaki, Mtanzani Digital
Jeshi la Polisi limesema idadi ya watu waouwawa na mtu mwenye bunduki ambaye hajafahamika katika tukio la kurushiana risasi jijini Dar es Salaam ni wanne, huku sita wakijeruhiwa.
Inadaiwa mtu huyo amefanya tukio hilo baada ya kuwavamia polisi, kuwafyatulia risasi na kuwaua kisha kuchukua silaha katika maeneo ya daraja la Salenda karibu na Ubalozi wa Ufaransa, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wahabari katika eneo la tukio, Mkuu wa Oparesheni Maalum za Kipolisi, Liberatus Sabas amesema tukio hilo la lililozua taharuki kwa wananchi limetokea leo Jumatano, Agosti 25, baada ya mtu huyo kufyatua hewani risasi huku akisikika akisema kuwa anawatafuta polisi.
“Leo Agosti 25, 2021 tumekutwa na tukio la kiharifu, mtu mmoja ambaye hajafahamika alifika eneo ambapo walikuwepo askari wetu wakiwa kazini, akachomoa bastola na kuanza kuwashambulia kwa risasi na kusababisha vifo vya askari watatu ambapo askari polisi ni wawili na mmoja wa Kampuni ya SGA.
“Alichukua silaha na kuanza kurusha risasi hovyo, akaelekea karibu na Ubalozi wa Ufaransa huku akirusha risasi, amejeruhi watu sita, Askari wetu wamemdhibiti na kumuua. Hivyo jumla ya watu wanne wameuawa kutokana na tukio hilo.
“Kwa sasa ni mapema sana kujua nia yake ya kufanya hivyo laini Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi,” amesema Kamanda Sabas.