26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake zaidi ya 150 waishio vijijini wakutana kujadili changamoto zinazowakabili

 Na Clara Matimo, Kilimanjaro

Wanawake zaidi ya 150 wanaoishi vijijini Kutoka mikoa  mbalimbali hapa nchini wamekutana jana Oktoba 14  Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili na kuiomba serikali pamoja na wadau wa maendeleo wawasaidie kuzitatua.

Wanawake hao wamekutana kupitia jukwaa la mwanamke wa kijijini  mwaka 2021 lililoandaliwa na mashirika mbalimbali yasiyo ya serikali yanayotetea haki za wanawake  likiwemo Tahea, TAWLA, Mviwaarusha na LSF  kwa  uratibu wa Shirika lisilo la serikali la We Effect linalojishughulisha kuboresha makazi ya watu wanaoishi katika makazi duni lenye makao yake jijini Nairobi nchini Kenya kwa kushirikiana na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Wakitoa shuhuda mbalimbali za changamoto ambazo wanakutana nazo vijijini kwenye jukwaa hilo lililobeba Kauli mbiu  isemayo ‘Umiliki wa ardhi ni nyenzo muhimu ya maendeleo kwa mwanamke anayeishi kijijini’ wanawake hao akiwemo Mariamu Daudi kutoka kijiji cha Vilabwa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani, Laurensia Lubigisa mkazi wa Kijiji cha Kabangaja Wilaya ya Ilemela na Ester Masele wa Kijiji cha Mhungwe Wilaya ya Misungwi  Mkoa wa Mwanza walisema  bado wanakabiliwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia pamoja na haki ya kunyimwa kumiliki ardhi  kutokana na mfumo dume ambao bado upo katika baadhi ya jamii zao.

Mmoja wa washiriki wa jukwaa la wanawake wanaoishi vijijini, Mariam Daudi, Mkazi wa Kijiji cha Vilabwa Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani akitoa ushuhuda kuhusu changamoto alizozipata katika umiliki wa ardhi. Picha na Clara Matimo.

Mariamu alisema  yeye kwa sasa anamiliki ardhi kwa jina lake kisheria baada ya kupata elimu kutoka Chama cha wanawake wanasheria Tanzania (TAWLA) lakini awali hakujua kama mwanamke anahaki kikatiba ya kumiliki ardhi kwa sababu kabla hajaolewa akiwa nyumbani kwao hakuruhusiwa kuridhishwa ardhi kwa madai kwamba ataolewa hivyo atamiliki ardhi kwa mume wake lakini baada ya kuolewa mume wake alimwambia hana haki ya kumiliki ardhi kwa sababu ni mwanamke.

“TAWLA imetutoa gizani na kutupeleka kwenye mwanga, imetupa fursa ya kujishughulisha katika kujitafutia mali jamii yetu sasa inauelewa  mkubwa  kuhusu haki ya mwanamke katika  kumiliki ardhi  awali hatukuwa tunajua haki zetu tulikuwa tunanyanyasiki ardhi ilikuwa inamilikiwa na wanaume tu.

“Mwanamke tangu ukiwa nyumbani kwenu  yaani binti kabla ya kuolewa ukiomba wazazi wakukatie eneo lako la ardhi unaambiwa wewe ni mtoto wa kike utaolewa hivyo hauna haki ya kuridhi ardhi hapa ukiolewa pia mume wako anakwambia wewe ni mwanamke tu hauna haki ya kumiliki ardhi, hata akitaka  kuuza au kununua ardhi hakushirikishi na hata akikushirikisha kama ananunua  unakuwa shahidi tu  sio sehemu ya mmiliki,’alisema na kuongeza .

“TAWLA imesaidia sana  kuwabadilisha wanaume zetu, saizi namiliki ardhi yangu na nimejenga nyumba ambayo mume wangu anaifahamu hata baadhi ya wanawake wenzangu wamenufaika baada ya elimu hiyo maana serikali yakijiji ilitukatia ardhi ambayo tunaimiliki kisheria na eneo lingine tunamiliki wote mimi na mume wangu hati za viwanja zina majina na sahihi zetu kwa hiyo na mimi ninahaki kama mume wangu kwenye maamuzi na matumizi ya eneo hilo,”alisema.

Kwa upande wake Laurensia Lubigisa,  alisema baada ya mume wake kufariki  mwaka 2012 ndugu wa mumewe walimpelekea  watoto wawili ambao alikuwa hajawahi kuwaona wakidai kwamba ni watoto wa marehemu hivyo anapaswa awagawia sehemu ya shamba ambalo ndilo analitumia kujipatia chakula kwa ajili ya kujikimu yeye na watoto wake saba.

“Nilikataa kwa sababu  marehemu mume wangu enzi za uhai wake hakuwahi kuniambia kama kuna watoto amezaa nje ya ndoa, nilipokataa nilipewa vitisho kutoka kwa ndugu wa marehemu mume wangu  wakaniambia wataniuwa lakini sikujali, nilitembea nalia kila wakati kwa miaka miwili hadi nilipokutana na Tahea wakaniunganisha na TAWLA ndiyo walionisaidia hadi sasa namiliki shamba hilo,”alieleza Laurensia.

Naye Maria Petrokutoka karatu alisema ingawa vikundi vinawasaidia kupata mikopo kutoka maeneo mbalimbali ikiwemo halmashauri lakini wamekuwa wakikutana na changamoto ya ndoa zao kuvunjika  kwani  baadhi ya wanaume huwaambia  wake zao  wawakopee fedha kwenye vikundi vyao  lakini wakiisha wakopea  hawarudishi na wanachama wanapokuja kuwakamatia vitu walivyoandika kama dhamana ya mkopo wanaume wanawapa takala.

“Ukiishamkopea mwanaume hatoi marejesho ukimwambia anakwambia kwani jina langu liko kwenye  karatasi ya mkopo hata kama unaumwa hauta lala kwa sababu unajua unadaiwa marejesho itakulazimu uinuke ukafanye shughuli ya kiuchumi uliyonayo ili upate marejesho hii nayo ni changamoto ambayo inatukabili wanawake wengi tunaoishi vijijini,”alisema Renada.

 Anna Mbuligwe mkazi wa kijiji cha  uliwa Mkoa wa Njombe, alisema endapo akikutana na Rais Samia Suluhu Hassan, atamuomba aelekeze nguvu zaidi  vijijini kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali yasiyo ya serikali yanayotetea haki za wanawake  kutoa elimu kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia na haki ya wanawake kumiliki ardhi maana  inamchango mkubwa wa kuimarisha ustawi wa amendeleo kwa wanawake na jamiini kwa kuwa bado maeneo mengi wanakabiliwa na changamoto hizo.

Muwakilishi wa Shirika la we Effect nchini Tanzania, Naseku Kisambu, alisema wameamua kuratibu maadhimisho hayo ambayo kitaifa hufanyika Oktoba 15 kila mwaka ili kupata fursa ya kusikia kwa karibu changamoto za wanawake wanaoishi vijijini waseme  taasisi binafsi pamoja na serikali ifanye nini kuboresha hali zao ikiwemo suala zima la umiliki wa ardhi.

“Maadhimisho ya kitaifa ambayo yatafanyika kesho (leo) Oktoba 15 yana kauli mbiu  inayosema’ tujenge ustahimilivu kwa mwanamke anayeishi kijijini katika kukabiliana na Uviko 19’ na sisi tukaona tuwe na kauli mbiu ndogo inayosema  ‘ardhi ni nyenzo ya maendeleo kwa mwanamke wa kijijini’  kwa kuwa mwanamke ana haki sawa na mwanaume katika kumiliki ardhi na kuitumia hata akiwa kwenye ndoa na tumebaini kwamba wanawake wengi  wanaoishi vijijini bado hawana uelewa wa haki yao hii ya kikatiba,”alisema Kisambu.

Mgeni rasmi katika jukwaa hilo, Mwenyekiti wa TAWLA, Lulu Ng’wanakilala, alitoa rai kwa wananchi kutambua kuheshimu, kulinda, kutetea  na kusimamia haki za wanawake wanaoishi vijijini na kuthamini  mchango wao katika kilimo pamoja na kuboresha hali ya kundi hilo na msichana anayeishi kijijini.

“Licha ya ukweli kwamba mwanamke wa kijijini ndiye mzalishaji mkubwa  wa chakula na uchumi bado amekuwa akiachwa nyuma katika mipango ya maendeleo,  kupitia maadhimisho haya naiomba jamii ibadilike na kumuangalia katika mtazamo chanya mwanamke huyu,”alisema.

Akizungumza kwenye jukwaa hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanawake Wanasheria Tanzania (TAWLA), Tike Mwambipile,  alisema lengo la jukwaa hilo ni kusikiliza mikasa na jitihada mbalimbali ambazo wanawake  wanaoishi vijijini wanakutana nayo ili wajifunze na kuanza kuchukua hatua kwa kushirikiana kutatua changamoto wanazokutana nazo  hasa katika eneo la ukatili wa kijinsia.

Alisema maadhimisho ya siku ya mwanamke anayeishi kijijini ambayo yanafanyika kitaifa leo Oktoba 15 Wilaya ya Moshi  mkoani Kilimanjaro yameadhimishwa kwa kutanguliwa na mambo manne ambayo ni msafara wa kijinsia uliotokea Mkoani Mwanza hadi Kilimanjaro ukitoa  elimu kuhusu mambo mbalimbali ikiwemo  haki ya mwanamke katika kumiliki ardhi, kutembea ambapo walitoa ujumbe katika jamii,  jukwaa la mwanamke anayeishi kijijini  lililofanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini na kongamano la kitaifa la mwanamke na ardhi litakalo hitimisha maadhimisho hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Grace Mwangwa,alisemaserikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo itazifanyia  kazi changamoto zilizoainishwa na wanawake hao kupitia jukwaa hilo ili kuboresha ustawi kwa kuwa inatambua mchango mkubwa wanaoutoa katika taifa.

Wanawake waliohudhuria jukwaa hilo wanatoka mikoa ya Mwanza,   Shinyanga, kilimanjaro, Njombe,  Arusha, Manyara, Pwani, Tabora, Tanga, Singida na Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles