30.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE WENGI HAWANYONYESHI KWA UTARATIBU’

Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema licha ya kwamba zaidi ya asilimia 97 ya wanawake nchini hunyonyesha watoto, lakini bado kuna tatizo la wengi kutonyonyesha kwa kufuata utaratibu ulioshauriwa na wataalamu wa afya.

Hayo yalielezwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani na uzinduzi wa mpango wa lishe.

Alisema takwimu za utafiti wa hali ya kidemografia na afya uliofanyika mwaka 2015, zinaonyesha asilimia 59 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wananyonyeshwa maziwa ya mama pekee bila kupewa chakula kingine kama inavyoshauriwa.

“Hii inamaanisha kuwa asilimia 41 ya watoto wenye umri huo hawanyonyeshwi ipasavyo na inawaweka katika hatari ya kupata utapiamlo na magonjwa yanayotokana na taratibu zisizofaa za ulishaji watoto.

“Takwimu zinaonyesha pia asilimia 11 ya watoto wenye umri chini ya miezi sita wanalishwa vyakula vingine vya ziada pamoja na kunyonyeshwa maziwa ya mama, asilimia 4 wanapewa maziwa mengine na asilimia 2 wanalishwa vinywaji ambavyo havina maziwa,’’ alisema Waziri Ummy.

Alisema takwimu hizo zinamaanisha kuwa asilimia 92 ya watoto wa umri chini ya miezi sita wanapewa vyakula ambavyo havina mchanganyiko wa kutosha, yaani mlo usiokamilika na ni sababu za kupata utapiamlo.

Waziri Ummy alisema utapiamlo kwa watoto unachangiwa na sababu nyingi na miongoni mwa hizo ni ulishaji usiofuata taratibu kwa usahihi, ambao huchangiwa na majukumu mengi yanayomkabili mama na hivyo kukosa muda wa kutosha wa kumtunza mtoto.

Alisema kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu inayosema “Sote kwa pamoja tuendeleze unyonyeshaji wa maziwa ya mama’’, ni vyema kila ofisi ya Serikali na binafsi zikatenga maeneo mazuri kwa waajiriwa kunyonyesha kama ilivyokuwa katika ofisi zao za Bunge Dodoma.

Waziri Ummy alisema waajiriwa pia wanatakiwa kufuatisha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004 inayompa nafasi mzazi akiwamo baba na mama kupata wakati wa likizo kwa malezi.

Pia alizishukuru kampuni za simu za Tigo, Airtel, Vodacom na Zantel kwa kutoa huduma bure ya “Wazazi nipendeni” kwa kupitia namba *152*05# kisha namba 2 unapata huduma za wazazi.

Naye Dk. Joyceline Kaganda kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC), alisema lishe bora kwa watoto inasaidia kuwafanya kuwa na akili timamu na kukua vizuri kiafya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles