24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE WATHUBUTU KUKABILI MABADILIKO

LEO  ni Siku ya Wanawake  Kimataifa.  Hii ni siku ambayo imeanza kuadhimishwa miaka mingi lakini bado yapo maswali mengi hasa kutoka kwa wanaume wakijiuliza kwanini iwepo siku ya wanawake?

Historia huwa haidanganyi, historia huweka masuala yaliyositirika bayana.  Hali ya wanawake ulimwenguni kote  katika nyanja mbalimbali kama siasa, afya, uchumi, kijamii na kadhalika imekuwa haziridhishi kabisa. Hali hizo ndio zilizosababisha wanawake kuinuka na kuanza kufanya mambo mbalimbali ya kujikomboa katika makucha ya mfumo unaowabagua, kuwakandamiza na hata kuwaumiza. Tanzania pamoja na uzuri wake bado kuna dhuluma, uonevu, mauaji  kwa watu wasio na hatia kama yanayotokea sehemu mbalimbali nchini na hata ukatili wa kijinsia. Wanawake wakiwa ni jeshi kubwa wanahitaji kuingia katika kufanya jambo litakaloleta mabadiliko chanya kwani wanawake wakipona jamii imepona.

Mwaka huu kimataifa kauli mbiu kwa Lugha ya Kiingereza ni "Be bold For change". Nimejaribu kweli kutafsiri kwa Kiswahili kauli mbiu hii na nikaona pengine tuseme " thubutu kukabili mabadiliko", au ungeweza pia kusema kwa lugha ya kijiweni " Kuwa ngangari kuleta mabadiliko". Hapa nchini tumeangalia kwa mwaka huu ni mabadiliko gani tunayodhani tuyape kipaumbele? 

Tumeona kuwa nchi inaelekea kwenye uchumi wa kati na inajielekeza kuwa nchi  ya viwanda na ili suala hili liwe la  ukweli kwa wanawake ni lazima uchumi  upewe kipaumbele kwa wanawake. Hivyo, uthubutu wa wanawake uwe katika kujielekeza katika mabadiliko ya kiuchumi.  Tunapoangalia uchumi tunaweza kuchukua tafsiri rahisi kuwa ni kila shughuli zinazofanywa na wanadamu, zenye nia  ya kutosheleza mahitaji waliyo nayo maishani. Uchumi huhusisha  uzalishaji, usambazaji na utumiaji  wa bidhaa na huduma zinazowezesha yote hayo.

Kwanini kauli mbiu idai uthubutu? Wanawake ninavyowaona mimi  nikiwa mmoja wao naona wanauthubutu mkubwa sana katika mambo mengi wanayoyafanya.Wakiwa ni walezi wa familia, wakiwa ni wazalishaji wa mahitaji muhimu ya nyumba zao.  Pamoja na hayo bado ni waathirika wakubwa sana pale uchumi unapoyumba. Kikwazo kikubwa kwa hapa kwetu kwa wanawake kufikia kuwa na uthubu katika kufikia mabadiliko ni suala zima la ubaguzi wa kijinsia na ukatili wa kijinsia. Haya mawili yamekuwa na athari mbaya kwa wanawake.

Wanawake wanaweza kuwa wazalishaji wazuri lakini wanaweza wasiwe na uamuzi wa kile walichozalisha. Wanawake wanaweza kuwa na uwezo mkubwa katika kuzalisha  kwa njia ya kazi mbalimbali lakini wakakataliwa kwa sababu tu za kijinsia. Kuna wanawake wengi ambao imebidi waache kufanya kazi zikiwamo za ajira kwa vile tu mume au mzazi ameamua kuwa wasifanye kazi.

Elimu tunayopokea inayo mwelekeo wa ubaguzi kijinsia. Kwa muda mrefu pamekuwa na kazi zinazosemekana ni za wanaume na hivyo wanawake wanaotaka kufanya kazi hizo hushindwa iwapo elimu haikuwaandaa kufanya hivyo.Wanawake wanaopewa elimu  katika masomo ya Sayansi, yanayoweza kuwaelekeza au kuwawezesha kuwa madaktari, wahandisi, mafundi inabidi wawe na uthubutu wa kutosha kuleta mabadiliko katika jamii. Watakueleza wale waliofanya hivyo jinsi ilivyokuwa si rahisi. Hata darasani wanaonekana kama wamekosea.

Huwa  sisahau kabisa siku taarifa ya habari kupitia redio Tanzania Dar  es Salaam wakati huo, iliposomwa na mwanamke. Huyu alikuwa kazini na ndipo alikokuwa akipata kipato chake. Siku hiyo waliosikia wengi walishangaa. Nakumbuka pale nilipokuwa watu wakiulizana "Hiyo ni taarifa habari au hongera mwanangu?" Wengine wakisema  “RTD sasa wanaleta mzaha” Wengine walisema yaani sasa wameshaanza kuonyesha dharau katika vitu vya maana, huu utani" nakadhalika.

Nadhani mwanamke yule aliyesoma taarifa ya habari kwa mara ya kwanza alihitaji uthubutu. Na iwapo alisikia yale yaliyokuwa yakisemwa  na watu huenda angekata tamaa kabisa. Mabadiliko kama haya yalihitaji uthubutu ndio maana sasa hakuna anayeshangaa taarifa ya habari kusomwa na mwanamke..

Tunahitaji kuthubutu ili tuone mabadiliko katika nyanja zote za kiuchumi. Kwa maana ya kuwa wanawake waweze kuwa na fursa katika uzalishaji, usambazaji na hata ulaji. Mifano ya kawaida kabisa ni kuwa katika uzalishaji ni kama nilivyokwisha kueleza hapo juu. Fursa za elimu itakayowawezesha kufanya shughuli za uzalishaji na hizi zinaweza kuwa kazi za mashambani, viwandani na hata maofisini.

Kwenye usambazaji nao pia wawe na mamlaka na uwezo wa kusambaza vile wanavyovipata katika uzalishaji. Pasiwe na vikwazo vya aina yoyote. Lakini pia katika ulaji. Unaweza usifahamu kuwa kuna wakati wanawake wanashindwa kula matunda ya kazi yao. 

Tuna mifano hai ya wanawake wanaofanya kazi na mshahara anauchukua mume au wasichana wanaofanya kazi mshahara anauchukua mzazi. Tumeshuhudia kisa cha mwanamke aliyeunguzwa na maji ya moto kwa kuwa tu aliamua kuchuma mhindi shambani na kuchoma ili ale. Mume hakutaka iwe hivyo kwani hakutoa ruksa.Yeye ndio mtoa ruksa hata kwa mhindi wa kuchoma.

Tukijiangaliza kama Taifa tunaweza kusema tumeshapiga hatua kubwa katika eneo la wanawake kupata fursa mbalimbali zinazoweza kukuza uchumi wao na wa jamii. Hata hivyo bado hatujafikia mahali tunapoweza kusema kama Taifa sasa tumefikia upeo wa mabadiliko katika jamii kuwa wanawake wanaishi bila ubaguzi , bila dhuluma na uchumi wao unakuwa. Hadi sasa bado tuna shida kubwa ya mabinti kutomaliza shule kwa kutolewa ili waolewe.

Na hii inatokea zaidi vijijini. Kuna wazazi wanaodiriki kuwataka mabinti zao wasifaulu mitihani ili wasiendelee na masomo  na wapatiwe waume wa kuwaoa. Ndoa za utotoni haziwezi kuleta wanawake wenye uthubutu hata kidogo.  Suala la ndoa za utoto ni kama tatizo linakutana na ukatili wa kijisia.Wanawake wengi wanakumbana na ukatili wa majumbani.

Takwimu zinaonyesha wanawake sita wa Kitanzania kati ya kumi wameshapigwa na waume zao. Vipigo vinatofautiana. Kuna wanaopigwa kiasi kwamba wanapata ulemavu, wapo wanaopoteza uzazi au kupoteza ujauzito, wapo wanaoshindwa  kufanya kazi kwa muda mrefu kutokana na ukatili wa kijisia.Wengine hufanyiwa ukatili wa kijisia wakiwa makazini mwao.

 Tunapoadhimisha siku hii ya Wanawake Ulimwenguni tujue hakika ipo sababu kubwa kwa wanawake wenyewe kujenga uthubutu ili waweze kuleta mabadiliko yatakayowezesha nao kuvuka kuelekea uchumi wa kati na hasa kufaidi Tanzania ya viwanda.

Mwandishi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles