27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake watakiwa kuchangamkia fursa ya zao la michikichi

 Na Clara Matimo, Sengerema

Katika kuhakikisha wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini wanakombolewa kiuchumi kwa kuwekewa fursa za biashara, kundi hilo limetakiwa kuchangamkia fursa zilizopo kwenye zao la michikichi.

Wito huo umetolewa na Afisa Kilimo wa Kata ya Kahumulo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, Emmanuel Mafuru, kwenye maadhimisho ya kilele cha siku ya wanawake duniani Machi 8, mwaka huu wakati akizungumza na wanawake wa kata hiyo.

Amesema zao la michikichi kuanzia shina, matunda, matawi na  majani vyote humuingizia faida mkulima kwani majani yake hutengeneza mifagio, ni chakula cha mifugo, makutu hutumika kujengea na kuezekea nyumba, pia hutumika kama kuni na kutengeneza fensi wakati moshi wa msoke hutumika kama sumu ya kuuwa mbu  matunda huzalisha vitu vingi ikiwemo maweze yanayotumiwa kama mafuta ya kula  levile ni malighafi ya kutengenezea mafuta ya kujipaka.

“Mbegu inasehemu mbili ganda ambalo nalo hutumika kama kuni na kiini ambacho huzalisha mafuta awamu ya pili yanaitwa mafuta ya mise, mafuta haya ni tofauti na mawese pamoja na sabuni maarufu kama sabuni  za kigoma,” amesema Mafuru.

Aidha, mtaalamu huyo wa masuala ya kilimo alibainisha kwamba mashudu ambayo hubaki baada ya kutoa mafuta ya mise hutumika kama chakula cha wanyama na shina la zao hilo hutengenezea mizinga ya asali pia huzalisha mbao kwa ajili ya kujengea nyumba ambazo haziliwi na mchwa.

Katika kuwawezesha wanawake wa Kata ya Kahumulo, Shirika lisilo la Serikali lenye makao yake jijini Mwanza la Mikono Yetu linalojishughulisha kuwawezesha wanawake na wasichana kumiliki rasilimali zalishi ikiwemo ardhi na mifugo ili waweze kujikwamua kiuchumi lilipanda miche ya michikichi 57 na mipera 27 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho hayo, huku tayari likiwa limeanza ujenzi wa kiwanda cha kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao pamoja na mifugo kinachotarajia kuwanufaisha wanawake zaidi ya 150.

Meneja Programu wa Shirika la Mikono Yetu, Sophia Nshushi,  amesema wameamua kuwawezesha wanawake hao kupanda zao la michikichi kwa sababu lina uwezo wa kutoa matunda kwa kipindi cha miaka 30 mfululizo baada ya kukomaa, pia ni zao kuu la sita la biashara  nchini hivyo litaiongezea serikali na wakulima hao kipato na  kupunguza changamoto ya upatikanaji mafuta ya kula nchini.

“Matarajio yetu ni kupanda miche mingi zaidi ili baada ya miaka mitatu wakianza kuvuna waisaidie serikali kupunguza uhitaji wa mafuta ya kula nchini,  kwa mujibu wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa anazindua zao la michikichi kuwa zao kuu la sita la biashara nchini miaka kadhaa iliyopita kule wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma, uhitaji wa mafuta ni tani 600,000 wakati uzalishaji uliokuwepo  ni tani 42,000 tu ndiyo maana tumeona ipo haja ya kuwahamasisha wanawake hawa watumie fursa hii kujikwamua kiuchumi,”amesema Nshushi na kufafanua:

“Ingawa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani hufikia kilele Machi 8, kila mwaka  lakini Shirika la Mikono Yetu tutaendelea kuutumia mwezi huu wote kwa ajili ya kupanda miche ya zao la michikichi  lengo letu ni kuhakikisha linapata mwitikio mkubwa katika kata hii na afisa kilimo ametuhakikishia kwamba ardhi ya eneo hili inafaa kwa kilimo cha zao hilo.

“Matamanio yetu ni kuona wanawake wa Kahumulo wanatambua  fursa zilizopo kwenye zao la michikichi, tumeanza ujenzi wa kiwand cha kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na mazao pamoja na mifugo  ndiyo maana leo pamoja na kupanda miche pia wameendeleza ujenzi wa kiwanda hicho kwa kupiga lipu tunatarajia kukizindua Oktoba 16, mwaka huu  siku ya maadhimisho ya kitaifa ya mwanamke anayeishi kijijini.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mikono Yetu, Esther Masawe, aliwasihi wanawake kulima kwa wingi zao hilo ili baada ya miaka mitatu watakapoanza kuvuna watumie fursa ya uwepo wa kiwanda hicho ambacho kitaanza uzalishaji Oktoba mwaka huu kujikwamua kiuchumi kutoka wazalishaji wadogo hadi wakati na hatimaye wawe wakubwa.

Baadhi ya wanufaika hao  akiwemo, Fausta Andrea, Yunia Misana na Prisca Berenado, walisema wataitumia vizuri fursa hiyo ili waweze kujikwamua kiuchumi maana wametambua faida nyingi zitokanazo na zao la michikichi.

Mazao mengine ya biashara ambayo yanategemewa na serikali kukuza pato la taifa ni pamba, kahawa, chai, tumbaku na korosho wakati  zao la michikichi lenye mashina 50 hadi 55 kwa ekari moja iliyopandwa mbegu za kisasa inakadiriwa kutoa mavuno ya  tani nne hadi tano sawa na lita 4,000 hadi 5,000, mbegu za kienyeji hutoa tani 1.5 sawa na lita 1,500 za mafuta kwa mvuno mmoja.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles