27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake wasipewe nafasi za upendeleo, wapambane wapigiwe kura

JAVIUS KAIJAGE

Kwa miaka mingi wanawake wengi  wamekuwa wakilalamika kuwa mfumo dume ni chanzo cha wao kuendelea kubaki nyuma licha  ya umuhimu wao katika ujenzi wa familia na jamii nzima kwa ujumla.

Malalamiko haya yasiyokwisha yanayotokana na sababu za kihistoria katika dhana hii ya mfumo dume ndio yamekuwa yakisababisha jamii ya wanawake kitaifa na kimataifa kuendelea kuchukua hatua za kudai haki zao.

Wanawake wamekuwa wakidai haki zao zikiwamo za kiuchumi mfano  kumiliki mali, kurithi mali pamoja na kupata nafasi za kisiasa ili kupata  nguvu ya uongozi itakayowasaidia kuwa na uamuzi katika masuala mbalimbali kuanzia ngazi ya kifamilia, kitaifa hadi kimataifa.

Ni ukweli usiopingika kwamba mapambano haya ya kudai haki ambayo kimsingi yalianzia Ulaya, hayakuwa ya bure bali yameanza kuzaa matunda ikiwamo wanawake kuwa na haki ya kumiliki mali, kurithi na kupata nafasi mbalimbali za uongozi.

Kuanzia barani Ulaya hadi Afrika, mataifa mengi yameanza kutambua umuhimu wa wanawake katika jamii na hivyo kuamua kuwapa nafasi mbalimbali za kiuongozi mfano, Rwanda ni nchi mojawapo ambayo tangu Rais Kagame aingie madarakani, wanawake wengi wamekuwa  wakipewa nafasi za juu kama vile ubunge na  uwaziri.

Si tu Serikali ya Rwanda pekee katika Bara la Afrika iliyofanikiwa kuwatambua na kuwathamini wanawake,  bali pia yapo mataifa mengine yaliyopiga hatua ikiwamo Tanzania ambayo tangu awamu ya tatu iliyokuwa chini ya Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, hadi awamu iliyoko madarakani ya Rais Dk. John Magufuli, wanawake wengi wamekuwa  wakipewa nafasi za juu za uongozi.

Pamoja na mafanikio haya machache ambayo yameanza kwa wanawake kupewa nafasi za uongozi hapa nchini, lakini ipo sababu ya kujiuliza ya kwamba taifa letu linapoelekea katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika miezi michache ijayo je, wanawake wamejipangaje ili kufikia ndoto halisi za kiuongozi?

Je, wanawake wanao mpango kabambe wa kujitokeza kwa wingi ili kuwania nafasi za uongozi wa serikali za mitaa katika maeneo mbalimbali ya nchi ili kutotoa mwanya wa mfumo dume kuendelea kutawala?

 Je, kama wanawake watakuwa wamejitokeza kwa wingi kuwania nafasi hizo za uongozi wamejipanga kimkakati ili kuendesha kampeni kisayansi na hatimaye kupata kura kwa wingi kutoka pande zote za jinsia kwa maana ya wanawake na wanaume ili hatimaye kupata ushindi wa kimbunga?Je,  wanawake ambao kimsingi kwa mujibu wa takwimu za sensa iliyopita ni wengi kuliko wanaume, watakuwa tayari kuwaunga mkono wanawake wenzao watakaojitokeza kugombea badala ya kupigana vijembe na kuoneana wivu kama ilivyozoeleka ili hatimaye kuuzika mfumo dume katika nyanja za kisiasa?

   Je, wanaume ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakishika nafasi mbalimbali za uongozi, watakuwa tayari kuwaachia wanawake wenye sifa za kugombea  nafasi hizo kama njia ya kuupiga teke mfumo dume?

Ni dhahiri ya kwamba katika dunia ya sasa ambayo kimsingi wanawake wengi wamesoma huku wakionyesha uwezo mkubwa katika kusimamia masuala  kadhaa,  hakuna sababu ya kuendelea kuwapa nafasi za upendeleo  kama vile viti maalum bali ni  kuwaacha wapambane katika sanduku la kupiga  kura na hatimaye wapate uongozi kwa kupigiwa kura kuliko kuteuliwa.

 Uchaguzi wa serikali za mitaa mara nyingi huwa ni dira na taswira ya uchaguzi mkuu hivyo, wanawake wakitumia vizuri fursa hii kwa kuwania uongozi kupitia vyama mbalimbali vya siasa na hatimaye kuchaguliwa, itawahamasisha wengine  wengi kujitokeza kuwania uongozi katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles