WANAWAKE wanene na wasomi wanakabiliwa na tatizo la kushika mimba kwa sababu ya kuandamwa na maradhi ya uvimbe kwenye kizazi.
Hayo yameelezwa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Vicent Tarimo, aliyefanya mahojiano ya ana kwa ana na MTANZANIA Jumamosi ofisini kwake, Dar es Salaam hivi karibuni.
Katika mahojiano hayo kuhusu afya ya mama na mtoto, tatizo la ugumu wa kushika ujauzito kwa baadhi ya wanawake pamoja na mambo mengine ya kitabibu, Dk. Tarimo, alisema wanawake wanene na wasomi kupindukia hukabiliwa na tatizo la uvimbe kwenye kizazi na hivyo kushindwa kushika mimba.
Alisema idadi kubwa ya wanawake walio katika hatari hiyo ni wanaoishi maeneo ya mijini ambao hujikuta wakikosa watoto maisha yao yote kwa sababu ya kushindwa kubaini sababu ya kushindwa kushika mimba.
Dk.Tarimo alisema utafiti wa kitabibu umeonyesha kuwa wanawake wanene na wasomi wanakalibiwa na ugumu wa kushika mimba kwa sababu kuu mbili ambazo ni mfumo wa maisha hasa ulaji wa vyakula visivyokuwa vya asili pamoja na kukaa muda mrefu bila ya kubeba ujauzito.
“Tatizo la uvimbe kwenye kizazi kitaalamu hujulikana kama fibroid au mayoma, kwa hivi sasa hali inaonyesha inazidi kuongezeka kwa kasi nchini, idadi ya wanawake tunaowapokea hapa Muhimbili inaongezeka lakini wanawake wanene na wasomi ndio wako katika hatari zaidi,” alisema Dk. Tarimo.
Alisema wanawake wasomi mara nyingi huchelewa kupata ujauzito kwa sababu ya kuzingatia zaidi shughuli za masomo hivyo kuruhusu kushika mimba wakiwa na miaka zaidi ya 20 hadi 30.
Dk. Tarimo alisema mwili wa mwanamke una homoni aina ya ‘estrogen’ ambayo huchochea mwanamke kuota uvimbe katika kizazi cha mama ambaye anachelewa kushika mimba.
“Mfumo wa maisha wa sasa unachangia kwa kiasi kikubwa kwa mfano vyakula lakini pia wanawake kuchelewa kubeba mimba kwa sababu za masomo. Unajua mwili wa mwanamke una homoni iitwayo estrogen hii ndiyo inayochochea uvimbe kuota katika kizazi cha mwanamke anapochelewa kubeba mimba.
“Lakini mwanamke akibeba mimba homoni ya progesterone huzalishwa. Hii huwa inazuia madhara yanayosababishwa na homoni ya estrogen na hivyo kuzuia kuota kwa uvimbe katika kizazi cha wanawake na kwa wanaozaa watoto karibu karibu huwa hawapati kabisa uvimbe huo,” alisema.
Akizungumzia tatizo hilo kwa wanawake wanene, alisema huwa wanapata uvimbe katika kizazi kwa sababu ya ulaji usiofaa wa vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na vile visivyo vya asili.
Alisema ulaji wa vyakula visivyokuwa vya asili husababisha mayai ya mwanamke kushindwa kupevuka kwa sababu ya kuzidiwa na mafuta yaliyo katika vyakula hivyo na aina nyingine ya unene wa wanawake ni wa kurithi kwa familia.
“Hii husababisha mayai kushindwa kupevuka kwa sababu ya kuzidiwa na mafuta yaliyoko ndani ya mwili wa mwanamke na unene pia ni wa kurithi kutoka kwenye familia,” alisema.
Aidha, Dk. Tarimo, aliwashauri wanawake waliojenga utamaduni wa kupima afya zao kila mara ili kujua mwenendo wa afya zao.
“Wengi wanakuja uvimbe ukiwa umekua mno wengine tunawafanyia upasuaji na kuwatoa hadi kilo tano hadi kumi za uvimbe, ni vyema wakawahi hospitalini kupata matibabu,” alisema Dk. Tarimo.