31.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 10, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake wanavyoshawishika kujiunga na ugaidi

Mwandishi wetu

WAKATI dunia zamani ilikuwa ikilia zaidi kwa kukabiliwa na maradhi, njaa na umasikini, sasa hivi kilio kimegeukia kwenye wimbi la makundi ya siasa kali ambayo hujihusisha na uhalifu na ugaidi kwa jina la dini.

Huku kukiwa na taarifa za wanawake kugonga vichwa vya habari kwa sababu ya ugaidi, mara nyingi kinachozungumzwa zaidi huwa ni mchango wao kama wahanga au watu wanaoweza kuwa washirika katika kukabiliana na tishio la ugaidi.

Kinyiume chake, wanawake wanaoshiriki na kuunga mkono itikadi kali wamekuwa wakati mwingine wakipuuzwa. Mtazamo huu ulibadilika wakati msichana mtoro wa miaka 15 Shamima Begum, alipoelezewa kuwa ‘msichana wa maana’ kwa Islamic State baada ya kupatikana katika kambi ya wakimbizi wa Syria.

Miaka minne iliyopita, aliondoka nchini Uingereza na marafiki zake wawili kujiunga na IS, lakini akadai kuwa alikuwa ‘mke tu.’

Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza, alimnyang’anya uraia wa Uingereza, akisema: “Kama unaunga mkono ugaidi, lazima utapata matokeo”. Anatarajiwa kupewa msaada wa kisheria kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Wanawake katika itikadi kali

Kisa cha Begum kimeibua maswali mengi kuhusu uhusika wa wanawake na utashi wao wa kushiriki ghasia zinazosababishwa na itikadi kali katika kundi la IS na makundi mengine.

Uchambuzi wa Rusi analysis unasema kuwa asilimia 17 ya waliopokea mafunzo ya itikadi kali katika Bara la Afrika ni wanawake, huku utafiti mwingine ukionyesha kuwa asilimia 13 ya waliopokea mafunzo ya itikadi kali katika kundi la IS kutoka mataifa ya kigeni waliopo katika mataifa ya Iraq na Syria ni wanawake. Idadi kamili si ya kuaminika na inaweza kuwa kubwa zaidi ya ile inayotajwa.

Tafiti kadhaa zilizoungwa mkono na Rusi na tafiti nyingine zimechunguza nafasi ya wanawake katika makundi ya ugaidi ya kimataifa kama vile IS na al-Shabab, moja kati ya makundi hatari ya kijeshi yanayosababisha mauaji barani Afrika.

Watafiti waliwahoji wanawake ambao walihusika moja kwa moja au kwa njia nyingine katika shughuli za al-Shabab, kubaini ni vipi waliweza kupata mafunzo, na athari walizopata wanawake hao kutokana na kushiriki katika ghasia za itikadi kali.

Kazi hiyo ya utafiti ilifanywa na wasomi wa Kenya, ambao waliweza kutumia uzoefu wao wa muda mrefu na mawasiliano ya jamii zilizobainika kuwa katika hatari ya kupewa mafunzo ya itikadi kali.

IS na al-Shabab

Majukumu waliyopewa wanawake yalikuwa tofauti baina ya makundi hayo.

Wakawake katika kundi la al-Shabab mara nyingi wamekuwa wakifungiwa katika maeneo fulani jambo ambalo linaweza kuwa linatokana na majukumu yao ya kitamaduni, kama wake wa wapiganaji na wasaidizi wa shughuli za nyumbani. Wakati mwingine wamekuwa wakifanywa kuwa watumwa wa ngono.

Wanaweza pia kusaidia katika kuwavutia wajumbe wapya. Utafiti mmoja nchini Kenya ulibaini kuwa wanawake walikuwa wanalaghaiwa na wengine ambao waliwaahidi kuwapatia kazi, msaada wa kifedha na kupewa ushauri nasaha.

kwa mfano, Hidaya (sio jina lake halisi), mmiliki wa saluni, alipewa mafunzo na mteja ambaye alimuahidi kuwa atawekeza na kupanua biashara yake. Alishawishiwa kusafiri katika jimbo la mpakani ambako alitekwa nyara na kupelekwa ndani ya Somalia.

Katika kundi la IS, wanawake huingizwa kwenye kundi hilo hasa kupitia mtandao -na huchangia zaidi katika kuonyesha imani za kundi hilo.

Katika kisa cha Shamima Begum, mwalimu wake alionekana katika propaganda za ushindi wa IS, licha ya madai yake kwamba alipokuwa Syria hakufanya jambo lolote isipokuwa kumtunza mumewe na watoto wake.

Wanawake katika kundi la IS pia wanaruhusiwa kuhudumu kama madaktari na wahudumu wa afya, kwa masharti fulani, ambapo kundi hilo linakikosi kinacholinda maadili ya wanawake.

Hivi karibuni, kundi hilo lilipopoteza maeneo yake katika nchi za Iraq na Syria, limekuwa tayari kuwaweka wanawake katika maeneo ya nafasi za mapigano, likitumia gazeti la Al-Naba kuwaita wanawake kujiunga na jihad na kutoa mkanda wa video mwaka jana, uliowaonyesha wanawake kadhaa wakiwa wamevalia magwanda ya jeshi nchini Syria.

Hata hivyo, tofauti baina ya makundi hayo zimekuwa zikififia kutokana na kila kundi kujifunza kwa kundi jingine.

Nchini Somalia, ambako al-Shabab linajaribu kuanzisha taifa la Kiisalamu linaloongozwa na sheria ya Kiislamu (sharia), matukio ya wanawake kushiriki katika vita na kulipua mabomu ya kujitoa muhanga yamekuwa yakishuhudiwa.

Uchunguzi wa mashambulio ya mabomu ya kujitoa muhanga ya al-Shabab kati ya mwaka 2007 2016 ulibaini kuwa asilimia tano yalitekelezwa na wanawake.

Hali ndivyo ilivyo katika maeneo mengine ya Afrika, kama vile Nigeria ambako kundi la wanamgambo wa Kiislamu la Boko Haram, limekuwa likiwatumia wanawake katika mashambulio ya mabomu ya kujitoa muhanga.

Sababu wanawake kujiunga na makundi ya jihad

Kuna sababu mbalimbali zijnazowafanya wanawake wajiunge na mafunzo ya itikadi kali.

Kwa kiasi fulani, inaonekana kilichowatia hamasa wanaume pia ndicho kinachowavutia wanawake kujiunga na makundi ya itikadi kali, kama vile mvuto wa fikra na faida za kifedha.

Hata hivyo, mbinu zinazotumiwa kuwalenga wanawake pia zilijitokeza, kama vile wito wa kuwataka wanawake warejee katika majukumu yao ya kitamaduni.

Kwa mfano, moja ya utafiti ulibaini kuwa wanaowaingiza watu katika kundi la al-Shabab walicheza na hisia za wasichana wa Kiislam wanaohofia kuwa kuendelea na masomo kutawafanya wachelewe kuolewa ili kuwavutia kujiunga na kundi hilo.

“Kama nikipata mwanamume ambaye atanioa na kunilinda, kwanini nihangaike kusoma au kupata elimu?” mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi aliwauliza watafiti.

Wengine walionekana kuvutiwa na matumaini ya kupata fedha na mafanikio mengine.

Hata hivyo, kufahamu kilichowafanya wajiunge limekuwa ni jambo gumu. Wengi miongoni mwa wanawake waliohojiwa walidai kuwa waliingizwa bila utashi wao.

Kama Shamima Begum, baadhi wanadai kuwa hawakuhusika katika shughuli za kundi, au walishiriki kinyume na utashi wao na baadhi wanasema walikuwa ni waathiriwa.

Japo baadhi huenda walihusika kwa namna fulani katika shughuli za kundi hilo, kukana kuwa waliwajibika ni njia inayowafaa katika kujaribu kurejea katika jamii zao wanaporudi.

Tathmini iliagizwa na BBC kutoka kwa wataalamu wanaofanyia kazi mashirika ya nje.

Martine Zeuthen ni mtaalamu wa maisha ya binadamu na tamaduni zao, ambaye anaongoza mpango unaodhaminiwa na Muungano wa Ulaya Rusi, wenye lengo la kupunguza utoaji wa mafunzo ya itikadi kali na ugaidi katika mataifa ya upembe wa Afrika.

Gayatri Sahgal ni Meneja wa Utafiti katika Taasisi ya Rusi. Huduma ya Royal United. Hii ni taasisi huru iliyobobea katika utafiti wa ulinzi na usalama.

Makundi ya kigaidi Mashariki ya Kati, Ghuba na Afrika:

Dola la Kiislamu Iraq na Syria (ISIS)

Wafuasi wengi wa kundi hili ni waumini wa madhehebu ya Sunni wenye msimamo mkali wa kidini. ISIS imepata nguvu kwa muda mfupi tu na kueneza ushawishi wake katika maeneo yote wanayoyadhibiti nchini Syria na Iraq.

Mwongozo na nadharia yao ni kifupisho cha jina lao – ISIS au Dola la Kiislam kuanzia Iraq, Syria na katika eneo la Sham.

Lengo lake ni kubuni dola kubwa la Kiislam litakaloziunganisha Syria, sehemu ya Iraq, Lebanon na sehemu kubwa ya Palestina na Jordan.

Kundi hili linasemekana kuwa na msimamo mkali zaidi kuliko hata al-Qaida. Sehemu kubwa ya operesheni zake zinagharimiwa na wafadhili binafsi kutoka mataifa ya Ghuba, hasa Qatar na Saudi Arabia.

Vyenzo vyengine vinavyowapatia fedha ni visima vya mafuta kaskazini ya Syria na hongo. Wataalamu wanakadiria kundi hili la kigaidi lina wapiganaji wasiopungua 10, 000 na kwamba limejivunia umashuhuri mkubwa zaidi katika ugomvi kati ya jamii ya Sunni walio wachache na Shia wengi nchini Iraq.

Zaidi ya hayo, ndani ya kundi hilo kuna wanamgambo kadhaa wa kigeni waliojitolea kupigana jihadi, baadhi yao wakiwa ni wale walioslimu.

Al-Nusra Front la Syria

Al-Nusra linaangaaliwa kuwa ni tawi la al-Qaida na jina lake linamaanisha “Waungaji mkono wa umma wa Syria.” Linajulikana kuwa kundi muhimu kabisa la waasi nchini Syria. Malengo yao ni pamoja na kuundwa kwa dola la Kiislamu nchini Syria na katika eneo la Mashariki la Bahari ya Kati.

Al-Nusra inasemekana wafuasi wake wanapatikana zaidi katika eneo la kaskazini mwa Syria, baadae lilitangaza utiifu wake kwa hasimu wake wa zamani, ISIS.

Boko Haram la Nigeria

Jina la kundi hili linamaanisha kwa ufupi kuwa ‘elimu ya Magharibi ni dhambi.’ Wanapigana kwa sehemu kubwa kaskazini ya Nigeria na wanapigania utawala wa Sharia ya Kiislamu kote nchini Nigeria. Wafuasi wake wanajulikana zaidi kutokana na utekaji nyara. Umaskini uliokithiri na ukosefu wa ajira kaskazini mwa Nigeria unawarahisishia kazi viongozi wa Boko Haram kuwasajili wanamgambo wapya.

Vikosi vya usalama vya Nigeria vinapata shida ya kukabiliana na magaidi hao wenye silaha za kila aina. Tangu mwaka 2003, mashambulizi yamekuwa yakifanyika dhidi ya vikosi vya usalama, idara za serikali, makanisa na shule na maelfu ya watu kuuliwa.

Al-Shabab la Somalia

Harakat al-Shabaab al-Mujahideen (HSM) au al-Shabaab (Vijana) kwa kifupi ni kundi la wanamgambo wa Kiislamu lililoundwa kati ya mwaka 2004 na 2006 nchini Somalia, wakati nchi hiyo ikiwa tayari imeshazama katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kundi hilo linapigania kuundwa kwa dola la Kiislamu katika Pembe ya Afrika. Nadharia yao ya itikadi kali ya dini ya Kiislamu haitambui mipaka. Wanafanya mashambulizi katika eneo lote la Afrika Mashariki.

Al-Shabaab wanadhibiti sehemu kubwa ya eneo la kati na kusini la Somalia. Wakuu wa kundi hilo hushirikiana na al-Qaida katika kuwapatia mafunzo wanamgambo. Zaidi ya hayo, kundi hilo lina mafungamano na Boko Haram.

Ansar-al-Sharia la Libya na Tunisia

Wenyewe wanajiita ‘Wafuasi wa Sharia ya Kiislamu’ na kundi hili lina makao yake nchini Libya na Tunisia. Makundi madogo madogo ya Ansar-al Sharia yanapatikana pia kwenye mataifa mengine ya Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Lengo lao ni kuanzisha sheria ya dini ya Kiislamu.

Ngome ya Ansar-al Sharia, tawi la Libya, ipo Benghazi.

Kundi hilo linabebeshwa jukumu la mashambulizi dhidi ya ubalozi mdogo wa Marekani mjini Benghazi, Septemba 11, 2012, ambayo yaliua watu wanne, ikiwa ni pamoja na ubalozi wa Marekani nchini Libya. Ansar-al Sharia linasemekana kuwa na mafungamano na al-Qaida, ingawa wenyewe wanakanusha dhana hizo.

Hizbullah la Lebanon

Kundi la wanamgambo wa Hizbullah nchini Lebanon limeundwa mwaka 1982. Wanajipatia uungaji mkono kutoka mashirika na taasisi za madhehebu ya Shia nchini Iran na Syria. Tawi la kijeshi la kundi hilo linaangaliwa nchini Marekani na katika nchi za Umoja wa Ulaya kuwa ni kundi la kigaidi.

Hamas la Palestina

Vuguvugu la Kiislamu la Hamas limeundwa mwaka 1987. Hilo ni tawi la Chama cha Udugu wa Kiislam katika Palestina. Baada ya Fatah, chama cha kiongozi wa utawala wa ndani wa Palestina, Mahmoud Abbas, Hamas ni kundi la pili muhimu linalowawakilisha Wapalestina.

Kinyume na Fatah, Hamas hawaitambui Israel. Lengo lao ni kuiona dola la Israel linateketezwa. Na ili kulifikia lengo hilo, wanatumia mbinu za kigaidi. Katika miaka ya ’90, walifanya mashambulizi kadhaa ya kuyatolea muhanga maisha nchini Israel.

Tangu mwaka 2007, Hamas ndio wanaotawala katika eneo la Gaza katika wakati ambapo Fatah wanatawala katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Al-Qaida – gaidi wa ulimwengu

Al-Qaida wanajulikana kama mama wa makundi yote ya jihadi ulimwenguni. Jina lake linamaanisha ‘msingi’ ama ‘chanzo kikuu.’ Ndilo kundi lililopanga mashambulizi ya Septemba 11, 2001 dhidi ya Marekani. Lengo lake ni kusimamisha dola la Kiislamu ambalo litayajumuisha mataifa yote ya Waislamu na waumini wa dini hiyo.

Baada ya kifo cha kiongozi wake, Osama bin Laden, al-Qaida sasa inaendeshwa na Aiman al-Zawahiri, ambaye ni mzaliwa wa Misri. Leo hii, mtandao huo una matawi mengine kadhaa yanayojitambulisha nao katika mataifa mbalimbali duniani, kama vile al-Qaida ya Magharibi na Kaskazini mwa Afrika (AQIM), ambayo inaendesha harakati zake kutokea Algeria hadi Mali, na pia tawi lake la Yemen, ambako ni kitovu cha wapiganaji wa jihadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles