26.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, December 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake wanaonyonyesha washauriwa kula milo mitano siku

Renatha Kipaka, Bukoba

Wanawake wanaonyonyesha mkoani Kagera wameshauriwa kula milo mitano kwa siku ili kupata maziwa yakutosha kwa mtoto.

Kauli hiyo imetolewa jana na Ofisa Lishe wa hospitali ya Rufaa Bukoba wakati Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma Mwassa alipofika hospitalini hapo kutoa zawadi mbalimbali kwa mwandishi wa habari Benson Eusace alifanikiwa kupata watoto wanne mapacha ambao bado wapo katika hospitali hiyo chini ya uangalizi wa madaktari.

Ngatunga ameongeza kuwa vyakula anavyopaswa kula mama anayenyonyesha ni kama mbegu za maboga, karanga, korosho, ufuta ambavyo vinapaswa kuongezwa kwenye kimiminika.

Amesema pia mama anatakiwa kupata vyakula vyenye asili ya uchachu kama limau ni vizuri vikachanganywa kwenye supu anayokunywa mama ikiwa ni pamoja na pilipili manga inaongezwa kwenye uji ili kumsaidia mama kuwa na maziwa ya kutosha.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatma aliyebeba zawadi kwa ajili ya kuipongeza familia hiyo ameishukuru hospitali hiyo kwa huduma nzuri waliyoitoa na wanayoendelea kuitoa kwa watoto hao tangu kuzaliwa.

“Natumia nafasi hii kuwashukuru madaktari kwa huduma bora hadi watoto hawa wanaendelea vizuri nami nimefika hapa kwa ajili ya kuwaona watoto wetu wanne na kujua hali zao nimeleta zawadi kwa ajili ya hongera kwa familia hii,” amesema.

Amesema lengo la kupeleka zawadi hizo ni kutambua ugumu na changamoto ambayo anaiona kutokana na watoto hao kuwa wanne kwani ni mtihani kidogo kuwalea licha ya kwamba ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu huku akitoa pole kwa mama wa watoto hao kuumwa na kulazwa katika hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando mkoani Mwanza.

“Kwa upekee mkubwa sana nimeleta nguo za watoto za kutosha, maziwa, magodoro mito na vyandarua na mengineyo kulingana na ugeni huu wa watoto hawa “amesema Mkuu huyo wa mkoa huyo.

Ameongeza kuwa wapo watoto 20 waliozaliwa kabla ya muda mkoani humo, huku katika Wilaya ya Muleba wakishuhudia mama mmoja kufanikiwa pia kupata watoto wanne na wanaendelea vizuri kiafya.

Mwassa amesema kuwa Serikali inajitaidi kuona watoto wote wanapata matunzo mazuri na uangalizi mzuri na kuwapatia maziwa ya mbadala watoto wenye shida ya maziwa ambao pia wanazaliwa kabla ya muda.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya watoto Mike Mabimbi, amesema kuwa watoto hao walizaliwa chini ya kilo 1.5 hivyo wanaendelea vizuri wakiwa wanapatiwa huduma safi na matibabu bora.

Dk. Mabimbi amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Kagera huku akiisisitiza jamii juu ya kuwatunza vizuri watoto wanaozaliwa kabla ya muda (njiti) na kuwa wanahitaji joto zuri, na kufikia uzito unaohitajika.

Pia amesema watoto hao wanatakiwa kunyonyeshwa vizuri huku akiomba kutoguswa guswa wanapokuwa wameruhusiwa kwenda majumbani hadi wapate kibali kutoka kwa madaktari.

Hata hivyo baba wa watoto hao wanne wakiwemo wawili wa kike wawili wa kiume, ameishukuru Serikali mkoani Kagera kupitia Mkuu wa Mkoa huo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, viongozi mbalimbali wa mkoa huo uongozi wa Hospitali hiyo, waandishi wa habari wenzake na jamii kwa ujumla kwa namna walivyomfariji tangu kujifungua kwa mke wake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles