RAMADHAN HASSAN-DODOMA
WANAWAKE waliotelekezwa na waliotelekezewa watoto, wametakiwa kufika katika Ofisi za Ustawi wa Jamii kwenye halmashauri zao ili hatua stahiki zichukuliwe kwa maslahi ya watoto na wao.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Faida Mohammed Bakari (CCM).
Katika swali lake, Faida alitaka kujua tamko na hatua za Serikali kwa kina baba wanaotelekeza watoto wao.
“Wanawake wengi walioachika na wajane, watoto wao hutelekezwa na kukosa matumizi toka kwa baba zao na kusababisha watoto kukosa huduma muhimu na wazazi hao wa kike kuteseka na watoto,”aliuliza Faida.
Akijibu, Dk Ndugulile alisema huduma za matunzo, malezi na ulinzi kwa watoto zinatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 kifungu cha 7 – 9, ambavyo vinatoa majukumu kwa wazazi na walezi wote kuhakikisha wanawalea na kuwatunza watoto wao.
Alisema kifungu cha 14 cha sheria hiyo, kinatoa adhabu kwa mzazi/ mlezi atakayekiuka kifungu hicho, atatozwa faini isiyozidi Sh milioni 5 au kifungo kisichozidi miezi sita, au vyote viwili, faini na kifungo.
Alisema kwa kipindi cha 2018/19 mashauri 11,897 yaliyohusu matunzo kwa watoto na wanawake yalishughulikiwa katika ngazi za Serikali za Mitaa.
“Idadi hii ni ongezeko la asilimia 148 ukilinganisha na idadi ya mashauri 11,815 yaliyopokelewa katika kipindi cha 2017/2018,” alisema.
Alisema ongezeko hilo ni ishara ya kuongezeka kwa hamasa kwa wakinamama wanaotelekezwa kuchukua hatua kwa kufika Ofisi za Ustawi wa Jamii kwa ajili ya utatuzi wa malalamiko yao.
“Niwaombe Ustawi wa Jamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha wanaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hii na kanuni zake ipasavyo,”alisema.
Zebaki ni hatari
Katika hatua nyingine, Serikali imesema kuna madhara ya kiafya na kimazingira katika matumizi ya kemikali ya zebaki kutokana na shughuli za uchenjuaji wa dhahabu.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kaliua,Magdalena Sakaya(CUF).
Katika swali lake Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Serikali inasemaje juu ya kuendelea kutumika kwa madini haya hapa nchini.
“Tafiti zilizofanywa ndani na nje ya nchi zimethibitisha kuwepo kwa madhara ya kiafya, kimazingira, ardhini katika matumizi ya madini ya zebaki kuchenjua dhahabu,”alisema Magdalena.
Akijibu swali hilo, Nyongo alisema Serikali kupitia Wizara ya Madini imechukua hatua mbalimbali katika kukabiliana na madhara hayo kwa kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wanaotumia zebaki katika shughuli za uchenjuaji wa madini ya dhahabu.
Alisema Wizara ya Madini imejenga vituo vya mfano katika maeneo ya Katente wilayani Bukombe, Lwamugasa wilayani Geita na Itumbi wilayani Chunya ambavyo vitatumika kufundisha teknolojia mbadala za uchenjuaji wa madini ya dhahabu zisizotumia kemikali ya zebaki na njia bora za utunzaji wa mazingira kwa wachimbaji eadogo.