24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake waiangukia Serikali wakati wa uchaguzi

CHRISTINA GAULUHANGA Na FERDNANDA MBAMILA – DAR ES SALAAM

WANAWAKE, wameiomba Serikali kuangalia upya utaratibu wa mikutano ya hadhara kipindi cha chaguzi  mbalimbali kwa kuwa baadhi yake imekuwa na lugha chafu na za kejeli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa mkutano  ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kuwajengea uwezo, kuwakabidhi ilani ya uchaguzi sambamba na kuweka mikakati mbalimbali, walisema kipindi hicho lugha za kejeli hasa kwa wagombea wasio na ndoa au wajane, imekuwa ni fimbo ya kuwanyima fursa kwa sababu wengi hukata tamaa kwa kuogopa kutolewa lucha chafu.

Mshiriki  kutoka Kata ya Mshewa Mbeya Vijijini , Sabina  Mwalyego alisemambali ya elimu inayotolewa ya kujitambua, bado rushwa ya ngono inavuma kwa kasi kipindi cha uchaguzi.

“Rushwa ya ngono bado tatizo  kipindi cha uchaguzi kwa sababu ukienda kuomba nafasi ili uteuliwe, kama huna ndoa baadhi ya watendaji au wapiga kura husema kwa vile huna ndoa kubali kujenga uhusiano wa kimapenzi ili upate sifa ya kuwa kiongozi,”alisema Sabina.

Alisema kauli hiyo, huwa inakera kwa sababu baadhi ya wagombea wengine waliolewa, lakini wameume zao wamefariki dunia hivyo kulazimisha uhusiano wa kimapenzi ni kuwanyima haki yao ya msingi ya kugombea.

Alisema ifike wakati wagombea wakakubali kushindana kwa hoja na si kwa matusi ili kupata kiongozi anayetakiwa na mwenye sifa.

Alisema mafunzo ya ulaghabishi yamewaongezea uwezo wa kutambua ukikanyagwa lazima utoe sauti, wanawake ni muhimu kuungana na kuwa na kiu ya kutenda haki pamoja na maendeleo.

Mwenyekiti wa Bodi ya TGNP, Asenny Muro aliwataka wanawake kushirikiana ili ifikapo 2020 washike nafasi nyingi sambamba na wanaume.

Alisema kwa sasa wanawake wana nafasi kubwa za uongozi baada ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na mtandao huo.

Alisema wanawake wengi hivi sasa, wameamua kujitoa kimasomaso  kugombea nafasi mbalimbali za uongozi hali inayochangia kuleta maendeleo kwa haraka kwakuwa wao ndio wabebaji wa majukumu mengi.

Akizungumzia takwimu za mwaka 2014/15 za wenyeviti wa Serikali za Mitaa, alisema wenyeviti walioshinda walikuwa  3, 929 ambapo kati ya hao wanawake walikuwa ni 435 tu.

Alisema Serikali ya vijiji, walikuwa ni 12, 273 wanawake walioshinda ni 225.

“Kwa upande wa wenyeviti wa vitongoji, walioshinda walikuwa 64,621, kati yao wanawake ni 362,”alisema.

Alisema takwimu hizo, zinaonyesha kupanda kwa idadi ya nafasi  kwa wanawake wanaogombea nafasi mbalimbali hivyo ni vema kuendelea kuwajengea uwezo wa kujiamini ili wajitokeze zaidi.

Alisema wanawake wamepewa kitu cha ziada, ndiyo maana hata nchi  ya Rwanda, asilimia 61.3 za wanaoshinda nafasi ya ubunge ni wanawake kwa sababu wamewaamini na wameonyesha kufanya vizuri zaidi.

Mshiriki mwingine kutoka Kata ya Pasua mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, Beatrice Kimambo alisema wanawake wengi wanajiyokeza kugombea lakini lugha za matusi zimekuwa nyingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles