Wanawake TALGWU walia rushwa ya ngono

0
383

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WANAWAKE wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU), wameiomba Serikali kuingia katika kupambana na ukatili kwa mwanamke hasa rushwa ya ngono mahali pa kazi.

Hayo yalielezwa jana jijini hapa na Mwenyekiti wa  Kamati ya ushauri wa wanawake Taifa wa chama hicho, Beatrice Njawa, wakati akisoma risala katika  mkutano wa siku mbili wa viongozi wanawake wa Talgwu kutoka mikoa yote nchini.

Njawa alisema vitendo vya rushwa ya ngono bado vipo katika baadhi ya ofisi na imekuwa ni changamoto kwao, hivyo wanaiomba Serikali kuliangalia jambo hilo kwa umakini.

“Rushwa ya ngono na mfumo kandamizi bado upo kwenye ofisi zetu, kupitia Talgwu tunaiomba Serikali iliangalie jambo hili licha ya kwamba kwa sasa limepungua lakini bado lipo katika baadhi ya sehemu,”alisema.

Alisema changamoto nyingine wanayokutana nayo ni uwakilishi mdogo wa wanawake katika ngazi ya maamuzi hivyo aliiomba Serikali kuweka mfumo wa pamoja kuhakikisha wanawake wanakuwa wengi katika ngazi za maamuzi.

Mwenyekiti huyo alisema changamoto zingine wanazokabiliana nazo ni kusitishwa kwa fao la uzazi, afya na usalama mahali pa kazi huku akitolea mfano baadhi ya sehemu vyoo kutokuwa rafiki kwa wanawake.

Alisema changamoto nyingine ni mfumo wa kuchagua wategemezi katika Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) kutokuwa rafiki kwao kwa kupangiwa watu wa kupata huduma hiyo.

Kwa upande wa Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri Tanzania, Pendo Berege alisema changamoto zote wamezipokea na watazifanyia kazi.

Alisema kwamba suala la uwakilishi mdogo kwa wanawake katika ngazi  za maamuzi  wamelijadili na wamekubaliana kwamba uwakilishi utaongezwa na kuonekana.

“Wanawake tunaweza tupeane sapoti kwa sababu kufika  tunapopataka ni sehemu moja ila kuwa msemaji wa mambo yetu ni jambo lingine, bado tunahitaji kuwa na viongozi wanawake haiwezekani katika vyama vya wafanyakazi 34 halafu tuna Katibu mmoja tu mwanamke,”alisema.

Naye, Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Nchini (Tucta) ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Talgwu, Tumaini Nyamhokya, alisema moja ya jambo wanalojivunia ni kupambana kuhakikisha darasa la saba wanarudi kazini pamoja na punguzo la kodi katika mishahara.

“Tulikaa na Waziri wa Fedha na Mipango vikao kadhaa na baadhi ya mambo yameenda vizuri na yameonekana,”alisema.

Naye, Mwenyekiti wa Talgwu Taifa, Selemani Kikingo, alisema awali kulikuwa kunachangamoto ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake lakini kwa sasa umepungua kutokana na matatizo hayo  kutatiliwa kuanzia  katika ngazi za chini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here