NA VERONICA ROMWALD
– DAR ES SALAAM
CHAMA cha Wakunga Tanzania (TAMA), tawi la Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dar es Salaam, kimepanga kutoa huduma ya upimaji wa saratani ya kizazi na satarani ya matiti bure kwa wanawake.
Hayo yalielezwa jana na Mwenyekiti wa TAMA – Muhimbili, Priscilah Kinyamagoha kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo mwenyekiti huyo alisema upimaji huo utafanyika Agosti 4, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani.
“Pamoja na huduma hizo, pia tutafanya upimaji wa shinikizo la damu, sukari, uzito na urefu, upimaji wa virusi vya ukimwi kwa hiyari, ushauri kuhusu lishe bora, ushauri kuhusu uzazi wa mpango, elimu juu ya unyonyeshaji sahihi kwa watoto chini ya umri wa miaka miwili na elimu juu ya afya ya kinywa na meno,” alisema.
Alisema TAMA itafanya upimaji huo kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI).
“Ikumbukwe kwamba Mei 5, mwaka huu huwa tunaadhimisha Siku ya Wakunga Duniani, lakini TAMA tulisogeza mbele maadhimisho hayo hivyo tutafanya Agosti 5, mwaka huu na tutatoa huduma hizo nilizozitaja,” alifafanua.