26.9 C
Dar es Salaam
Monday, December 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wanawake Kipunguni wadhamiria kusambaza elimu kudhibiti rushwa ya ngono

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital


Baadhi ya wanawake katika Kata ya Kipunguni wamesema wametambua madhara ya rushwa ya ngono hivyo wameibeba ajenda hiyo na kuisambaza kwa wenzao ili kudhibiti vitendo hivyo.

Kupitia mradi wa ‘Wezesha uelewa wa haki zuia rushwa ya ngono ndani ya jamii’ unaotekelezwa na Kikundi cha Sauti ya Jamii Kipunguni, wanawake mbalimbali kutoka katika kata hiyo wamejengewa uwezo wa kuepuka vitendo vya rushwa ya ngono.

Mmoja wa wanawake hao Sea Kazadi (54), amesema baada ya mafunzo hayo sasa ana ujasiri wa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kwamba anaendelea kusambaza elimu kwa wanawake wengine ili kudhibiti vitendo hivyo.

Sea ambaye ni Mwalimu wa Vicoba amesema ana vikundi vyenye wanawake 255 na kila anapokutana nao anawapa elimu ya kupambana na rushwa ya ngono na umuhimu wa kuripoti vitendo vya ukatili.

“Unakutana na mtu anakuambia bila mimi huwezi kupata chochote, niliwahi kugombea uenyekiti wa serikali za mitaa lakini fomu yangu ilibadilishwa mwaka niliozaliwa ikaandikwa ndio mwaka niliomaliza darasa la saba, kwahiyo ilivyopelekwa kwenye kamati ya uteuzi ikaonekana huyu hafai kuwa kiongozi,” amesema Sea.

Naye Mariam Ngomaitala (34) ambaye aligombea nafasi ya viti maalumu katika uchaguzi mkuu wa 2020 amesema mafunzo hayo yamewapa mwanga na chaguzi zijazo watajitokeza kugombea.

“Wanawake wenzangu wanaotaka kugombea wasitishwe na vitendo vya rushwa ya ngono, ikitokea wakakutana navyo watoe taarifa Takukuru kwa kupiga namba 113,” amesema Mariam.

Kwa upande wake Aisha Abdallah (32), amesema kabla hajapata mafunzo hayo hata nyumbani kwake alikuwa akiishi katika mazingira ya mfumo dume kwa kuamini mtoto wa kiume hawezi kufanya kazi yoyote.

“Baada ya mafunzo nilitoa elimu nyumbani kwangu na mpaka sasa mtoto wangu wa kiume anaosha vyombo na kazi zingine na wala hanung’uniki…ametambua anaweza kufanya kazi bila jamii kumbeza,” amesema Aisha.

Mkurugenzi wa Sauti ya Jamii Kipunguni, Selemani Bishagazi, amesema wanawake na wasichana 100 wenye nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kutoka katika Kata ya Kipunguni walipatiwa mafunzo kuhusu rushwa ya ngono na uelewa wa haki.

Mradi huo unaofadhiliwa na Women Fund Tanzania Trust unalenga kuendeleza kampeni ya kuzuia rushwa ya ngono kwa wafanyakazi wa kazi za majumbani na wanawake wenye ndoto za kuwa viongozi, umuhimu wa kuripoti vitendo vya ukatili kwenye mamlaka husika na kudai haki na kuwajibika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles