23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WANAWAKE HUACHA MASOMO CHUONI KWA KUSHINDWA KUDHIBITI FEDHA

Na JOSEPH LINO


WASICHANA wengi huacha masomo ya elimu juu kutokana na sababu za changamoto za masuala ya kifedha.

Nchini Marekani asilimia 52 ya wasichana mwaka jana walishindwa kuendelea masomo ya chuo kikuu kwa sababu  mbalimbali ikiwamo ukosefu wa fedha.

Lakini hilo ni tofauti kwa wavulana ambao kati ya 1,000 wenye umri wa miaka 18 hadi 25 waliofanyiwa utafiti, ni asilimia 41 pekee hukosa masomo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Charles Schwab Foundation, Charles Schwab ambaye alifadhili utafiti huo, anasema ni muhimu vijana wawe wanajiandaa kifedha ili kukidhi baadhi ya gharama zisizotarajiwa pindi wanapokuwa chuoni.

“Kila mtu anahitaji kujua jinsi ya kuanda bajeti ya fedha na kuishi kulingana na uwezo wake. Ni vema kupanga bajeti kwa ajili ya siku zijazo,” anasema Schwab.

Nusu ya watu walioshiriki utafiti huo, waligundua kuwa wanafunzi wengi huwa hawawezi kusimamia fedha zao wakiwa chuo kikuu.

Pia ulibaini kuwa wengi wao hawakupata mafunzo ya usimamizi wa fedha binafsi pindi walipokuwa shule ya sekondari, elimu ambayo ingewasaidia kwa kiasi kikubwa.

Wanafunzi hao waliofanyiwa utafiti wanasema hawakuandaliwa kusimamia fedha zao pindi wanapokuwa masomoni.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 51 ya wanawake walielezea kuwa hawakuwa na utayari wa kusimamia fedha zao, ikilinganishwa na asilimia 39 ya wanaume.

Wanafunzi wengi wa kike huhangaika katika masuala ya kudhibiti fedha, hali inayowafanya washindwe kuamua kujiunga na elimu ya juu.

Asilimia 68 ya wanawake wanasema uwezo wao kifedha ulichangia kufanya uamuzi wa kujiunga na chuo.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 74 ya wanafunzi hawamudu gharama za ziada za kupata uzoefu wa taaluma zao, ikiwamo mafunzo kwa njia ya vitendo bila malipo au kwenda nje kuongeza ujuzi.

Aidha, asilimia 68 ya wanafunzi hao walikuwa wanadai mkopo wa chuo, lakini mmoja kati ya watano walikuwa na wasiwasi kwamba kudaiwa mkopo kunaweza kusababisha kukosa nafasi zingine za kupata fedha za kujiendeleza.

Kwa upande mwingine wa utafiti uliyofanywa na Taasisi ya Public Agenda nchini Marekani inasema sababu kubwa ya wanafunzi kuacha masomo ya elimu juu ni changamoto za kifedha.

Utafiti unasema kuwa wanafunzi wengi ambao wanafanyakazi huku wanasoma, huwa wanapata ugumu wa kujigawa mara mbili – majukumu ya kazi na masomo.

Pia ulibaini kuwa asilimia 31 huwa wanaacha chuo kutokana na kiwango kikubwa cha ada, wakati asilimia 54 wanasema walishindwa kuendelea na masomo kutokana na kuelemewa na majukumu ya kazi na masomo kwa wakati mmoja.

Aidha, wanafunzi wengi pia huacha chuo kutokana na mitindo ya maisha wakiwa chuoni kama unywaji wa pombe kupita kiasi, starehe ambazo husababisha wazazi kususa kutoa ada, kufukunzwa chuo kwa kufeli masomo na hata kuacha wenyewe kutokana na kukosa mwelekeo na washauri wazuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles