RAYMOND MINJA- IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa, Alli Hapi, ameziagiza halmashauri mkoani hapa kuwatoza faini wanaume ambao wake zao wajawazito wanachelewa kuhudhuria kliniki badala ya faini hizo kuwakabili kina mama pekee.
Hapi alitoa maagizo hayo wakati wa kuzindua jukwaa la
mawasiliano ya afya kwa watu wazima mjini Iringa, maarufu
‘naweza’ lenye lengo la kuwajengea uwezo wanawake wenye umri kati ya miaka 18 na 49 kutumia mifumo ya afya.
Alisema kumekuwapo na kawaida ya kuwatoza faini wajawazito mkoani humo wanaochelewa kwenda kliniki wakati wa ujauzito huku wanaume wao wakiachwa wakati wanatakiwa kuwajibika katika kumhudumia mtoto kunzia tumboni hadi anapofika duniani.
Mkuu huyo wa mkoa alisema jukumu la kulea mimba mpaka kujifungua si la mama peke bali ni la wazazi wote wawili hivyo na wanaume wanapaswa kuwajibika kwa kumuhimiza mke wake kwenda kliniki mapema.
“Ninaziagiza halmshauri zote kuanzia sasa, ni marufuku kuwatoza faini hizi kina mama na sasa muanze kuwatoza faini hao wanaume wanaoshindwa kuwahimiza wake zao kwenda kiliniki kwa kuwa jukumu la kulea mimba si la mama peke yake bali ni jukumu la wazazi wote wawili,
hivyo nao wanapaswa kuwajibishwa,” alisema.
Mwakilishi wa mradi wa Shirika la misaada la Marekani (USAID), ’ tulonge afya’ unaoratibiwa na jukwa hilo, Frank Rweikiza alisema umelenga kutoa huduma jumuishi za
afya katika maeneo matano likiwamo VVU/Ukimwi, malaria, uzazi wa mpango, afya ya mama na mtoto na TB.
“Ndani ya jukwaa hili kuna kifurushi kinachowalenga wajawazito na wenza wao kwa lengo la kupunguza vifo kabla na wakati wa kujifungua,” alisema Rweikiza.
Martini Shekinyau wa programu ya uzazi salama
kitengo cha afya ya uzazi na mtoto kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto alisema Tanzania imepanga kupunguza vifo vya watoto lakini bado kuna changamoto kwa wanawake.
Alisema changamoto kubwa ya umbali wa vituo vya afya pamoja na elimu ndogo ya afya ya uzazi vinachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake hao.
Alitoa takwimu za wizara hiyo 2015 -1016 ambazo zinaonyesha wanawake 556 kwa kila vizazi 100,000 nchini hufariki dunia kila mwaka pamoja na watoto wachanga 25 kwa kila vizazi hai 1000.
“Sababu kuu ya vifo hivyo vinavyozuilika kama kutakuwa na taarifa na huduma bora za afya ni pamoja na kutokwa na damu nyingi wakati wa kujifungua, kifafa cha mimba, kuharibika kwa mimba, uchungu pingamizi, upungufu wa damu na uambukizi wa magonjwa mengine,’’alisema Shekinyau.