FRANCIS GODWIN, IRINGA
WAKAZI wa Kata ya Mlowa wilayani Iringa, wameanza kuandika wosia mapema kama kinga ya kuwalinda dhidi ya vitendo vya manyanyaso wajane na watoto wanaowaacha, baada ya kufariki dunia.
Wakizungumza juzi kwa nyakati tofauti, wakati mahojiano maalumu na timu ya tathimini, baada ya mafunzo yaliyotolewa na Shirika na shirika lisilo la kiserikali la Iringa Civil Society Organizations (ICISO –UMBRELLA), chini ya ufadhili wa miradi ya Internews ,USAID na fhi360,wakati hao, walisema kabla ya elimu kutolewa hakuna mwanaume aliyekuwa tayari kuandika wosia.
Mkazi wa Kijiji cha Nyamahana, Daud Ndihungule alisema pamoja na kutokuwa na utalaamu wa kuandika wosia, ameanza kuorodhesha mali zake na kuweka mgawanyo kwa familia yake.
“Nilianza na kuandaa na kumbukumbu ya maisha yangu, niliyozaliwa na kuweka kumbukumbu sahihi ya mke wangu halali ninayeishi nae, idadi ya watoto na mwisho kuandika mali ambazo tunazimiliki.
Mimi,mke wangu na watoto tumeshiriki kuchuma mahali, nimeona ni vizuri nikaweka utaratibu mzuri nikiwa bado niko hai,”alisema Ndihungule
Alisema kabla ya kupata elimu ya haki sawa katika umiliki wa ardhi,mirathi na wosia, wanaume wa kijiji hicho wameonyesha kubadilika kwa kuishi tofauti na wake zao.
Alisema bila kuandika mirathi husababisha migogoro mingi kutokana na mali zinazoachwa.
“Pamoja na kuwa mjane na watoto ndiyo, wanaopaswa kuangaliwa zaidi katika mgawanyo wa mali, mashemeji walikuwa wakichangamkia kuchukua mali za marehemu,”alisema.
Mkazi wa Mafuluto, John Kidanyali alisema bado kuna haja ya asasi ya ICISO kuendelea kutoa elimu mara kwa mara jinsi ya kuwahamasisha wanaume na hata wanawake kuandika wosia.
“ Ujue kijijini tunaishi kama ndugu wa familia mmoja, ukitokea msiba kijiji kizima tunafika kushiriki,wakati wa kumaliza misiba tunashuhudia mambo mengi,”alisema.
Kwa upande wake, mkazi wa Nyamahana, Christina Nzala aliomba elimu kuendelea kutolewa kwa maeneo mengine maana juu ya umiliki wa mali kwa wanawake na watoto.
Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Mafuluto, Ditrick Kaywanga alisema kutolewa elimu hiyo kumepunguza migogoro.
Katibu Mtendaji wa ICISO, Raphael Mtitu alisema shirika lake limekuwa likifanya kazi mkoa mzima wa Iringa.
Alisema lengo la kufanya tathimini ya mafunzo hayo, ni kutaka kujua kama elimu hiyo iliwafikia ama haikuwasaidia lakini walichojifunza ni kuwa elimu hiyo imeweza kuibua hamasa kubwa ya wanawake waliodhurumiwa mahali zao.