GLORY MLAY-DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema wapo katika hatua za mwisho kundaa mpango wa kuwalazimisha wanaume kupima afya zao.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, Dk. Ndugulile, alisema wamepanga kuanzisha kambi vituo vya daladala, migodini na viwanja vya mipira ambako wanaamini watawapata wanaume kirahisi.
Alisema mpango huo umekuja baada ya wanaume wengi kutokuhudhiria kliniki na wake zao wakati wa ujauzito kwa kuogopa vipimo.
Dk. Ndugulile alisema wanawake wamekuwa wakihudhuria kliniki wenyewe na wanapoulizwa kuhusu wenza wao, wanakuwa hawana majibu ya kueleweka, hivyo kuanzishwa mpango huo kutasaidia kupunguza magonjwa mengi kwa kina baba.
“Mpango huo upo katika hatua za mwisho kuhakikisha tunapiga kambi katika maeneo makubwa kuwapima wanaume wote ili kujua afya zao, wamekuwa wazito kufika katika vituo vya afya na wake zao jambo ambalo linaongeza magonjwa kwenye familia.
“Asilimia ndogo ya wanaume wanakuja kupima na wake zao, lakini wanapogundulika kuwa na magonjwa fulani wanakuwa wazito kutumia dawa, hivyo kusababisha wengi kufa mapema na kuacha familia zao hatarini,” alisema Dk. Ndugulile.
Alisema anaamini mpango huo utafanikiwa asilimia 100 endapo wanaume watatoa ushirikiano wa kutosha.