|Francis Godwin, Iringa
Baadhi ya wanaume mkoani Iringa wameomba sheria ya ndoa ifanyiwe marekebisho na kutamka kuwa pale mke anapotelekeza familia asiwe tena mke halali wa ndoa.
Rai hiyo wameitoa jana katika mkutano wa utoaji elimu ya fursa sawa kwa wote na haki za wanawake na watoto wa kike katika umiliki wa mali, ulioandaliwa na Asasi isiyo ya Serikali ya Iringa Civil Society Organization (ICISO) kwa vijiji vya Makifu, Mahuninga na Kisilwa.
Akizungumza kwa niaba ya wanaume katika mkutano huo, mmoja wa wanaume hao, Ally Mdapo amesema baadhi ya wanawake wamekuwa na tabia ya kuzitelekeza familia kwenda mijini ambako hukaa miaka zaidi ya sita.
“Akishakaa muda wote huo anarudi kijijini, kitendo hicho kimesababisha wanaume kuoa mke mwingine na wakati huo huo yeye akirudi anataka atambulike kama mke, tunaomba sheria irekebishwe mwanamke huyu asiwe tena mke halali wa ndoa tofauti na ilivyo sasa,” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya wanawake katika Kata ya Mahuninga wilayani, Iringa mkoani humo waliokuwapo katika mkutano huo, wamesema hawako tayari kurithiwa kwa kuachiwa mali ikiwamo ardhi na nyumba pindi wanapofiwa na waume zao.
“Zamani vitendo vya wajane kulazimishwa kuolewa na ndugu upande wa kiume baada ya mume kufariki lilikuwa kubwa jambo lililosababisha vifo vinavyotakanavyo na magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi.
“Ndugu upande wa kiume wakiona mume wako amefariki mara tu baada ya kuzika unaona mdogo mtu wau kaka mtu anatanguliza koti na kiti nyumbani kwa mjane na baada ya muda analeta sanduku la nguo zake ukipokea koti ama kiti ujue tayari anakuwa mume wako,” amesema mmoja wa wanawake hao, Matrida Myovela.
Kwa upande wake mwezeshaji wa ICISO, Ahazi Sibale, amesema: “Kuhusu wanawake wanaotengana na waume zao na baadaye kurudi, sheria ya ndoa inatambua hao ni wake halali na sheria inamtambua mke halali ni yule aliyeolewa kwa ndoa au wale walioishi pamoja kwa muda wa miaka mitatu na kuachana kwao hadi mahakamani na si vinginevyo, hata hivyo mali zote zilizopatikana wakati huo ni mali za wanandoa hao.”