30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

WANAUME HUATHIRIWA ZAIDI AJALI ZA BARABARANI

NA VERONICA ROMWALD– DAR ES SALAAM


TAKWIMU za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaeleza kati ya watu wanne wanaopata ajali kila siku duniani, watatu huwa ni wanaume.

Inakadiriwa kila mwaka duniani watu wapatao milioni 1.25 hufariki dunia katika ajali, sawa na vifo 3,400 kila siku.

Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Ofisa Mawasiliano wa WHO – Geneva, Elena Alties, wakati alipokuwa akiwasilisha mada katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya usalama barabarani.

Elena alisema kundi linaloathirika zaidi na ajali za barabarani ni watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 29 na kwamba wengi huwa ni watumiaji wengine wa barabara, wakiwamo watembea kwa miguu, waendesha pikipiki na baiskeli.

Alisema asilimia 90 ya ajali hutokea katika nchi zinazoendelea, ikilinganishwa na zilizoendelea, huku ajali zikionekana kusababisha vifo vingi kuliko hata maambukizi ya virusi vya Ukimwi, kifua kikuu na malaria.

Kwa mujibu wa WHO, ajali za barabarani hutokana na sababu mbalimbali, hasa za makosa ya kibinadamu kama vile ulevi, mwendokasi, kutokuzingatia sheria za usalama barabarani, kutokuvaa kofia ngumu na kutokufunga mikanda.

Aidha Elena alisisitiza kuwa ikiwa hatua hazitachukuliwa, hali itakuwa mbaya zaidi ifikapo mwaka 2030 kuliko ilivyo sasa.

“Ajali za barabarani zina athari nyingi kiuchumi, kijamii. Takwimu za Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Tanzania zinaonyesha takriban asilimia 2.8 ya pato la taifa hutumika katika kukabili athari za ajali,” alisema.

Mwanasheria kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini, Gaspar Rwebangila, aliwashauri waandishi kuandika habari za utafiti wa kina kuainisha mambo yanayochangia ajali nyingi kutokea.

“Kwa mfano, fanyeni tafiti kwa nini Tanzania hadi sasa ingawa yapo makubaliano mbalimbali ya kimataifa, hatujayasaini kama hatua ya kukabiliana na ajali,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles