Wanaume 60,000 wafanyiwa tohara Simiyu

0
626
Mratibu wa mradi wa Tohara kutoka IntraHealth Mkoa wa Simiyu Dkt. Kentgen Evarist akitoa mafunzo kwa waendesha pikipiki za kubeba abiria wa Wilaya za Itilima na Meatu.

Derick Milton, Simiyu

Zaidi ya wanaume 60,000 wamefanyiwa tohara salama kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Oktoba mwaka jana hadi Septemba mwaka huu katika Mkoa wa Simiyu ikiwa ni zaidi ya asilimia 100 ya lengo ambalo liliwekwa la kuwafikia wanaume 58,246 kupitia kampeni ya Tohara Kinga.

Hayo yamesemwa leo na Mratibu wa Ukimwi mkoa, Dk Hamis Kulemba wakati wa mafunzo kwa waendesha pikipiki za kubeba abiria (bodaboda) wa Wilaya za Itilima na Meatu yaliyokuwa na lengo la kuongeza uhamasishaji kwa vijana na wanaume kujitokeza zaidi kufanyiwa tohara.

“Kupitia kampeni ya Tohara kinga inayoendeshwa na shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya Afya IntraHealth International kwa kushirikiana na serikali tulikuwa na lengo la kuwafikia wanaume 58,246 lakini tumevuka na kuwafikia wanaume 63,240 sawa na asilimia 109,” amesema.

Amesema kuwa kutokana na Mkoa wa Simiyu kuwa na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi kwa kiwango cha asilimia 3.9, kampeini hiyo ambayo bado inaendelea mpaka 2021 itafanikisha kupunguza kabisa maambukizi mapya kutokana na tohara kuwa kinga kwa zaidi ya asilimia 60.

Mratibu wa Mradi huo kutoka IntraHealth Dk. Kentgen Evarist amesema lengo la mafunzo hayo ni kutaka waendesha pikipiki hao kutumia nafasi waliyonayo kwenye jamii kuhamasisha vijana wengi zaidi wajitokeza kufanyiwa tohara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here