Na Jonas Mushi, Dar es Salaam
WANATAALUMA nchini wametakiwa kuchangamkia fursa ya kwenda kusoma Shahada ya Uzamivu (PhD) kupitia mradi wa DAD ili kupunguza changamoto ya uhaba wa wahadhiri wa vyuo vya elimu ya juu.
Mradi wa DAD ulioanza mwaka 2010/2011 unatekelezwa na Serikali ikishirikiana na Serikali ya Ujerumani, ambao unatoa ufadhili wa kwenda kusoma masomo ya uzamifu kwa wanataaluma 20 kila mwaka nchini Ujerumani.
Wito huo ulitolewa jana na Ofisa Udahili Mwandamizi wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Mahundu Fabian, wakati akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya mkutano na wawakilishi wa wanafunzi wa elimu ya juu chini ya mwamvuli wa Shirikisho la Wanafunzi wa Elimu ya Juu (TAHLISO), kujadili changamoto za kitaaluma na mikopo zinazowakabili.
Alisema pamoja na kuwapo kwa uhaba wa wahadhiri wenye sifa ya kufundisha vyuo vikuu nchini, bado kuna mwitikio mdogo kwa wanataaluma wanaofanya kazi vyuoni kwenda kusoma ili kuongeza taaluma zao.
“Tuliona kwamba wanataaluma hawajiendelezi ili kupata sifa za kufundisha elimu ya juu ambayo ni kuwa na PhD, hivyo Serikali yetu na ya Ujerumani zikaanzisha mradi wa kufadhili masomo ya PhD kwa wanataaluma 20 kila mwaka.
“Tulifanya hivi tukijua pengine tatizo ni fedha lakini pamoja na ufadhili huo bado mwitikio ni mdogo kwani kati ya nafasi 20 zinazotolewa wanajitokeza watu watano hadi 10 tu,” alisema Dk. Fabian.
Alisema moja ya changamoto ambazo wanafunzi hao walizieleza katika mkutano huo ni pamoja na uhaba wa wahadhiri na kudai kuwa kwa kiasi kikubwa wanafundishwa na watu wenye Shahada ya Uzamili (Masters) badala ya PhD.
Alisema wanafunzi hao pia walilalamikia baadhi ya vyuo kutoa mitihani mingi ambayo haijaidhinishwa na TCU suala ambalo ni kosa kisheria.
“Wanafunzi wanatakiwa kufanya mitihani iliyoidhinishwa na TCU pekee na chuo kinachoongeza mitihani vinafanya makosa na tutafuatilia suala hili ili kuvichukulia hatua,” alisema Dk. Fabian.
Kuhusu mikopo, wanafunzi hao walitoa madai yao ya muda mrefu ikiwamo kucheleweshewa fedha za kujikimu,
Akijibu suala hilo, Meneja Mawasiliano wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Omega Ngole, alisema wamekuwa wakijitahidi lakini wakati mwingine matatizo yapo vyuoni.