29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa, wasanii wamlilia Kibonde


Bethsheba Wambura, Dar es Salaam

Muda mfupi baada ya kifo cha mtangazaji wa kituo cha Radio cha Clouds Fm, Ephraim Kibonde, wanasiasa na wasanii mbalimbali wameandika ujumbe mbalimbali kuonyesha masikitiko na kuguswa kwao kutokana na msiba huo.

Kibonde amefariki alfajiri leo Alhamisi Machi 7, jijini Mwanza baada ya kuugua kwa muda mfupi katika mazishi ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Vpindi na Uzalishaji, Ruge Mutahaba, Bukoba mkoani Kagera.

Baadhi ya wanasiasa akiwamo Mbunge wa Kigoma Mjini Zito Kabwe kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, wameelezea masikitiko yao kutokana na kifo cha Kibonde.

Zitto Kabwe
Kupitia ukurasa wake wa Twitter Zitto ameandika; “Nimepokea habari za kifo cha Ephraim Kibonde kwa masikitiko makubwa sana, pole zangu kwa familia ya Clouds kwa msiba huu, kazi ya Mola haina makosa wafiwa wote Mungu awapitishe salama katika mtihani huu mkubwa,”.

Ridhiwani Kikwete
Mbunge wa Chalinze naye ameandika katika ukurasa wake wa Twitter “Umauti ni njia tumetengenezewa ili kujua utukufu wa mwenye ujuzi, anayeumba, kuamsha na kuhukumu, kapumzike ndugu yetu Ephraim Kibonde mwendo umeumaliza,”.

Nape Nnauye
“Jamanii natamani iwe ni ndoto sio kweli,” ameandika katika ukurasa wake wa Twitter Mbunge wa Mtama Nape akionyesha kushtushwa na taaarifa za kifo cha Kibonde.

Anthony Mtaka
Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu ameandika katika ukurasa wake wa Instagram; “Pumzika kwa amani kaka na rafiki yangu Ephraim kibonde, mtangazaji na MC uliyeifanya kazi yako kwa weledi mkubwa sana, ndani ya nyumba yetu hatutakusahau maana wewe ndiye uliyekuwa Mshereheshaji ‘MC’ wa harusi yetu.
“Natoa pole kwa familia ya Clouds Media kwa kuondokewa na mmoja kati ya watangazaji nguli ambaye kazi yake iliongeza hamasa ya wafuatiliaji wa vipindi vyenu,”.

Maria Sarungi
Naye mwanaharakati Maria Sarungi Tsehai ameandika katika ukurasa wake wa Twitter “Pumzika kwa amani Ephraim Kibonde, inahuzunisha sana, umeondoka mapema mno, Mungu ailaze roho yako mahala pema peponi,”.

Nao baadhi ya wasanii akiwamo Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz na Ali Kiba, wametuma jumbe kuelezea walivyopokea taarifa za kifo cha Kibonde.

Diamond
Katika ukurasa wake wa Instagram ameandika “Pumzika kwa amani Kaka.”

Ali Kiba
Katika ukurasa wake wa Twitter “Tumshukuru sana hatuna jinsi Mungu ana mambo yake pumzika kwa amani Kaka.”

Masanja Mkandamizaji
Masanja ameandika katika ukurasa wake wa Twitter; “Kuna siku kubwa katika kifo, juzi kaka yetu Ephraim Kibonde alikuwa MC katika msiba wa kaka yetu Rugemalira leo hatunaye, Ee Mungu tujalie moyo wa tafakari na shukrani katika yote, ukawafariji zaidi familia ya Kibonde hasa watoto wake ambao siku si nyingi walimpoteza mama yao.

Lady Jay Dee
Mwanamuziki Judith Wambura maarufu Lady Jay Dee naye ameeonyesha kushtushwa na taarifa za kifo cha Ephraim Kibonde na ameandika katika ukurasa wake wa Instagram; “Hili ni jambo zito kwa watu wenye ukaribu na Kibonde, tunakaa tunakunywa, tunacheka siku nyingine mmoja wetu anatwaliwa, Mwenyezi Mungu wa rehema ukawafariji watoto, ndugu, jamaa na marafiki kwa pigo hili, tunashukuru kwa kila jambo, pumzika kwa amani ‘Brother’ (Shemeji).

Baada ya kupokea taarifa hizi wafanyakazi wenzake na Kibonde kutoka Clouds Media Group akiwamo mtangazaji Gardner Habash (Captain) ambaye walikuwa wakitangaza pamoja kipindi cha Jahazi kwa masikitiko wameandika jumbe katika kurasa zao kulezea hisia zao juu ya kifo cha mwenzao.

Gardner
“Mungu nakuomba nisaidiae, nielekeze nifanyeje Baba muumba,” ameandika kwa masikitiko katika ukurasa wake wa Instagram.

Mwili wa Kibonde unarajiwa kuwasili leo saa nne usiku kutoka jijini Mwanza na kupokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kisha kupelekwa na kuhifadhiwa katika Hospitali ya Lugalo na baada ya taratibu za mazishi kukamilika ataagwa na kuzikwa Jumamosi Machi 9, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles