27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WANASIASA WAKENYA WAMIMINIKA KWA WAGANGA TANZANIA

NAIROBI, KENYA


WAKATI Uchaguzi Mkuu wa Kenya ukizidi kukaribia, idadi ya wagombea kutoka kaunti za Migori na Homa Bay wanaosafiri kwenda Tanzania kusaka huduma za waganga wa kienyeji imeongezeka.

Wanasiasa hao wanaowania viti mbalimbali, wamekuwa wakisafiri hadi miji ya Tarime, Musoma na Mwanza kutafuta msaada wa 'nguvu za giza’ kuwawezesha kupata ushindi bila jasho katika uchaguzi huo wa Agosti 8.

Inadaiwa waganga hao wamekuwa wakiwapa wanasiasa hirizi wanazodai kuwa na uwezo wa kuwapokonya wapinzani wao wapigakura.

Wengi wa wanasiasa hao walianza kumiminika nchini Tanzania Februari, mwaka huu kabla ya kuanza michujo ya wagombea ndani ya vyama.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na gazeti la Taifa Leo la hapa, wanasiasa hao wanaamini waganga wana uwezo wa kuwahakikishia ushindi katika kinyang’anyiro cha Agosti.

“Wengi wa wanasiasa hao wanaamini kuwa hawawezi kupata ushindi bila msaada wa nguvu za giza. Tumekuwa tukiwaona wengi wao wakipitia hapa na kuingia Tanzania,” alisema George Ogwang’ ambaye ni wakala wa ukaguzi wa mizigo katika eneo la mpakani la Isebania.

“Ninamjua mmoja wa wanasiasa ambaye alipata huduma za waganga hawa na bado akabwagwa kwenye mchujo,” aliongeza.

Mohammed Yaya ambaye ni mganga wa jadi mjini Tarime, aliliambia Taifa Leo kwamba ni kawaida kwa biashara kunoga kila mara Kenya inapokaribia Uchaguzi Mkuu.

“Wao huja kupata huduma zetu na wanalipa fedha zozote ambazo tunawatoza,” alisema.

Wasaidizi wa karibu wa wanasiasa mbalimbali, walikiri kuwa waajiri wao huamini waganga wa kienyeji.

Huchukua saa nne kusafiri kutoka Migori hadi Mwanza, lakini ni dakika 50 tu kwa gari la binafsi kusafiri hadi Tarime.

Yaya alisema kuwa wanamtoza mwanasiasa kiasi cha fedha kulingana na kiti ambacho anawania, lakini kiasi hicho wakati mwingine hufikiwa kwa makubaliano.

Utumiaji waganga ulianza wakati wa ujio wa demokrasia iliyoruhusu vyama vingi na visa hivi vimekuwa vikiripotiwa katika kanda zote za nchi wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu.

Novemba 1994, Waziri wa zamani, Musikari Kombo, alipoteza kiti chake cha ubunge wa Webuye baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kutumia waganga kushinda uchaguzi huo.

Kiongozi huyo wa zamani wa chama cha Ford-Kenya, alishtakiwa kwa kuwalipa waganga wawili ili kuwapa wapigakura kiapo kinachojulikana kwa lugha ya Kibukusu kama 'khulia silulu’, yaani kula kitu chenye uchungu.

Kicheko kilizuka mahakamani wakati maelezo ya jinsi kiapo hicho kilivyotolewa mbele ya majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles