28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Wanasiasa hawa wanajifua kumkabili rais Trump

HASSAN DAUDI NA MITANDAO

UMEBAKI mwaka mmoja kabla ya Marekani kuingia katika Uchaguzi Mkuu. Tayari wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema Rais Donald Trump atakuwa na kibarua kizito kurejea Ikulu kwa awamu ya pili ya uongozi wake ulioanza mwaka 2016.

Duru za kisiasa zimejiridhisha kwamba kuna wanasiasa takribani 40 kutoka chama kikuu cha upinzani, Democrat, ambao watawania kiti cha Urais dhidi ya Trump.

Hata hivyo, kwa utafiti wa kina, duru hizo zimedai kwamba wagombea 21 wanaweza kumpa wakati mgumu kiongozi huyo. Je, ni akina nani hao na ni tishio kiasi gani kwa Trump?

John Delaney

Huyo ni Mbunge wa Jimbo la Maryland, ambalo lina wilaya sita. Yuko mstari wa mbele katika wale wanaoitaka nafasi ya kukabiliana na Rais Trump.

Katika mahojiano yake na gazeti la New York Times, mwanasiasa na mfanyabiashara huyo alitangaza nia yake hiyo. “Nafikiri mimi ni mtu sahihi kwa kazi hiyo. Njia pekee ya kulifanikisha hilo, ni kupambana kuliko mwingine yeyote,” alisema Delaney.

Oprah Winfrey

Umashuhuri wake unatokana na kazi yake ya utangazaji wa vipindi vya televisheni na mabilioni ya fedha aliyonayo kutokana na biashara zake.

Winfrey ni kipenzi cha wanachama wa Democratic na kuna uwezekano mkubwa wa kukabidhiwa tiketi ya chama hicho kukabiliana na Trump hapo mwakani. Wamekuwa wakimtumia katika kampeni kutokana na umaarufu na ushawishi wake, hasa kwa wanawake.

Licha ya kukanusha mara kwa mara kuwa hana mpango na kiti hicho, wafuatiliaji wa siasa za Marekani hawasiti kusema anaweza kushawishika miezi michache ijayo.

Tom Steyer

Wengi wanakumbuka alichokifanya katika chaguzi zilizofanyika mwaka jana, ambako bilionea huyo alitumia Dola za Marekani milioni 110 (zaidi ya Sh bil 250 za Tanzania) kukisaida Chama cha Democratic.

Hivi karibuni, akihojiwa na chombo kimoja cha habari, alishindwa kukataa nia yake ya kukitaka kiti cha urais na kusema atatangaza uamuzi wake juu hilo miezi michache ijayo.

Hillary Clinton

Mwanamama huyo pia anapewa nafasi kubwa ya kurejea kupimana ubavu na Trump na tayari kuna mpango wake wa kuzunguka nchi nzima akiwa na mumewe, Bill Clinton.

Pia, kitabu chake kipya kilichoelezea namna alivyopoteza nafasi ya kuingia Ikulu mbele ya Trump mwaka 2016 ni ishara tosha kwamba anataka kujaribu tena.

John Kerry

Aliwahi kuwa Katibu wa Ofisi ya Rais na hivi karibuni alisema hajawahi kuupa kisogo uwezekano wa kugombea kiti cha urais hapo mwakani.

“Natakiwa kulifikiria hilo? Ndiyo, nitalitafakari,” alisema Kerry na kuongeza kuwa hajaanza mkakati wowote wa chinichini kuutafuta mlango wa Ikulu.

Kirsten Gillibrand

Kwa sasa ni Seneta wa New York na katika moja ya hotuba zake za hivi karibuni, alionesha wazi kuwa anataka kumng’oa Trump katika kiti cha urais.

“Nimetembelea jimbo langu, nimezunguka nchi nzima. Nimeona namna Rais Trump alivyotugawa kwa misingi ya chuki. Hiyo imenishawishi kupambana niwezavyo kurudisha heshima ya nchi hii,” alisema.

Chris Murphy

Taarifa zimedai kuwa Seneta huyo wa Jimbo la Connecticut ameuanza kimyakimya mchakato wa kuisaka Ikulu mwaka 2020. Katika mahojiano yake ya hivi karibuni, Murphy amekuwa akimkosoa waziwazi Rais Trump, akisema uongozi wake ni wa ovyo kabisa.

Robert Casey Jr

Baada ya kuwa Seneta wa Pennsylvania kwa awamu tatu, sasa mwanasiasa huyo haoni sababu ya kutokabiliana na Rais Trump mwakani. Alichokisema ni kwamba anahisi ana jukumu zito la kwenda Ikulu kurekebisha madudu yaliyofanywa na Trump. “Ngoja tuone,” alisema.

Michael Bloomberg

Tishio jingine kwa Rais Trump ni bilionea huyo. Trump mwenyewe aliwahi kusema angependa apewe Bloomberg hapo mwakani, lakini ukweli ni kwamba hakitakuwa kibarua chepesi kwake.

Bloomberg anataka kwenda Ikulu na anakubalika ndani ya Democrat. Hata hivyo, mwanasiasa huyo anakabiliwa na kashfa mbalimbali wakati akiwa Meya wa Jiji la New York, jambo linaloweza kumfanya awe mwepesi kwa Trump.

Eric Holder

Aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sasa anakitaka kiti cha urais. Katika mahojiano yake na mtangazaji maarufu wa vipindi vya televisheni, Stephen Colbert, alisema anavutiwa na mpango huo. Wakati wa kampeni za chaguzi ndogo za mwaka jana, alishiriki kwa kiasi kikubwa kuwanadi wagombea wa Democrat.

Mitch Landrieu

Ni wiki chache tu zimepita tangu alipoonekana na Rais aliyempisha Trump, Barack Obama, ikielezwa kuwa walikutana kujadili mustakabali wa Chama cha Democrat. Kwa sasa, mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 58, ambaye pia ni msomi wa sheria, ni Meya wa New Orleans.

Terry McAuliffe

Aliyekuwa Gavana wa Virginia, McAuliffe, naye anataka kuiwakilisha Democratic kumkaba koo Rais Trump ifikapo 2020.

Katika hotuba aliyoitoa akiwa katika ziara yake katika Jimbo la Lowa mwishoni mwa mwaka jana, alisema hawezi kupuuzia ndoto ya kuwa Rais wa Marekani.

Sherrod Brown

Ushindi kwa awamu tatu mfululizo katika Jimbo la Ohio umempa jeuri Seneta Sherrod Brown, ambaye amesema anahusishwa na mpango wa kuitaka Ikulu. Huku akiwa mkosoaji mkubwa wa Rais Trump, anachojivunia mwanasiasa huyo ni ushawishi wake kwa wafanyakazi na umaarufu mkubwa wa mkewe ambaye ni mwandishi wa habari.

Julian Castro

Kama kuna mwanasiasa asiyeficha kwamba anataka kwenda Ikulu mwaka 2020, basi ni Castro. Akihojiwa na televisheni ya MSNBC, alisema: “Kuna uwezekano mkubwa wa kugombea urais.”

Meya huyo wa zamani wa Texas alisema ataweka wazi rasmi ndoto yake hiyo mwishoni mwa mwaka jana, lakini hadi 2019 inaingia hakuwa amefanya hivyo.

Elizabeth Warren

Seneta huyo wa Massachusetts amekuwa mkosoaji mzuri wa uongozi wa Rais Trump, ukiwamo utemi wake dhidi ya wahamiaji na waumini wa Dini ya Kiislamu.

Mwanamama huyo ni mmoja kati ya wasomi wenye heshima kubwa Marekani, akiwa na historia ya kufundisha masomo ya sheria katika Chuo Kikuu cha Texas, Chuo Kikuu cha Pennsylvania na Harvard.

Kamala Harris

Anaushikiliwa wadhifa wa useneta katika Jimbo la California na pia ni mwendesha mashitaka. Ni Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya India kukalia kiti hicho katika historia ya Marekani.

Tayari mwanamke huyo ametajwa kuanza kukutana na wahisani mbalimbali kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kumwezesha kuingia Ikulu mwaka 2020.

Endapo atampiku Trump, basi Harris atakuwa mwanamke mweusi wa kwanza kuwa Rais wa taifa hilo lenye nguvu duniani. Wengi wanaitaja hiyo inaweza kumwongezea mvuto kwenye vyombo vya habari.

Cory Booker

Miezi michache iliyopita, alikaririwa katika mahojiano yake na waandishi wa habari akisema hakuna kitakachoweza kumzuia kugomea urais mwaka 2020.

Katika kile kinachoakisi tamaa yake ya kwenda Ikulu, Seneta huyo wa New Jerseys amekuwa akizunguka katika majimbo mbalimbali, ikielezwa kuwa ni mbinu ya kuanza kutafuta ‘sapoti’.

Eric Swalwell

Licha ya wote waliotajwa kuwa na ushawishi, mwakilishi huyo wa California anaweza kuwa zaidi yao. Inaaminika kuwa kuna asilimia kubwa ya Democrats kumpa ‘kijiti’.

Ni kweli ana umri mdogo, miaka 37, lakini ni maarufu mno kwa nguvu ya ushawishi aliyonayo. Kuna taarifa kwamba miezi michache ijayo atatangaza nia.

Bernie Sanders

Kwa wanaofuatilia siasa za Marekani, watakumbuka kuwa Seneta huyo wa Vermont alikuwa kwenye kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2016, lakini alizidiwa kete na Hillary Clinton, ingawa wengi waliona ni yeye ndiye angeweza kumgaragaza Trump.

Akiwa na umri wa miaka 77 kwa sasa, amesema yuko vizuri na ametamba kuwa yeye ndiye anayeweza kumlaza mapema Rais Trump katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Beto O’Rourke

Jina lake katika ulingo wa siasa lilipaa kwa kasi mwaka 2016 alipoteuliwa kugombea ubunge wa Texas dhidi ya Ted Cruz wa Republican.

O’Rourke hakushinda, lakini wengi walivutiwa na hotuba zake na tangu hapo akawa mmoja kati ya marafiki wakubwa wa Rais Obama. Ameahidi kutangaza nia miezi michache ijayo.

Joe Biden

Kwa awamu mbili mfululizo, alikuwa makamu wa rais wa Obama, lakini hiyo haitoshi kumnyima hamu ya kwenda kuwa na sauti ya mwisho pale Ikulu.

Inaelezwa kuwa si tu wenzake ndani ya Democratic, pia ana mshabiki wake kule Republican.

Akiwa na umri wa miaka 76, minne zaidi ya aliyonayo Trump, Biden amesema ni mkubwa kuliko kiongozi huyo, hivyo anaweza kuiongoza vizuri Marekani kuanzia mwaka 2020.

“Nafikiri mimi ndiye mtu mwenye vigezo zaidi kuwa Rais wa nchi hii,” alisema na kusisitiza kuwa ana uzoefu mkubwa na kazi za Ikulu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles