23.2 C
Dar es Salaam
Monday, February 6, 2023

Contact us: [email protected]

WANASHERIA NCHINI WAVURUGANA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WANACHAMA wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), wameonekana kuvurugana baada ya baadhi yao kufungua kesi Dar es Salaam na Dodoma, wakipinga uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Machi 18, huku baadhi ya wagombea urais wakisema kufunguliwa kwa kesi hizo ni njama chafu.

Hali hiyo imekuja wakati Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harison Mwakyembe, ambaye pia ni mwanasheria na mwanachama wa TLS, mara kadhaa akisema Serikali itakifuta chama hicho endapo kitajiingiza katika siasa.

Kujiingiza katika siasa anakokuzungumzia Dk. Mwakyembe, kunatafsiriwa kuwa ni endapo Mbunge wa Singida Mashariki na Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayegombea urais wa chama hicho, atachaguliwa.

Wanachama wa TLS waliofungua kesi hizo dhidi ya chama hicho na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ni Godfrey Wasonga na Onesmo Mpinzile.

Wasonga alifungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakati Mpinzile alifungua katika Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma na wote kwa pamoja wanaomba mahakama itoe amri ya kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo.

Jana Lissu na Waziri wa Mambo ya Ndani wa zamani, Lawrance Masha, walizungumza na vyombo vya habari wakisema wanatarajia kuwasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na Dodoma zilipofunguliwa kesi hizo, waombe kuunganishwa katika kesi hizo za kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.

 “Tunanunua kesi, hivyo kati ya leo (jana) na Jumatatu tutapeleka maombi Mahakama Kuu Dar es Salaam na Dodoma tuunganishwe kama wadaiwa, tuna wasiwasi kuna njama na uchaguzi ukizuiliwa masilahi yetu yatakuwa yamevurugwa.

“Wasonga ni mgombea katika uchaguzi huu (anagombea ujumbe wa Baraza Kuu la TLS), yeye na Mpinzile pia ni wanachama wa CCM, hivyo na wao wameingiza siasa katika uchaguzi huu,” alisema Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Alisema mambo yanayojitokeza katika uchaguzi huo yanawashangaza wengi kwani hayakuwahi kutokea tangu kuundwa kwa TLS mwaka 1954.

“Serikali imejiingiza moja kwa moja katika uchaguzi huu na haijawahi kutokea kwa wanachama kupinga mahakamani. Kuwa kiongozi wa chama au bungeni, vyeo vyote hivyo havina maana unapofikia uchaguzi wa uongozi TLS.

“Hoja ya msingi ni kuwa mwanachama mwenye sifa za kugombea, hivyo matamko yote yanayotolewa yako nje ya utaratibu na sheria iliyounda TLS na kanuni zake kuhusiana na uchaguzi,” alisema.

Alizitaja baadhi ya sifa za kugombea ni kuwa mwanachama wa TLS kwa zaidi ya miaka 10, kuwa wakili wa kujitegemea, kulipa ada za uwakili, kulipa kodi za Serikali na kuwa na leseni ya biashara.

Lissu alisema wao ni wagombea halali kwa sababu hata kamati iliyoundwa kusimamia uchaguzi huo, ilijiridhisha kwamba wana sifa na wanakidhi vigezo vilivyopo.

“Masuala ya uongozi na chama hayatambuliwi kabisa na sheria iliyounda TLS. Hatumuhitaji Dk. Mwakyembe (Waziri wa Sheria na Katiba), Rais Dk. Magufuli ama mtu yeyote, bali kamati na wanachama ndio waamuzi pekee.

“Hofu ya Mwakyembe ni ‘totally unfounded’ na anatakiwa afahamu kwa sababu ni daktari wa sheria,” alisema Lissu.

 

LAWRANCE MASHA

Masha ambaye pia anagombea urais katika chama hicho, alisema kitendo kilichofanywa na wanachama hao kwenda kufungua kesi, ni kinyume na taratibu za TLS ambazo zinaelekeza mwanachama mwenye malalamiko kuyawasilisha kwanza kwenye chama na asiporidhika ndipo aende mahakamani.

Alisema wanachama hao walikuwa na nafasi ya kuweka pingamizi dhidi ya wagombea walioteuliwa na kwamba hadi Februari 15 ambayo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho, hakukuwa na mwanachama aliyejitokeza kupinga.

“Hakuna anayegombea kutokana na sababu za kisiasa, kama kungekuwa kuna njama isingekuwa rahisi mimi na Lissu tuchukue fomu. Nawashangaa sana mawakili wenzangu waliojitokeza kupinga uchaguzi huu.

“Tuna taratibu zetu ndani ya TLS na kuna wengine wameamua kuzifuata wamepeleka malalamiko yao kwenye sekretarieti. Kuwa CCM, Chadema au TLP si kigezo cha kukatazwa kugombea na hilo tutalipigania,” alisema Masha.

Kwa mujibu wa Masha, malalamiko yaliyowasilishwa na wanachama hao kwa kufuata utaratibu, yanahusu utaratibu wa uchaguzi, jinsi TLS inavyoshirikiana na Chama cha Wanasheria Afrika Mashariki na suala la ada.

 

FRANCIS STOLLA

Akizungumza na MTANZANIA, Francis Stolla ambaye pia ni mgombea urais katika chama hicho, hakukubali wala kukataa kuunganishwa katika kesi hiyo badala yake alisema atafanya uamuzi baada ya kupitia hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani.

“Nimepata tetesi kwamba kuna mashauri yamefunguliwa mahakamani, lakini sijapata hati za shauri kujua nini kinachodaiwa. Nikipata hati ndio nitaomba kujiunga au la,” alisema Stolla.

 

HOFU YA KUFUTWA TLS

Masha alimtaka Dk. Mwakyembe kuwa muwazi na kueleza hofu aliyonayo badala ya kutoa matamshi yasiyoeleweka.

“TLS iko katika mfumo mzima wa utawala, suala la kuifuta itabidi liendane na kurekebisha sheria nyingi na katiba yenyewe.

“Tishio hili ni kubwa na ukiifuta TLS mfumo mzima wa utendaji haki hautawezekana na hakuna yeyote yule atakayejiita wakili msomi.

“Sisi ni wanasheria na tunajua sheria, tungetaka kuwa chama cha siasa tungeenda wenyewe, hatuhitaji ushauri wao, hivyo wasitupotezee muda,” alisema Masha.

Akifafanua kuhusu mfumo wa utendaji haki, alisema makamishna wa viapo ni lazima wawe wanachama wa TLS, Tume ya Utumishi wa Mahakama, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Tume ya Kurekebisha Sheria lazima ziwe na wajumbe kutoka TLS.

Uchaguzi wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Machi 18 jijini Arusha na utatanguliwa na mkutano mkuu utakaofanyika Machi 17.

 

DK. MWAKYEMBE

Hivi karibuni, Dk. Mwakyembe akizungumza na wageni wa TLS waliomtembelea ofisini kwake mjini Dodoma, alisema: “Kama wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu.

“Hatuna nia ya kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa sheria yenu iko chini yetu, mkiharibu kwa lolote wizara ndiyo yenye wajibu wa kuwatolea maelezo katika hilo mnalotaka kulifanya, sasa kuna mgongano wa masilahi je, ninyi kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?”

Mbali na Lissu, Masha na Stolla, wagombea wengine wanaowania urais wa TLS ni Godwin Mwapongo na Victoria Mandari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles