22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

WANASAYANSI WATENGENEZA MJI BANDIA WA MIMBA

Na JUSTIN DAMIAN

WANASAYANSI nchini Marekani wamefanikiwa kutengeneza mji bandia wa mimba (uterus) utakaowezesha watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao (extremely pre mature) kukua na kuishi wakiwa na afya njema.

Kifaa hicho ni tofauti na vifaa vilivyopo (incubators) kwa kuwa kinaweza kuokoa maisha ya mtoto mdogo ambaye vifaa vilivyopo sasa haviwezi kumfanya akue na kuendelea kuona maisha.

Wanasayansi hao wamejaribu kifaa hicho chenye mji wa mimba bandia kwa kutumia mimba ya kondoo ambaye aliweza kukaa kwa wiki nne na kuendelea kukua vizuri. Kondoo wengine ambao wamefanyiwa majaribio wamekua vizuri na mmoja wao ana mwaka mmoja akiwa na afya njema.

Watafiti hao wamesema ugunduzi huo ni hatua kubwa katika sayansi ya tiba na wanasema wana matumaini makubwa kwamba utafanya kazi kwa ufanisi huo huo kwa binadamu ambao kutokana na sababu mbalimbali huzaliwa kabla ya muda.

Timu hiyo ya watafiti kutoka Hospitali ya Watoto ya Philadelphia nchini Marekani wametengeneza mji wa mimba bandia kwa kumpachika kondoo ambaye muda wake wa kuzaliwa bado kwenye mfuko maalumu ambao umeunganishwa kwenye mfumo wa hewa ya Oxygen.

Kama watafiti hao watafanikiwa, ugunduzi wao huo utatumika vyumba ambavyo vitajazwa maji maji maalumu (amniotic fluid) kuweza kuokoa maisha ya watoto wadogo ambao huzaliwa kabla ya muda wao.

Matatizo ya watoto ambao huzaliwa kabla ya muda ni moja ya chanzo kikubwa kinachoongoza kwa vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano duniani, hii ni kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Inakadiriwa kuwa zaidi ya watoto milioni 15 huzaliwa kabla ya muda wao kila mwaka na mwaka 2015 watoto milioni moja walifariki dunia.

Kondoo hao waliowekwa kwenye kifaa hicho maalumu wakiwa na umri sawa na mtoto wa binadamu aliyezaliwa kati ya umri wa wiki 23-24, walikaa kwenye kifaa hicho kwa wiki nne huku wakifuatilia kwa karibu maendeleo yao kila siku.

“Kondoo waliofanyiwa majarabio walionesha matokeo mazuri. Wakipewa chakula pamoja na hewa ya kutosha, walionesha ukuaji mzuri wa mapafu, ubongo,” inasomeka sehemu ya ripoti ya utafiti huo.

Kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mtafiti Mkuu Dk. Alan Flake anasema; “lengo letu lilikuwa ni kufikia siku 21 hadi 28 ya kumuweka kwenye kifaa hiki. Baada ya hapo tunawatoa nje na kutathmini utendaji kazi wa mapafu yao katika mazingira mapya. Tuligundua kuwa yalikuwa yakifanya kazi vizuri kama kondoo wa umri sawa aliyezaliwa kwa njia ya kawaida. Baada ya kuridhika na ukuaji wa mapafu, tulikwenda hatua nyingine kwa kuanza kuangalia maendeleo ya ubongo pamoja na viungo vingine.”

Anaongeza tumeweza kufanya majaribi mengi na yote yameonesha mafanikio makubwa. Kondoo wote wa majaribio walipotolewa kwenye kifaa hicho maalumu waliweza kuishi katika mazingira mapya. “Tuliwapa maziwa kwa kutumia chupa na wakakua. Wapo vizuri katika kila kitu. Bahati mbaya hakuna kipimo cha kwa ajili ya wanyama lakini tunauhakika wapo sawa kabisa,” anasema mtafiti huyo.

Culin Duncan ni Profesa wa Sayansi na Tiba ya Afya ya Uzazi katika Chuo Kikuu cha Edinburg nchini Uingereza, ambaye hajahusika kwa njia yoyote katika utafiti huo, anasema utafiti huo ni hatua kubwa katika kuzuia vifo vya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao.

“Hii ni hatua muhimu na kubwa katika kunusuru maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao. Utafiti huu hauna maana ya kuchukua nafasi ya tumbo la mwanamke kipindi cha nusu ya ujauzito, ni hatua muhimu ya namna mpya ya kuweza kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa katika umri mdogo ambao kabla ya ugunduzi huu, wasingeweza kuishi,” anasema katika taarifa yake.

Anasema: “Ni hatua nzuri na muhimu, lakini bado kuna changamoto kubwa ya kuboresha mfumo mzima ili kuweza kupata matokeo bora zaidi ambayo yataendana na mahitaji na mazingira yaliyopo sasa.

“Hii itahitaji utafiti zaidi kabla ya kuweza kuitumia rasmi kwa binadamu na itachukua muda kidogo,” anaongeza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles