25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaougua shinizo la damu hatarini kuugua figo

Nora Damian – Dar es Salaam

WANAOUGUA kisukari na presha kwa muda mrefu, wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya figo, imeelezwa.

Tafiti zinaonyesha asilimia saba  ya Watanzania wana matatizo ya figo huku ugonjwa huo ukipanda kwa nafasi zaidi ya 10 na kuwa miongoni mwa magonjwa sita hatari duniani.

Akizungumza na MTANZANIA, Dar es Salaam juzi, daktari bingwa wa magonjwa ya figo,Egina Makwabe, alisema magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndiyo chanzo kikuu cha matatizo ya figo. 

Dk. Makwabe alikuwa akizungumza baada ya ufunguzi wa kitengo cha matibabu ya figo Hospitali ya Kardinali Rugambwa kitakachotoa huduma ya kusafisha damu kwa wagonjwa ambao figo zao zimeshindwa kufanya kazi.

“Tanzania na duniani kote kuna vitu vinavyoongoza kwa kusababisha tatizo la figo, namba moja ni kisukari, wagonjwa wanaokuwa na kisukari kwa muda mrefu zaidi ya miaka mitano na kuendelea wana uwezekano mkubwa wa kupata matatizo ya figo.

“Kisababishi kingine ni presha, pia matumizi ya muda mrefu ya dawa za mitishamba na za kizungu zikiwemo za maumivu aina ya diclofenac na nyingine bila kuwa na ushauri wa daktari,” alisema. 

Alisema ili kuzuia magonjwa ya figo ni muhimu kudhibiti kisukari, shinizo la damu, kuepuka matumizi holela ya dawa, kubadilisha mfumo wa maisha, kuzingatia ulaji bora na kufanya mazoezi.

Kuhusu kitengo hicho, alisema kitafanya kazi kwa wagonjwa saba kwa wakati mmoja na kwamba kimegawanyika katika sehemu tatu yaani cha wagonjwa ambao hawana maambukizi yoyote, wenye matatizo ya homa ya ini aina ya B na wenye HIV na homa ya ini aina ya C.

“Kitengo hiki ni cha kisasa kimezingatia viwango vya kimataifa, wagonjwa watakaotibiwa hapa ni wale waliofikia hatua ya mwisho ya figo kushindwa kufanya kazi,” alisema.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kadinali Rugambwa, Sarah Deogratius, alisema kitengo hicho kimejengwa kwa ushirikiano na Africa Health Care Network (AHN) ili kusaidia wagonjwa wenye uhitaji wa huduma hiyo ambao walikuwa wakilazimika kuifuata katika vituo vilivyopo katikati ya mji.

Alisema gharama za huduma hiyo zitakuwa kati ya Sh 200,000 hadi 240,000 kuwawezesha wananchi wengi hasa wa kipato cha chini kuweza kumudu.

“Kulikuwa na uhitaji mkubwa kwa sababu eneo hili halina huduma hii, hivyo tutawapunguzia wananchi gharama ya nauli na muda waliokuwa wakiutumia kufuata katika vituo vilivyopo katikati ya mji,” alisema Dk. Sarah.

Hospitali hiyo ambayo ipo chini ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, ilianzishwa mwaka 1986 kama zahanati na mwaka 2005 ilipandishwa hadhi na kuwa hospitali.

Kwa siku inahudumiwa watu 350 hadi 400 na kwa upande wa wajawazito wanaojifungua kawaida kwa mwezi ni wastani wa 130 – 150 na wanaofanyiwa upasuaji ni 60 – 80.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yudas Ndungile, ambaye alimwakilisha Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alisema kuna ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo wanaohitaji kusafisha damu lakini vituo vinavyotoa matibabu hayo ni vichache na kusababisha msongamano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles