27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

WANAOTUPA WATOTO MITAANI KUSAKWA

Na JANETH MUSHI- ARUSHA


charles-mkumbo

BAADA ya kukithiri kwa matukio ya utupwaji wa watoto wachanga kwenye mitaro ya maji machafu, majalalani na katika maeneo mbalimbali, Jeshi la Polisi, Mkoa wa Arusha, limeanza msako wa kuwakamata watuhumiwa hao ili kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema wamelazimika kuendesha operesheni hiyo nyumba kwa nyumba ili kuwasaka watuhumiwa wa matendo hayo ya utupwaji wa watoto wachanga.

“Matukio ya utupwaji watoto katika maeneo mbalimbali na watu wasiojulikana, yamekithiri kwa kiasi kikubwa, ndiyo maana tumeanza msako wa kuwakamata watuhumiwa hao nyumba kwa nyumba na kuwafikisha katika vyombo vya dola.

“Tunataka kuondoa vitendo hivyo vya ukatili  ambavyo vinazidi kushika kasi ndiyo maana tumelazimika kuendesha operesheni hiyo ili kukomesha vitendo hivyo vya kikatili na tunaomba jamii kutoa ushirikiano ili tuweze kufanikiwa kukamata watuhumiwa hao,” alisema Kamanda Mkumbo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto, Mkoa wa Arusha, Inspekta Happyness Temu, alisema kasi ya utupaji wa watoto wachanga imeongezeka.

Kwa mujibu wa Inspekta Temu, mwaka 2015 hadi 2016, watoto 58 waliokotwa katika maeneo mbalimbali jijini hapa.

“Dawati letu kwa kushirikiana na taasisi nyingine za kiserikali na zisizokuwa za kiserikali, tumekuwa tukitoa elimu kwa jamii juu ya kupinga vitendo vya kikatili dhidi ya watoto ila bado vitendo hivyo vimezidi kuongezeka,” alisema Inspekta Temu.

Naye  Ofisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo, Mkoa wa Arusha, Blandina Nkini, alisema kwamba, miongoni mwa sababu zinazochangia utelekezwaji na utupwaji wa watoto ni pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ulevi wa kupindukia, umasikini pamoja na baadhi ya wanaume kuzikimbia familia zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles