Wanaosajilia wenzao laini za simu kitanzini

0
2566

Grace Shitundu – Dar es salaam

WAKATI zikiwa zimesalia siku mbili kufikia ukomo wa siku 20 zilizoongezwa na Rais Dk. John Magufuli  kufunga laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa alama za vidole, uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini lipo kundi kubwa la watu wenye vitambulisho vya Taifa au namba za vitambulisho hivyo ambao wamewasajilia wale wasiokuwa navyo.

Jambo hilo limeelezwa na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) kuwa ni kosa kisheria kumsajilia laini  mtu aliyefikisha miaka 18 kwa kitambulisho ambacho si chake na adhabu yake ni faini au kwenda jela. 

Katika uchunguzi wake MTANZANIA Jumamosi limebaini kuwa, hatua ya wenye vitambulisho vya Taifa kuwasajilia ama ndugu, jamaa, marafiki au jirani zao ni kutaka kuwahi tarehe ya mwisho ya kutumia laini zisizosajiliwa kwa alama za vidole ambayo ni Januari 20 mwaka huu.

Uchunguzi unaonyesha wengi ambao husajilia wengine laini hawajui kama ni kosa na inapotokea yule aliyemsajilia akatekeleza uhalifu atayewajibika ni yeye aliyemsajilia.

MTANZANIA Jumamosi linafahamu kuwa ikitokea yule uliyemsajilia akatekeleza uhalifu wowote mfano wizi au mauaji akihusisha simu yake, mtu wa kwanza kuwajibika ni yule aliyemsajilia.

Mbali na kosa la kumsajilia mtu adhabu yake kuwa wazi, pia sheria imeeleza bayana kuhusu adhabu ya mtu anayethibitika kutekeleza makosa mengine ya uhalifu mfano hayo ya wizi au mauaji.

Baadhi ya watu ambao wamesajili laini kwa kutumia vitambulisho vya jamaa zao walisema; wamefanya hivyo ili kunusuru kukosa mawasiliano.

“Kwa mfano mimi kanisajilia mdogo wangu kwa kutumia kitambulisho chake, nimefanya hivyo kwasababu Nida(Mamlaka ya Vitambulisho Vya Taifa) kuna foleni sana na ninaona kupata kitambulisho itakuwa ndoto kwa sasa na mawasiliano ni muhimu kwangu.

“Nimeona bora hata wakifunga laini baada ya hizo siku 20 nibaki na angalau na hii moja” alisema mkazi mmoja wa Dar es salaam ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.

Mwingine aliyesajiliwa laini ya simu ni mwanafunzi wa kidato cha sita ambaye licha kufikisha miaka 18 amelazimika kufuata njia hiyo kutokana na kushindwa kupata namba ya kitambulisho cha Taifa kwa wakati.

“Mimi kanisajilia mama, nilikwenda Nida licha ya foleni kubwa namba zenyewe za kusubiri na hazitabiriki,” alisema.  

Kundi jingine ambalo limeonekana kupewa msaada wa kusajiliwa laini ni wasichana wa kazi za majumbani.

“Kwa mfano mimi namuacha dada na watoto nyumbani muda mwingi ninakuwa kwenye utafutaji wa maisha  na hana mawasiliano nafanyaje hapo zaidi ya kumsajilia laini ili nipate mawasiliano ya nyumbani,”

“Tunajua ni changamoto msichana anaweza kuondoka na laini uliyomsajilia lakini masharti nayo ya Nida ni changamoto, hawa wasichana wengi wametoka vijijini na wengi wao kuwa na cheti cha kuzaliwa ni mtihani na mchakato wa kukitafuta nao unahitaji muda,” alisema dada mmoja.

KAULI YA TCRA

Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Ofisa Mwandamizi Mkuu wa TCRA, Semu Mwakyanjala alisema kuwa ni kosa kumsajilia mtu mwingine laini kwa kitambulisho ambacho sio chake.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroni na Posta (EPOCA) ya mwaka 2010 inaeleza wazi kuwa ni kosa kumsajilia laini mtu mwingine.

Alisema miongoni mwa adhabu anazoweza kupewa atakayekutwa na hatia ni kulipa faini isiyopungua shilingi milioni tano au kwenda jela miezi sita au adhabu zote mbili kwa pamoja.

“Ni ukiukaji wa sheria kutumia namba ya simu iliyosajiliwa na mtu mwingine, na iwapo unamsajilia simu mtu laini ya simu na ikiwa imetumika vibaya kwa uhalifu, aliyesajili atawajibika moja kwa moja kwa uhalifu huo”, alisema Mwakyanjala.

Hata hivyo alifafanua kwamba kwa mtoto ambaye hajafikisha miaka 18 anaruhusiwa kusajiliwa laini na wazazi wake ambao watatumia vitambulisho vyao vya taifa.

“Kwa watoto ambao wako chini ya miaka 18, wazazi wao wanaruhusiwa kuwasajilia laini zao kwa kutumia vitambulisho vyao” alisema Mwakyanjala.

Wakati zikiwa zimesalia siku mbili kabla ya kuzimwa kwa laini hizo ambazo hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole, laini milioni 22.4 ziko hatarini kufungiwa.

VIONGOZI WAPATA WAKATI MGUMU

Suala hilo la usajili wa simu kwa alama za vidole linaonekana kuwapa wakati mgumu viongozi wanaoendesha na kusimamia zoezi hilo.

Juzi Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola pamoja na menejimenti ya Nida  waliitwa Ikulu, Dar es Salaam  na Rais Dk. John Magufuli.

Viongozi hao ambao walikuwa wafanya mkutano na waandishi wa habari walishindwa kufanya hivyo baada ya kupokea wito huo kwa dharura na hivyo kuondoka kwa helkopta kutoka jijini Dodoma kuelekea Dar es Salaam.

Mara kadhaa waziri huyo ameonekana kuchukua hatua kadhaa ikiwamo kuwaita viongozi wa Nida huku wengine akiwachukulia hatua.

Awali Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuwa Desemba 31 mwaka jana ingekuwa siku ya mwisho ya kutumika laini zisizosajiliwa kwa mfumo huo, lakini Rais Dk. John Magufuli aliongeza muda hadi Januari 20, mwaka huu.

Rais Magufuli alisema anaongeza muda huo ili watu walioshindwa kusajili namba zao kwa sababu ya kuugua na wasiokuwa na namba ama vitambulisho vya taifa, waweze kumalizia mchakato huo.

Alisema muda huo ukiisha hakuna kisingizio chochote kitakachokubalika na kuiagiza TCRA kuzima laini zisizosajiliwa.

Akizungumza na gazeti dada la hili la MTANZANIA juzi, Kaimu Meneja Mawasiliano wa TCRA, Mwakiyanjala, alisema hadi kufikia Januari 12 mwaka huu, laini zilizosajiliwa ni 26,170,137 sawa na asilimia 53.8 ya laini 48,648,864 zinazotumika nchini.

 “Laini za simu 22,478,727 sawa na asilimia 46.3 bado hazijasajiliwa kwa mfumo wa alama za vidole,” alisema Mwakiyanjala.

Takwimu zinaonyesha hadi Desemba 10 mwaka jana, laini zilizokuwa zinatumika zilikuwa 47,063,603 ambazo zinamilikiwa na watu milioni 21.1.

TCRA ilisema zoezi hilo ni endelevu, hivyo kwa watakaositishiwa huduma za laini za simu wanaweza kuendelea na utaratibu wa usajili kwa lengo la kuzirudisha au kupata laini mpya.

“Kwa watumiaji au waombaji wapya wa laini za simu, wataendelea kusajiliwa muda wote na usajili huo kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole ni endelevu,” alisema Mwakiyanjala.

TCRA pia ilisema kwa wanadiplomasia au taasisi ambazo hazijakamilisha usajili wa laini za simu au zinazotumika kwenye vifaa vyao vya mawasiliano, wanatakiwa waendelee kufuata utaratibu uliowekwa.

Tangu Mei mwaka jana, Serikali ilizielekeza kampuni za simu kuanza usajili wa laini za simu kwa kutumia alama za vidole.

Hata hivyo, usajili huo umekumbwa na changamoto nyingi kutokana na wananchi wengi kutokuwa na namba ama vitambulisho vya taifa.

Katika maeneo mbalimbali nchini kumeshuhudiwa foleni kubwa za watu katika ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wakihangaika kutafuta namba au vitambulisho huku wengine wakilalamikia kufuatilia bila mafanikio.

Wakati akizungumza jijini Mbeya Aprili mwaka jana, Rais Magufuli alisema Watanzania milioni 14 ndio waliokuwa wamepata vitambulisho vya taifa.

Aidha takwimu zilizotolewa Januari 2 mwaka huu na Mkurugenzi Mkuu wa Nida, Dk. Anold Kihaule, zinaonyesha watu milioni 7.6 tayari wana namba na kila siku mamlaka hiyo inaendelea kuzitoa sehemu mbalimbali nchini.

Dk. Kihaule alitoa takwimu hizo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alipotembelea kituo cha kuchakata taarifa za waombaji nchi nzima kilichopo Kibaha mkoani Pwani.

Masauni aliagiza kuongezwa idadi ya watumishi katika kituo hicho na saa za kufanya kazi hadi kufikia 16 ili kwenda sambamba na muda ulioongezwa na Rais Magufuli.

Alisema katika vituo mbalimbali vya Nida wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia kufuatilia vitambulisho bila mafanikio, licha ya kwamba wengine waliomba miaka mitatu iliyopita.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here