27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

WANAOPOTEZA PASIPOTI KUTOZWA SH 500,000

Na SHEILA KATIKULA-MWANZA


IDARA ya Uhamiaji imewaonya wanaopoteza hati za kusafiria watalazimika kulipia upya kati ya Sh 500,000 na 750,000 badala ya Sh 130,000 ya awali.

Hayo yalisemwa juzi na Naibu Kamishna wa Uhamiaji Mkoa wa Mwanza, Paul Eranga, wakati wa uzinduzi wa utoaji hati mpya za kusafiria za kisasa za kielektroniki (pasipoti).

Alisema kumekuwa na wimbi kubwa la watu kusingizia kupotea kwa pasipoti zao, hivyo uamuzi wa Serikali kwa sasa ni kuwatoza malipo ya ziada kama adhabu kwa wale ambao watapoteza.

Kamishna huyo pia alisema baadhi ya raia wamekuwa wakisingizia kupoteza pasipoti zao kwa lengo la kupata mpya pale wanapokwenda nchi za nje na kufanya makosa.

“Wakienda nje na kufanya makosa, pasipoti zao huwekwa kwenye kundi la watenda makosa, hivyo husingizia zimepotea ili wapewe zingine mpya kuondoa kumbukumbu hiyo.

“Kwa sasa ukipoteza pasipoti yako kwa mara ya kwanza utalipa Sh 500,000 kuipata mpya, hii ikiwa na malipo ya adhabu kwa kuwa mzembe kiasi cha kupoteza, lakini ukipoteza tena kwa mara ya pili, basi utalazimika kupata nyingine kwa gharama ya Sh 750,000,” alisema.

Alisema uamuzi huo umefikiwa kwa kuwa watu wengi wamekuwa wakiichukulia pasipoti kama jambo la kuchezea, hivyo lengo la Serikali kuwatoza gharama kubwa ni kutoa adhabu ambayo itawafanya kuwa makini na kuitunza kama nyaraka muhimu.

Eranga alisema tangu Januari 31, mwaka huu utoaji pasipoti mpya ulipozinduliwa, tayari wamepokea maombi 30,941 na kuyafanyia kazi, hivyo aliwataka wananchi kuchangamkia fursa kwa kuwa mfumo wa sasa ni rahisi, kwamba mtu anaweza kupata pasipoti ndani ya saa moja au siku moja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongela akizindua huduma hiyo, alitoa wito kwa wananchi kutoa taarifa mapema pale wanapobaini au kuwa na shaka na mtu asiye raia ili hatua za kisheria zifuatwe.

Aidha aliwaagiza maofisa uhamiaji kufanya kazi zao kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria, taratibu na miongozo iliyowekwa na Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa huduma stahiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles