Na GABRIEL MUSHI, DAR ES SALAAM
Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage ametangaza kuanza kuchukua hatua za kuwafutia leseni mawakala wote wanaouza saruji kwa bei ya juu licha ya kutokuwapo kwa upungufu wa bidhaa hiyo kwa sasa.
Hatua hiyo imekuja baada kutengamaa kwa mitambo ya uzalishaji malighafi ya saruji katika viwanda kadhaa nchini ambao ulisababisha uhaba wa saruji sokoni kwa zaidi ya siku 20.
Mwijage ametoa kauli hiyo leo Agosti 27, 2018 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda Tanzania Portland Cement (Twiga) kilichopo Wazo na Camel Cement Company kilichopo Mbagala.
Akizungumza na uongozi wa kiwanda kinachozalisha saruji ya Twiga, Mwijage amesema lazima baadhi ya mawakala watolewe kafara ili kudhibiti hali hiyo.
Pia ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kumpatia orodha ya mawakala wote wanaosambaza bidhaa hiyo pia waagizwe kushusha bei ya saruji ambayo sasa imepaa hadi Sh 18,000 katika baadhi ya maeneo.
“Mimi nimefanya kazi hapa miaka 18, nafahamu mchezo wote wa vijana wako wanaoufanya, ndio maana nakuagiza uniletee orodha ya mawakala wote wanaosambaza saruji ili niwabaini na kuwafutia leseni.
“Kwa sababu sasa Dangote anazalisha tani 4,500 kutoka tani 2000 kwa siku, Twiga anazalisha tani 6,000 kutoka tani 3,500 kwa siku, Tembo tani 1,100, Nyati tani 2,000 hivyo hakuna uhaba wa saruji sasa. Tayari hali imetangamaa ila kwanini bei iendelee kubaki juu.
“Kiujumla kwa siku tunazalisha tani 16,000 na sasa tunatumia tani milioni 5.8 kutoka tani milioni 4.8 kwa mwaka na viwanda vyote vilivyosimikwa sasa vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.5 kwa mwaka,” amesema.
Aidha, alisema ili kuendelea kuhimili soko la ndani na la nje, tayari kuna viwanda vitatu ambavyo ni cha Mamba, Nyati namba 2 na kiwanda cha wachina cha Engian ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha malighafi inayotumika kuzalisha saruji (clinker) zaidi ya tani milioni saba kwa mwana.
“Suala hili la saruji kupanda, naomba watu wanivumilie, dawa ya kupanda naijua, saruji imejaa sokoni, bei inashuka yenyewe, ila wale wanaopandisha inaitwa ‘profiteering’ siku ya kiama inshallah basi hukumu ni yao kama wanataka kuishi duniani shauri yao hukumu ni yao.
Aidha, Meneja Undelezaji Biashara wa Kampuni ya Saruji ya Twiga (TPCC), Mhandisi Danford Semwenda ni kazi ngumu kuwadhibiti mawakala wa uuzaji wa saruji hiyo hivyo wanaomba ushirikiano kutoka serikali ili kudhibiti hali hiyo.
Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Camel, Ghalib Hassan Ghalib alisema kutokuwapo kwa umeme wa uhakika nao umekuwa kikwazo kwa kiwanda hicho kufikia malengo ya kuzalisha tani 600 kwa siku na hivyo kuzalisha tani 400.