25.2 C
Dar es Salaam
Monday, December 2, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaonyanyasa wawekezaji sasa kukamatwa

Raymond Minja Na Francis Godwin – Iringa

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kuwakamata na kuwaweka mahabusu watendaji wa idara za Serikali, wanaonyanyasa wawekezaji bila kufuata taratibu.

Amesema Serikali imefungua milango ya uwekezaji wa viwanda kwa wadau wake bila kuweka vikwazo vyovyote  hivyo wanaoleta vikwazo lazima washughulikiwe.

Kauli hiyo aliitoa jana mjini Iringa baada ya kuzindua Kiwanda cha maji Mkwawa.

Alisema kuwa lengo la Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji, ni kutaka kuona pia wawekezaji wanawekeza bila vikwazo.

“Hivyo kila mwekezaji ambaye anataka kuwekeza awekeze bila vikwazo na akiomba ardhi apewe kwa ajili ya kujenga kiwanda chochote. Serikali imedhamiria kubadilisha uchumi wake hadi kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2020,” alisema.

Alisema kupitia viwanda zimeweza kuzalishwa ajira kwa Watanzania za viwandani ambazo hazihitaji elimu kubwa, huku mtu yeyote anaweza kupata ajira kwa sifa yake.

“Leo (jana) tumeona pia maji kutoka Mkoa wa Iringa, Mkwawa yanazidi kusambaa. Kutoka Iringa maji haya yameweza kusambaa kila kona, pia tunashuhudia Watanzania wengi  wakiwamo wana Iringa nao wamepata ajira hapa,” alisema.

Majaliwa alisema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli itaendelea kudhibiti uingizwaji wa bidhaa mbalimbali kutoka nje ili kulinda viwanda vya ndani.

Pia alitembelea kiwanda cha maziwa cha Asas, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Iringa na aliipongeza kampuni hiyo.

Alisema Serikali imedhamiria kukuza uchumi na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 kupitia sekta ya viwanda.

 “Serikali imefanya mageuzi makubwa kwenye sekta ya mifugo ili kuhakikisha inaleta tija kwa wafugaji na taifa kwa ujumla, hivyo wafugaji endeleeni kuimarisha ushirika wenu. Wizara ya Mifugo iendelee kuwaelimisha wafugaji ili wafuge kitaalamu,” alisema Majaliwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha Maziwa cha Asas, Fuad Abri, alisema wana mpango wa kupanua uzalishaji kwa kujenga kiwanda kingine cha kusindika maziwa katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya na kipo katika hatua za mwisho kukamilika.

Naye, Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda cha Maji cha Mkwawa, Ahmed Huwel, alisema kiwanda chao kilianzishwa mwaka juzi kwa lengo la kuzalisha na kufanya biashara ya maji safi na salama pamoja na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Alisema kiwanda chao kimeajiri watumishi 158, kati yao wanaotoka nje ya nchi ni watatu tu na kwa upande wa ajira zisizo rasmi ni zaidi ya 3,000 na kwamba wanatarajia kuziongeza kwa wananchi wengi zaidi baada ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda kingine cha kutengeneza vinywaji baridi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles