25.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 9, 2024

Contact us: [email protected]

Wanaohusika mradi wa Magadi Soda Engaruka watakiwa kukamilisha taratibu

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali imewataka viongozi wa taasisi zinazohusika na mradi wa kimkakati wa Magadi Soda ulioko Engaruka wilayani Monduli,Mkoani Arusha, kushirikiana katika kukamilisha taratibu ili mradi uanze kutekelezwa kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dk. Hashil Abdallah jana Desemba 21,2023, alipotembelea mradi huo kwa lengo la kuona utekelezaji wake na kutatua changamoto mbalimbali.

Akizungumza katika na viongozi wa taasisi zinazohusika na mradi huo Dk. Abdallah amesema ziara ya makatibu wakuu katika kuutembelea mradi huo ni ishara tosha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuona unaanza kutekelezwa mara moja.

“Ziara hii imeshirikisha wizara tatu na jumla ya taasisi nne na itafanya kazi kwa kushirikiana na vijiji vinne katika kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mradi na kuanza kutekelezwa kwa mradi huu ni dhahiri kuwa utasaidia katika kuboresha maisha ya wakazi wa Engaruka na Taifa kwa ujumla, kuongeza mapato kwa serikali ,” amesema.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali amebainisha kuwa kuanza kuchimbwa kwa madini ya magadi soda nchini kutaokoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kimekuwa kikitumika kuagiza bidhaa hiyo kutoka nje ya nchi kwa ajili ya matumizi viwandani ambapo takwimu zinaonyesha kuwa serikali hutumia kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja kwa mwaka.

“Sisi kama wasimamizi wa sekta ya madini hapa nchini tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuwa magadi soda ni madini muhimu sana kwa ajili ya ustawi wa viwanda vingi hapa nchini kwa kuwa yanatumika kama malighafi na tuna viwanda ambavyo tayari vinategemea malighafi hii muhimu,” amefafanua Mahimbali.

Katika hatua nyingine Mahimbali amewataka wakazi wa Engaruka kuhakikisha wanachangamkia fursa mbalimbali zitakazojitokeza kipindi mradi huu utakapoanza kutekelezwa.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo, (NDC) Dk.Nicolaus Shombe, amebainisha kuwa NDC kama mwekezaji kwa niaba ya serikali tayari imekamilisha hatua mabalimbali za kuelekea kuanza kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo kufanyika kwa upembuzi na tathmini ya mazingira.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Happyness Laizer pamoja na Katibu Tawala wa Wilaya ya Monduli, Muhsin Kassim wamesema wapo tayari kupokea mradi huo, huku wakitoa rai kwa wananchi kuchangamikia fursa zitakazotokana.

Wakizungumza kwa niaba ya wananchi wa Engaruka viongozi wa eneo hilo wakiwemo Diwani na Mtendaji wa Kata ya Engaruka na wenyeviti wa vijiji vya Engaruka juu, Engaruka chini, Irerendeni pamoja na Oldonyo Lengai wameonyeshwa kufurahishwa na hatua ya serikali kuamua kutekeleza mradi huo utawakaowaletea maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika upatikanaji wa ajira, ukuaji wa biashara na uchumi kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles