25.5 C
Dar es Salaam
Friday, September 29, 2023

Contact us: [email protected]

Wanaofanya usafi vyooni hatarini kupoteza maisha

AVELINE KITOMARY -DAR ES SALAAM

SHIRIKA lisilo la kiserikali la Water Aid Tanzania limesema watu wanaojihusisha na kazi za usafi vyooni wako hatarini zaidi kupoteza maisha kutokana na mazingira hatarishi.

Ripoti hiyo iliyotolewa jana na shirika hilo likishirikiana na Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Kazi Duniani (ILO) na Benki ya Dunia, inasema pamoja na kuimarika kwa huduma za jamii katika nchi zinazoendelea, bado wafanyakazi wa usafi wa vyoo wako hatarini kuathirika kiafya.

Pia ripoti hiyo ilieleza kuwa nchi ya India pekee kati ya mwaka 2017 na 2018, imethibitika kuwa watu watatu wanaofanya uzoaji wa taka za chooni hufariki dunia kila baada ya siku tano, huku kwa mwezi mmoja watu 18 wanapoteza maisha na kwa mwaka ni watu 216.

Akitoa ripoti hiyo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meneja Miradi Mwandamizi wa Water Aid Tanzania, Twaha Mubarak alisema katika kuadhimisha Siku ya Choo Duniani leo, wanatoa wito kwa Serikali kutengeneza mazingira wezeshi na mfumo rasmi kwa watu wanaofanya kazi za usafi wa uzoaji taka wa vyoo.

 “Katika suala la usafi, bado kuna watu hatujawatazama sawasawa, watu hawa ni wale wanaofanya kazi sekta ya usafi, hasa wale wanaohusika na uzoaji wa taka za chooni hadi kutupa takataka.

“Ripoti inabainisha mazingira mabaya ya mamilioni ya wafanyakazi ambao wanafanya kazi katika mazingira hatarishi kwa afya zao.

“Pamoja na kuimarika kwa huduma za jamii, kundi hili limekuwa likiachwa katika mazingira mabaya, hawana vitendea kazi, lengo la ripoti ni kuinua ufahamu kuhusu mazingira hatarishi wanayopitia watu hawa wa mnyororo wa usafi kama kusafisha vyoo, kutapisha mashimo ya vyoo, kusafisha mitaro na kusimamia njia ya kutibu maji taka.

“Wafanyakazi hawa mara kwa mara wanagusa vinyesi vya binadamu wakiwa hawana vifaa vya kuwakinga, hali hii inaweza kuwafanya kupata magonjwa hatarishi.

“Ukiacha vifo, kuna wale wanaopata maumivu, ajali na magonjwa ya mara kwa mara au yanayojirudia na pia kuna ugonjwa kama kipindupindu ni hatari,” alisema Mubarak.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhai Mazingira na Watu (Umawa), Mathias Milinga aliiomba Serikali kuongeza nguvu katika kazi za uchakataji wa maji taka ili kuongeza ajira kwa vijana.

“Huwa tunakuwa na mfumo rasmi wa kuchakata na kufanya uzalishaji ambao utatumika kwa mahitaji ya binadamu, ipo mitambo ambayo inatumika, yale maji taka yanafaa kutengenezea mbolea, mkaa wa kupikia, gesi na pia maji masafi, kwa hiyo hii itasaidia kutunza mazingira,” alisema Milinga.

Siku ya Choo Duniani huadhimishwa Novemba 19 kila mwaka na kwa mwaka huu kaulimbiu ni ‘Tusiache mtu yeyote nyuma’.

Mwisho

Asilimia 16 ya vijana Tanga hupata mimba

Na Amina Omari – Tanga

UKOSEFU wa elimu ya afya ya uzazi kwa vijana, umesababisha asilimia 16 ya kundi hilo kupata mimba za utotoni mkoani Tanga.

Hayo yalisemwa jana na Mratibu wa Afya ya Uzazi kwa Mama na Mtoto mkoani Tanga, Doroth Lema wakati akieleza kwa waandishi wa habari sababu za uwepo wa mimba za utotoni.

Alisema changamoto kubwa ni ukosefu wa elimu sahihi ya masuala yanayohusu afya, hivyo kusababisha vijana wengi hususani wa kike kuwa wahanga wa mimba zisizotarajiwa.

“Iwapo elimu ya afya ya uzazi itawafikia vijana wengi, hasa wakati wa umri wa mabadiliko, watajitambua na kujilinda dhidi ya mimba za utotoni na hata maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi,” alisema Doroth.

Mratibu wa Ubora wa Huduma za Afya Mkoa wa Tanga, Dk. Rehema Maggid alisema  takwimu zinaonyesha tatizo la mimba za utotoni lipo zaidi mijini, ikilinganishwa na vijijini.

Dk. Rehema alisema vijana wa mjini ndio waathirika wakubwa kutokana na maendeleo ya utandawazi na hivyo kushindwa kupata taarifa kuhusu afya kwa kina.

Alisema endapo elimu ya uzazi itatolewa kwa kushirikiana viongozi, wadau wa afya, wazazi na walezi, itasaidia kuleta mabadiliko makubwa.

“Sasa Mkoa wa Tanga tumetekeleza mradi wa kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa makundi ya vijana ili wajitambue na kufanya uamuzi sahihi na kwa wakati mwafaka,” alisema Dk. Rehema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,750FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles