Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
WAFANYAKAZI wanane wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wanaokabiliwa na tuhuma za kughushi vyeti vya kidato cha nne wamekutwa wana kesi ya kujibu.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanane wa upande wa mashtaka na kuona kwamba kuna haja kwa washtakiwa kujitetea.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beata Massawe, Jackline Juma,
Philimina Mtagurwa na Amina Mwinchumu.
Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi, Nyigulila Mwaseba, wakati kesi hiyo inaendeshwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro.
“Mahakama imepitia ushahidi wa mashahidi wanane wa upande wa Jamhuri, imeuona kwamba ushahidi huo una nguvu, hivyo washtakiwa mna kesi ya kujibu, mnatakiwa kujitetea,” alisema Hakimu Mwaseba.
Baada ya kusema hayo mahakama iliahirisha kesi hiyo hadi Juni 17 na 18 mwaka huu, kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, washtakiwa hao wanadaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri
wao ambaye ni BoT.
Washtakiwa Justina, Beata na Amina wanadaiwa kughushi vyeti hivyo mwaka 2001. Christina, Siamini, Janeth na Philimina, wanadaiwa
kughushi vyeti hivyo mwaka 2002.
Washtakiwa hao wanadaiwa kughushi vyeti hivyo na kutoa hati za uongo BoT kuonyesha vimetolewa na Baraza la Mitihani Tanzania wakati si
kweli.