Nyemo Malecela – Kagera
JESHI la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu saba kwa tuhuma za mauaji ya wanandoa Elizeus Rubanie (35) na Juliana Joseph (28), waliouawa kwa kukatwa mapanga wakiwa wamelala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Revocatus Malimi alisema tukio hilo lilitokea Kitongoji cha Mangasini, Kijiji cha Mabale, Kata ya Nyakahura, Tarafa ya Lusahunga, Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Kamanda Malimi alisema wakati wanandoa hao wamelala nyumbani kwao, walivamiwa na watu ambao hawakuwafahamu kwa idadi, sura na majina na kuwaua kwa kuwakatakata mapanga maeneo mbalimbali ya miili yao wakati huo watoto wakiwa wamelala chumba kingine.
Aliwataja waliokamatwa kuhusiana na tukio hilo ni Sophia Joseph (45), Joseph Magambo (47), Alphonce Karoli (37), Martine Makabe (36), Alex Leopard (44), Salvatory Mwiliza (38) na Aloyce Leopord (45).
Kamanda Malimi alisema kabla ya tukio hilo kutokea, kulikuwa na mgogoro wa ardhi (shamba) kati ya marehemu (Elizeus) na baadhi ya wanaukoo kwa muda mrefu.
“Eneo walilokuwa wakiishi marehemu na familia aliachiwa na babu yake mzaa baba ambaye aliwahi kuishi katika kijiji hicho kabla ya kuhama kwa shinikizo la wanajamii, wakimtuhumu kuwa ni mwizi, ndipo akaamua kuondoka na kumwacha mjukuu wake (Elizeus) akiishi na familia yake.
“Baada ya babu huyo kuhama, jamii waliungana na baadhi ya ndugu kwenye ukoo, hasa shangazi wawili wa Elizeus, wakimsakama na familia yake kwa kumtolea vitisho vya kumdhuru, wakimtaka ahame kwenye shamba hilo sababu hana haki ya kumiliki ardhi hiyo,” alieleza Kamanda Malimi.
Alisema mgogoro huo umekuwa ukisuluhishwa kwa muda mrefu na viongozi wa Serikali ya kijiji.
“Jamii ishirikiane na Jeshi la Polisi kufichua migogoro iliyopo, ambayo imekuwa chanzo cha mauaji na vitendo vingi vya ukatili wanavyofanyiwa wanawake, watoto na wazee kwa kuuawa.
“Kazi ya kutoa uamuzi ni ya mahakama, hivyo wanajamii wataweza kuonywa au kuelimishwa njia sahihi za kufuata kutatua migogoro hiyo,” alisema Kamanda Malimi.