32.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 12, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wamshtaki Pinda kwa Kinana

Mizengo-PindaNA ELIYA MBONEA, NGORONGORO

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, anadaiwa kutoa ahadi hewa ya magunia 10 ya mahindi kwa kila kaya kwa mwaka kama njia mbadala ya kilimo cha kujikimu kwa wananchi wanaoishi ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, mkoani Arusha.
Ahadi hiyo aliitoa Septemba 19, mwaka juzi, akiwa Endulen wilayani hapa, bila kuwapo kwa maandishi ya Serikali, hatua inayoligharimu Baraza la Wafugaji la Wilaya ya Ngorongoro kwa sasa mbele ya wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Nainokanoka wakati wa mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, mkazi wa eneo hilo, Nabulu Kolombo, alisema wanashangaa ahadi ya Waziri Mkuu Pinda imekuwa hewa na haina utekelezaji hadi sasa.
“Njaa imetuathiri sana hapa, tumejitokeza kukusikiliza Katibu Mkuu kwa sababu tunaiheshimu Serikali. Hatujawahi kuhama kwenda vyama vya upinzani, bado CCM inatuua kwa njaa kwani tunashindia mlo mmoja,” alisema Kolombo huku akitokwa machozi.
Kolombo aliendelea kumueleza Kinana kwamba kama si upendo wa Mungu, basi asingekuta wakiishi kwenye makazi yao kutokana na kufanyiwa vitendo vya hovyo vya kupewa mahindi bila mboga.
“Ahadi ya Pinda ilikuwa mbadala wa kulima ndani ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, kwani sheria haziruhusu kulima hata bustani, tunaomba umkumbushe kwani alikuja akatuahidi, kumbe alikuwa anatudanganya wanachama wenzake wa CCM
“Lakini pia chakula wanachotupa kwa sasa hakitoshi, na bado wanaendelea kutuletea unga bila mboga, hivi na nyinyi mnaishi kama hivi. Kama kuna makosa tulikosea wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro tunaomba Serikali itusamehe. Hivi sasa hatuendi hata kwenye shughuli za maendeleo,” alisema Kolombo.
Akijibu malalamiko hayo, Kinana alisema kwamba hana uwezo wa kutoa majibu ya kuridhisha kwa wakati, hivyo atahakikisha ndani ya mwezi mmoja anakwenda na viongozi waliopewa dhamana kwenye viwanja hivyo.
“Nakwenda Dar es Salaam, nitakutana na Waziri Mkuu Pinda ili tuzungumze kuhusu jambo hili. Lakini pia nitakutana na Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri anayeshughulikia Maafa na Waziri wa Chakula kisha nitawaleta hapa baada ya mwezi mmoja ujao, kwani serikali haiwezi kushindwa kutatua matatizo ya wananchi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles