Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
WAKAZI wa Mkoa wa Pwani wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kutembelea banda la Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali zikiwamo a vyeti vya kuzaliwa.
Akizungumza na gazeti hili katika maonyesho ya tatu ya wafanyabiashara na uwekezaji katika viwanja vya maonyesho mjini Kibaha mkoani Pwani jana, Msaidizi wa Usajili Mwandamizi na Mratibu wa Shughuli za RITA Mkoa wa Pwani, George Chuwa, amesema kumekuwapo na mwitikio mkubwa wa wananchi kutembelea banda hilo kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
“Tukiwa siku ya pili ya maonyesho yetu hapa Kibaha, kumekuwapo mwitikio mkubwa wa wananchi kuja kupata huduma kwenye banda letu, kama unavyoona mwenyewe watu wa kada mbalimbali wanafika.
“Wengi wao wanakuja kupata huduma za vyetu vya kuzaliwa, vya watu wazima au watoto… hili ni jambo jema maana nyaraka hizi ndo zinasaidia wewe au mimi kupata huduma za serikali,”amesema Chuwa.
Amesema kitendo cha maonyesho hayo kuwekwa karibu na wananchi kumechangia mno wananchi wengi kupata huduma.
“Unajua eneo hili la maonyesho liko karibu na barabara kuu hapa, kama mtu anatoka ofisini au ana shughuli zake ni rahisi mno kufika na kuhudumiwa kwa wakati akiwa na nyaraka zake zote zilizokamilika, hili ni jambo zuri mno,”amesema.
Amesema wananchi wengi wanaofika kwenye banda hilo, wanahitaji huduma ya kurekebisha nyaraka zao au kujaza fomu kamili ili kupata huduma.
“Pamoja na huduma hii, tunatoa elimu ya shughuli za wakala huu kwa kila mtu anayefika hapa namna, kama unavyojua mbali na kutoa nyeti za kuzaliwa, ndoa, tunashughulika pia na kuwashauri wananchi kuandika wosia wakiwa hai kwa ajili kuepuka matatizo ambayo yanaweza kujitokeza wakati mwana familia mmoja anapofariki dunia.
“Katika eneo hili bado watu ni wagumu kidogo, sisi tunaendelea kuwaelemisha kila wakati, tunaamini ufanya hivi kutasaidia mno kupunguza migogoro isiyokuwa na lazima pindi mwana familia mmoja anapoaga dunia, huepusha migogoro isiyokuwa ya lazima,”amesema.
Kuhusu changamoto, Chuwa amesema baadhi ya wananchi wanaofika kwenye bando hilo huwa na upungufu wa nyaraka zinazotakiwa, kama vile barua ya utambulisho kutoka Serikali za Mitaa.
“Tunapata changamoto kubwa ya baadhi ya wananchi kuja bila kuwa na nyaraka zilizokamilika kama vile barua za utambulisho kutoka Serikali za Mitaa, hivyo wanalazimika kurudia…naomba wajitahidi kukamilisha ili wakifika hapa tunawahudumia mara moja,”amesema.
Ametoa kwa wananchi wa Mkoa wa Pwani na maeneo ya jirani kutumia fursa hiyo kutembelea banda hilo wakati huu wa maonyesho, baada ya kusubiri au kwenye ofisi zao siku za kazi ambazo huwa na msongamano mkubwa wa watu. Amesema gharama ya kupata cheti cha kuzaliwa baada ya kukamilisha taratibu zote ni Sh 10,000 tu.
Maonyesho hayo yamezinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete, yamehudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Tanga, Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Dar es Salaam yanatarajiwa kufungwa Oktoba 10, mwaka huu.