21.2 C
Dar es Salaam
Sunday, August 14, 2022

Wananchi walia viwango vipya bima ya afya

Na AVELINE KITOMARY

-DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa (NHIF) kuzindua mfumo wa vifurushi vipya, baadhi ya wananchi wamesema havina wigo mpana wa kupata matibabu kama ilivyoainishwa kwenye vipeperushi.

Wakati madhumuni ya NHIF  kwa vifurushi hivyo yakiwa ni kuongeza wigo wa wananchi kupata bima ya afya, kuwapa fursa wale walio nje ya sekta rasmi kunufaika na kuongeza mapato ya mfuko huo, wenye mtazamo tofauti wanasema malengo hayo huenda yasifikiwe.

Baadhi ya mambo yaliyokosolewa na wananchi hao ni gharama kubwa za utoaji huduma za afya kupitia vifurushi na vizuizi vingi ikiwamo katika huduma za dawa, vipimo na zile za matibabu ya kibingwa na uzazi.

Aidha wameshtushwa vifurushi hivyo kutojumuisha magonjwa makubwa kama saratani, moyo, figo na mengine ambayo yanawagharimu fedha nyingi.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, mmoja wa wafanyabiashara katika Soko la Mawasiliano, Wilaya ya Ubungo, Musa Mbile alisema kuna haja ya huduma muhimu kupewa kipaumbele na kutokuwekewa muda wa kusubiri baada ya mwanachama kupata kadi ya bima.

“Kuna vizuizi kwenye aina ya huduma ambazo zinatarajiwa kutolewa na hivyo viwango vya fedha ambavyo vimeainishwa, yaani inashangaza kuwa tayari vitu vya muhimu vimewekewa ‘limitation’, mtu unamwambia eti baada ya kulipia miaka miwili mfululizo ndio aanze kupata huduma ya uzazi,” alisema Mbile.

HUDUMA ZA UTOAJI DAWA ZAKOSOLEWA

Katika huduma za utoaji dawa  kama ilivyoainishwa katika vifurushi vyote vitatu – Najali Afya, Wekeza Afya na Timiza Afya – ada ya kujiandikisha na kumwona daktari inalipiwa na mfumo wa bima katika vifurushi vyote.

Katika huduma ya kulazwa inapatikana kwa siku 30 tu kwa mwaka kwa kila mnufaika mmoja kwa kifurushi cha Najali Afya, huku kwa kifurushi cha Wekeza Afya inapatikana kwa siku 45 na kwa kifurushi cha Timiza Afya inapatikana kwa siku 60.

Huduma za dawa kwa kifurushi cha kwanza inapatikana kwa vituo vya zahanati na kituo cha afya, huku ngazi ya mwisho kwa kifurushi kikubwa cha Timiza  Afya ikiwa ni hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa dawa zote zinazoruhusiwa na mfumo huo.

“Wakati huohuo tayari kuna huduma zinaonekana kuwekewa vizuizi. Mfano dawa mtu analipa fedha halafu unamwambia dawa zinazoruhusiwa kituo cha afya tu na matibabu ya sehemu zingine, kwa hicho kifurushi cha kwanza huwezi kupata matibabu hospitali ya wilaya wala mkoa, sasa nikitakiwa kwenda rufaa nitafanyaje na mimi uwezo wangu ni wa kifurushi cha Najali Afya?

 “Hiyo bima haiwezi tena kunisaidia, labda waseme tu ni kwa ajili ya kutibu malaria na U.T.I kwenye zahanati, lakini kama lengo ni kuwasaidia wanachi na wanataka wananachi wengi wajiunge, kuna watu wanakaa mwaka mzima hajaugua ukisema unaweka ‘limitation’ ya magonjwa kama kansa, magonjwa ya moyo hizo ndio zenye gharama kubwa,” alisema Mbile.

Aliongeza; “Ni bora sasa kama wameamua kutupa huduma kwa njia ya bima watu wote wapate dawa kuanzia vituo vya afya, hospitali za wilaya, hospitali za mkoa na hata hospitali za rufaa na kwa gharama nafuu.”

Hoja ya Mbile kuhusu huduma ya uzazi ilitiliwa mkazo zaidi na mmoja wa wakazi wa Mbezi Beach, Zainab Almasi  aliyesema huduma hiyo inatakiwa kupewa kipaumbele zaidi, hivyo ni bora masharti hayo yakaboreshwa zaidi.

“Huduma za mama na mtoto kama za uzazi zinatakiwa zipewe kipaumbele kuliko hata zingine, sasa hapa kwenye kina mama wazazi watakufa wakati amekata bima kwa sababu haziruhusu matumizi ya haraka ya bima, hii inahitaji marekebisho.

“Haiwezekani mimi nikate bima na siku nataka kujifungua kama sijafikisha miaka miwili nikose huduma au nitoe tena gharama wakati tayari nina bima,” alisema Zainab.

MATIBABU YA KIBINGWA NA VIPIMO

Aidha wananchi wameshangaa vifurushi hivyo vipya kutoa vipimo kama x-ray, echo & EEG na Ultrasound, na kuacha vipimo vikubwa kama vya MRI na CT-Scan.

Zaidi vifurushi hivyo vimeelekeza huduma za kibingwa ziwe ni zile zinazopatikana katika hospitali ya mkoa pekee.

Kutokana na hayo, wananchi wameshauri kuongezwa vipimo vikubwa kwenye vifurushi hivyo ili waweze kupata huduma bora zaidi.

“Kwa upande wa huduma za kibingwa, nyingi zipo kwenye hospitali kubwa za rufaa kama KCMC, Muhimbili na Bugando, hizi ndio zingetakiwa ziwepo katika vifurushi vya bima kwa sababu na zenyewe zinatumia gharama kubwa, sasa zisipokuwepo mtakuwa mmemsaidiaje mwananchi masikini?” alihoji Salum Bakari, mkazi wa Ubungo.

Bakari pia aliomba wazee wapunguziwe gharama za bima za afya.

“Maana gharama zao ziko juu zaidi, hawana tena fedha hawa, kwani walishaitumikia nchi kwa muda mrefu. Nilitegemea gharama zao zingekuwa kama zile za watoto,” alisema Bakari.

KAULI YA ACT WAZALENDO

Juzi Chama cha ACT-Wazalendo kilitoa mawazo mbadala kwa Serikali kutoa ruzuku kwa wananchi kupata huduma za MRI na CT Scan kwa kuwalipa NHIF.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dorothy Semu alisema vifurushi hivyo vinahitaji kuboreshwa zaidi ili kila mwananchi wa kipato cha chini apate huduma bora za matibabu.

“Serikali inajali afya za watu, haina budi kutumia mfumo wa hifadhi ya jamii na kuachana na masuala ya vifurushi kwani mfumo huo unawezesha wananchi kujiwekea akiba na kuiwezesha Serikali kutoa huduma kwao kupitia fedha hizo,” alisema Dorothy.

Katika hilo hilo, kiongozi wa chama hicho, Zitto Kabwe naye ameonekana kuingia katika mjadala mzito na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na NHIF, baada ya kauli hiyo ya chama chake na ile aliyoitoa baadae kupitia akaunti yake ya Twitter.

Katika andiko lake la kwenye Twitter, ambalo aliambatanisha na moja ya barua  inayoonyesha mabadiliko ya viwango vya bima kwa watumishi, Zitto alisema wamepata ushahidi kuwa sasa kiwango cha chini cha kulipa NHIF ni Sh 40,000 kutoka 18,000 kwa mwezi.

Zaidi alisema kuwa waathirika ni wafanyakazi wa sekta ya umma na sekta binafsi ambao jumla yao nchi nzima ni takribani milioni 2.3.

Kisha akamalizia kwa kuandika “Serikali ya CCM ni Adui wa wafanyakazi nchini”.

Ni hoja hizo za Zitto zilimwibua Waziri Ummy kupitia katika akaunti yake ya Twitter, akimwonya mwanasiasa huyo kutofanya siasa katika jambo hilo.

“Kaka yangu tusifanye siasa kwenye hili. Vifurushi hivi ni kupitia utaratibu wa hiyari sio lazima. Pili, havijafuta bima ya afya ya jamii (CHF) ambapo  kiwango cha kuchangia kwa mwaka ni Sh 30,000 kwa kaya hadi watu sita. Aidha, vifurushi  vya watoto, wakulima nk. bado vipo,” alisema Ummy.

Aidha NHIF nao walimjibu Zitto kwamba; “Suala hili halina ukweli wowote kwa kuwa mfuko haukufanya mabadiliko  yoyote kwa watumishi wa umma. Mabadiliko yoyote yanayofanywa na mfuko huzingatia taratibu na sheria za uanzishwaji wa mfuko.”

Awali NHIF walitoa taarifa wakifafanua kuhusu kusambaa kwa taarifa za ongezeko la michango kwa watumishi kutoka Sh 18,000 hadi kufikia 40,000 kwa mwezi.

Katika hilo NHIF walisema hakuna mabadiliko yoyote  katika michango ya watumishi ambayo ipo kwa mujibu wa sheria ya uanzishwaji wa mifuko No. 395 (9).

“Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtumishi atachangia kiasi cha asilimia tatu na mwajiriwa atachangia kiasi cha asilimia tatu kwa mshahara wa mtumishi kwa mwezi,” ilisema taarifa hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,656FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles