25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi waiangukia Tarura

Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM


WAKAZI wa Kata ya Kisukuru Manispaa ya Ilala   Dar es Salaam, wameiomba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), kuijenga kwa lami barabara ya Majichumvi- Bonyokwa yenye kilomita mbili  kupunguza foleni katika barabara nyingine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti juzi walipokuwa wakiifanyia ukarabati wa muda barabara hiyo, wakazi hao walisema ni muhimu ikajengwa kwa lami ili irahisishe usafiri katika maeneo yao.

Mmoja wa wakazi hao, Isaac Swai alisema Serikali iangalie namna ya kuwafidia waliojenga pembezoni na kuipanua barabara hiyo kwa kuwa inayawia ugumu kwa gari kupishana.

“Barabara hii ni kubwa inatumiwa na wakazi wa Bonyokwa, Segerea, uwanja wa ndege na maeneo mengine kuelekea Ubungo, iwapo wakiitengeza itawarahisishia kupunguza foleni katika barabara nyingine,” alisema Swai.

Naye Diwani wa Kata ya Kisukuru, Joseph Saenda (Chadema), alisema ameunda kamati maalumu ya watu wanne kuifanyia ukarabati barabara hiyo ambayo iliharibika vibaya wakati wa mvua.

Alisema ameweza kuwahamasisha wananchi wa kata hiyo kuchangia fedha na nguvu zao katika ukarabati wa barabara ambao mwitikio wake ni mkubwa na kufanikiwa kuziba mashimo hayo.

“Maendeleo ni ya wananchi bila kubagua itikadi zao za vyama ndiyo maana wameitikia vyama vyote kukabiliana na adha hii,” alisema Saenda.

Amewataka wananchi kujitolea katika kushiriki shughuli za maendeleo na kuisaidia serikali kutatua changamoto zinazowakabili.

“Wananchi wasisubiri serikali kuwatatulia changamoto ambazo wao wenyewe wana uwezo wa kukabiliana nazo na kuzipatia ufumbuzi,”alisema Saenda.

Ofisa Uhusiano wa Manispaa hiyo, Tabu Shaibu alimpongeza diwani huyo kwa kuwahamasisha wananchi kusaidia serikali kuikarabati barabara hiyo.

“Tuna greda mbili ambazo hutumiwa kukarabati barabara lakini kwa sasa ziko katika matengenezo na barabara hii ilivyoharibika isingeweza kusubiri kwa kuwa mvua iko karibu,” alisema Tabu.

Alisema alichokifanya diwani Saenda kuwahamasisha wananchi katika maendeleo yao kinastahili kuigwa na viongozi wengine kuwahamasisha kufanya kazi za maendeleo kama kujenga zahanati, barabara na kazi nyingine za maendeleo katika maeneo yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles