25.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Wananchi wahimizwa kutumia mfumo wa GePG

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Serikali imesema uanzishwaji wa mfumo wa kielektroni wa ukusanyaji wa fedha za umma (GePG), umeanza kuzaa matunda kutokana na ongezeko kubwa la makusanyo, huku ikiwahimiza wananchi kutumia mfumo huo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha wahariri jijini Arusha jana kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Richaed Kwitega, alisema mfumo huo umeleta mapinduzi makubwa ambayo sasa yanasaidia Serikali kutekeleza miradi ya mpango mkakati.

“Sote tunafahamu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati yenye lengo la kuwaletea wananchi maendeleo.

“Miradi hiyo ni pamoja la ule wa Kufua umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), Mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Kutoa elimu bila ada kwa elimu ya msingi na sekondari, miradi ya kusambaza maji nchi nzima, kuboresha miundombinu ya barabara pamoja na miradi mingine mingi ambayo utekelezaji wake unahitaji fedha nyingi,”alisema.

Kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa miradi hii kwa kiasi kikubwa unategemea fedha za ndani, suala la ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuyasimamia limekuwa likipewa kipaumbele kikubwa na Serikali kupitia wizara yake.

Alisema katika kuhakikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani unaongezeka na usimamizi wake unaboreshwa, wizara imebuni na kuunda mfumo wa kielektoniki unaotumika kukusanya fedha zote za umma.

Ameongeza kuwa mfumo huo, ulianzishwa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizokuweko serikalini katika ukusanyaji wa fedha za Umma.

“Changamoto hizi ni pamoja na gharama kubwa za miamala inayohusu makusanyo ya fedha za umma, utaratibu usio rafiki kwa mlipaji wa huduma za umma unaoanzia namna anavyopatiwa ankara, anavyolipia ankara yake, anavyothibitisha malipo, anavyopatiwa stakabadhi hadi anavyopatiwa huduma; kulikuwa na machaguo (options) machache ya njia za kulipia (mabenki, mitandao ya simu za mkononi au Mawakala) kwa sababu kuongeza machaguo kulikuwa kunaongeza gharama za ukusanyaji kwa taasisi,

“Ilipohitajika kufungamanisha mfumo wa ankara wa taasisi na mifumo ya ulipaji (kama vile mabenki, mitandao ya simu za mkononi na mawakala wakubwa (Aggregators) gharama ilikuwa kubwa kwa sababu kila Mfumo ulifungamanishwa peke yake; Ilikuwa ni vigumu sana kupata taarifa ya makusanyo yanayofanyika kwa wakati huo huo.

“Changamoto nyingine, ni taasisi kusimamia mikataba mingi inayohusu makusanyo ya fedha za umma kwa kuwa kila njia ya kulipia ilitakiwa kuwa na mkataba wake; kulikuwa na utofauti katika viwango ambavyo kila taasisi ilikuwa inalipia kama gharama ya miamala kwa njia ileile ya malipo.

“Kwa mfano; benki/mtandao mmoja wa simu ulikuwa unatoza viwango viwili tofauti kwa taasisi mbili za umma anazozikusanyia fedha za umma),fedha zinazokusanywa na taasisi ya fedha hazikuwa zinaingia moja kwa moja kwenye account ya taasisi inayotoa huduma mpaka baada ya kipindi fulani ili kuruhusu usuluhishi (Reconcilliation) wa miamala kufanyika kwanza na hivyo kuchelewesha fedha kwenda kuwahudumia wananchi,” amesema Kwitega.

Alisema ili kukabiliana na changamozo wizara kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) ilibuni na kutengeneza Mfumo wa Kielektroniki wa Ukusanyaji Mapato ya kodi, maduhuli,tozo na huduma mbalimbali za Serikali (GePG).

“Huu ni mfumo unaowezesha ukusanyaji wa fedha za umma kielektroniki. Mfumo huu umebuniwa na kutengenezwa na wataalamu wa ndani wa Serikali. Aidha Mfumo huu upo kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Umma (PFA) ya mwaka 2001 kupitia marekebisho ya mwaka 2017 (Sura 348), na Waraka wa HAZINA Namba 3 wa mwaka 2017.

“Sheria ya Fedha za umma inawataka maofisa masuuli wote kukusanya fedha za Umma kupitia Mfumo wa GePG. Mfumo huu ulianza kutumika rasmi mnamo Julai mosi, 2017 ambapo ulianza na taasisi saba (7). Kwa sasa Mfumo huu unatumiwa na taasisi za Umma zaidi ya mia tano (500). Mfumo huu ndiyo unatoa kumbu kumbu namba (“Control number”) ya kulipia huduma na tozo mbalimbali za Serikali,”alisema Kwitega.

Alisema mfumo wa GePG umeleta faida kubwa na nyingi, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa uwazi na udhibiti katika ukusanyaji wa fedha za umma,uupata taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu makusanyo; Kuwa na Viwango na utaratibu unaofanana katika ukusanyaji wa Fedha za Umma kwa taasisi zote za Umma; Kuchochea ubunifu katika ukusanyaji wa fedha za Serikali na sekta ya fedha kwa ujumla kwa kuweka mazingira rafiki na ya usawa kwa Wakusanyaji.

Alisema umesaidia kutoa huduma bora na rahisi ya malipo ya fedha za Umma hivyo kuchochea ongezeko la makusanyo; Fedha kufika haraka katika akaunti kuu za makusanyo zilizoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT),kuwasaidia benki na mitandao ya simu kuwa na Sehemu moja tu ya kuunganisha mifumo yao na Mifumo ya taasisi za Umma (“Single point of Linkage”), hivyo kuzifikia taasisi za umma na kutoa huduma za kifedha kwa urahisi.

Alisema kuziwezesha benki na mitandao ya simu kuwa na mazingira rafiki na ya usawa katika Ukusanyaji wa Fedha za Umma; Kuzisaidia taasisi za Umma Kupunguza gharama zitokanazo na uwekezaji katika miundombinu ya Tehama pamoja na “Software Development” katika suala la ukusanyaji wa mapato; Urahisi katika usuluhishi wa miamala na uuluhishi wa taarifa za kibenki,kupunguza gharama za miamala inayohusu ukusanyaji wa Fedha za Umma; kumuongezea mlipaji wa huduma za umma machaguo mengi ya njia za kulipia huduma za Umma (Benki za Biashara zaidi ya ishirini na tano, Mawakala wa Benki, na mitandao ya simu yote sita na mawakala wanaotumia Mashine Maalum za Malipo zijulikanazo kama “Point of Sale – POS”.); na kurahisisha ulipaji wa huduma za umma hivyo kuokoa muda.

Alisema mwanzoni mwa mwaka wa Fedha 2020/21, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ilitoa kazi kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuufanyia thathmini ya kiutendaji Mfumo wa GePG.

Alisema Septemba 2020, taarifa ya tathmini ya kiutendaji ya mfumo huu ilitolewa na wataalam kutoka Chuo cha Tehama cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (CoICT). Katika taarifa hiyo imebainika kuwa Mfumo wa GePG umewezesha kuongezeka kwa makusanyo ya Serikali kwa ujumla wake na kwa taasisi moja moja.

“Mfano makusanyo ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) yameongezeka kutoka Sh 95,000,000,000.00 kabla ya kuanza kwa mfumo hadi kufikia Sh 115,000,000,000.00 baada ya kuanza kutumia mfumo wa kielektroniki; Wakala wa Vipimo (WMA) mapato yao yameongezeka kutoka kiasi cha shilingi bilioni 1.0 kwa mwezi kabla ya Mfumo wa GePG mpaka kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kwa mwezi baada ya kujiunga na GePG,” alisema Kwitega.

Alisema Taasisi nyingine zimepunguza gharama walizokuwa wanalipia ada za miamala ya kielektroniki inayohusu makusanyo ya fedha za umma.

“Kwa mfano Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ilikuwa ikilipa zaidi ya Sh bilioni 38 kwa mwaka kwa mawakala wa kuuza umeme. Baada ya kufunga mfumo wa GePG kwa sasa shirika halilipi chocho,” alisema Kwitega.

Alisema wizara inatambua kuwa Mafanikio ya mfumo huu wa GePG yanategemea ushiriki wa wananchi wote katika kuutumia.

“Kila mwananchi anayelipia huduma yoyote ya Umma ni lazima ahakikishe kuwa amepewa “Control number” na taasisi inayotoa huduma hiyo, na akiwa analipa ahakikishe amelipa kwa kutumia “Control number,”alisema.

Aliwaomba wahariri na wanahabari kuwaelemisha wananchi kutumia control number wanapofanya miamala ya serikali kwani kwa kufanya hivyo watakuwa na uhakika kwamba fedha walizolipa ziko salama na zimekwenda moja kwa moja mikononi mwa Serikali kwa ajili ya kuboresha maisha yao kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii.

Alisema kama watapatiwa uelewa mpana wananchi kuhusu utasaidia mno kusonga mbele na kuongeza mapato.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles