25.1 C
Dar es Salaam
Saturday, December 9, 2023

Contact us: [email protected]

Wananchi wa Malampaka waahidiwa maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria

Na Samwel Mwanga, Maswa

WAZIRI Wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amewaahidi wananchi wa Mji wa Malampaka Wilayani Maswa Mkoa wa Simiyu kupata maji ya uhakika kutoka Ziwa Victoria.

Akizungimza na wananchi Julai 22, 2022 katika mkutano wa hadhara mjini Malampaka, Waziri Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi amesema tayari mradi huo umekwisha kuanza baada ya Serikali kutoa fedha.

Sehemu ya wananchi wa mji wa Malampaka Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu wakifuatilia mkutano wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Maswa Magharibi.(Picha Na Samwel Mwanga).

Amesema maji hayo ambayo yatatoka kijiji cha Hungumalwa wilayani Kwimba yatapita kwenye mji huo ambao ni makao makuu ya jimbo hilo kabla ya kufika mji wa Malya na hatimaye mji wa Sumve wilayani Kwimba mkoa wa Mwanza.

Amesema mji wa Malampaka umekuwa ukikua kila kukicha hivyo wananchi wake kutopata maji ya uhakika ambayo ni ya visima kutokana nakuzidiwa na idadi ya watu.

“Mji wetu huu wa Malampaka ndiyo uso wa jimbo la Maswa Magharibi ni lazima uwe na maji ya uhakika na kadri shughuli za kiuchumi zikiendelea kwa kasi kama vile ujenzi wa reli ya kisasa na bandari ya nchi kavu tunahitaji maji ya uhakika ambayo yatatoka ziwa Victoria kwani idadi ya watu imeongezeka mara dufu.

“Hayana maji ya visima tuliyonayo kwa sasa hayawatoshelezi wakazi wa mji wetu wa Malampaka hivyo suluhisho pekee ya shida ya maji hapa ni Maji ya ziwa Victoria ambayo ninawahaidi tutayapata katika siku za hivi karibuni,”amesema Ndaki.

Waziri Ndaki amesema maeneo mengine yatakayonufaika na maji hayo kwenye jimbo hilo ni vijiji vyote vilivyoko kwenye Kata za Mataba na Nyabubinza.

Ameongeza kuwa atausimamia mradi huo ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo kwenye jimbo hilo wanapata maji safi na salama na yenye uhakika na kuondoa kelele zilizopo za wananchi wa Mji wa Malampaka kutokuwa na maji ya uhakika.

Awali, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira mjini Maswa(MAUWASA), Leonard Mnyeti alisema Mamlaka hiyo ndiyo imekuwa ikihudumia mji huo wa Malampaka lakini vyanzo vya maji vilivyopo havitoshelezi mahitaji ya maji kwa wakazi wa mji huo.

Amesema kwa sasa mji huo una wakazi 15,000 ambao mahitaji yao ya maji ni lita milioni moja kwa siku lakini wao wanazalisha lita 100,000 kwa siku hivyo hayatoshelezi.

mefafanua zaidi kuwa kwa sasa mwarobaini wa tatizo la maji katika mji wa Malampaka ni maji ya ziwa Victoria na tayari mradi huo umekwisha kuanza baada ya serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutoa maji kwenye Kijiji cha Mhalo hadi kijiji cha Hungumalwa wilayani Kwimba na hatimaye maji hayo kufikishwa katika mji huo.

“Tuliandika andiko serikalini tukiomba kiasi cha fedha Sh bilioni 29 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji haya kutoka ziwa Victoria na tayari serikali imeshatoa sehemu ya fedha hizo na mradi umeanza hivyo niwahakikishie wananchi wa mji wa Malampaka na Vijiji jirani kile kilio chenu cha kutopata maji yasiyotosheleza kinakwenda kuisha kwa siku za hivi karibuni,” amesema Mnyeti.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles