WANANCHI TARIME WASIKILIZWE, WASIVUNJE SHERIA

0
516

KWA siku mbili sasa, hali si shwari katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara mkoani Mara, kutokana na wananchi wengi kuvamia mgodi huo na kupora mali kadhaa.

Hali hiyo imesababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu kubwa ikiwamo kupiga mabomu ya machozi ili kutawanya kundi kubwa la wananchi ambao hawakutaka kutii amri ya jeshi hilo.

Mgodi huo upo chini ya Kampuni ya Acacia ambayo kwa siku za karibuni imekuwa na mvutano mkali na Serikali juu ya ulipaji wa kodi.

Tukio hilo, limetokea siku mbili mfululizo, kwa madai kuwa wananchi zaidi 400 wanaida hawajalipwa fidia ya maeneo yao kwa muda mrefu.

Bila kujali athari ambazo wangeweza kupata, wananchi hao walikwenda hadi kwenye mtambo wa kufua dhahabu na kufanya uharibifu.

Jambo hili ni la hatari kwa sabau tunaamini eneo hilo, ni hatari kwa maisha ya watu ambao hawana ujuzi wa aina yoyote.

Tunasema hivyo kwa sababu eneo hili lina mitambo  ambayo inatumia umeme mkubwa, linapaswa kuwa chini ya uangalizi wa wataalamu na si wananchi tu ambao hawana ujuzi wowote. Jambo hili kamwe halikubaliki.

Pamoja na wananchi kuwa na madai yao ya kutolipwa fidia muda mrefu, hayawapi mamlaka ya kujichukulia sheria mkononi kiasi hicho.

Tunatambua uongozi wa Kampuni ya Acacia, umekiri kudaiwa fedha hizo baada ya kuchukua maeneo yao kwa muda mrefu ili kupisha shughuli za uchimbaji.

Hii ni kutokana na maeneo mengi, kugundulika kuwa na madini yalipogundulika, wananchi waliondolewa kwa kufanyiwa tathimini ya  mali zao, yakiwamo mashamba, nyumba na kuahidiwa kulipwa fidia, lakini hadi sasa hawajalipwa stahiki, jambo ambalo linazua maswali.

Pamoja na uongozi wa Acacia kubandika majina ya wananchi katika ubao wa matangazo wanaopaswa kulipwa stahiki zao, hali imekuwa kinyume kabisa na kusababisha wengi kufurika kwenye ofizi za kampuni hiyo.

Pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga kushindwa kuzungumzia tukio, tunamshauri atumie uwezo wake kuhakikisha wananchi hao wanapata haki zao, huku akiwasihi wasivunje sheria kama tunavyoona sasa.

Tunatambua siku zote kuwa madai haya yamekuwapo kwa muda mrefu katika mgodi huo ambao ulianza kazi ya uzalishaji mwaka 2002.

Licha ya malalamiko hayo, mgodi huo pia umekuwa ukilalamikiwa kwa kusabababisha madhara mengi kwa wananchi wanaozunguka mgodi huo.

Tunajiuliza maswali mengi bila kupata majibu, hivi mgodi huu kweli umeshindwa kuwalipa wananchi hawa fidia, licha ya kuwa na uwezo huo?

Inasikitisha kuona jambo ambalo lilipaswa kumalizwa miaka kadhaa iliyopita, linachukua muda mrefu kiasi hiki na mwisho wa siku husababisha wananchi kupatwa na hasira zisizokuwa za msingi.

Kwa maana hiyo, tungependa kuona kuanzia sasa, Acacia wanachukua kila aina ya hatua ya kumaliza mzozo huu ambao mwisho wa siku watakaoathirika zaidi ni wananchi ambao wameamua kupambana na vyombo vya dola.

Sisi MTANZANIA, tunaushauri uongozi wa Acacia  kukutana na wawakilishi wa wananchi ili kumaliza jambo hili haraka iwezekanavyo. Wakati huo huo tukiwasihi wananchi wasivunje sheria za nchi kwa kujichukulia sheria mkononi.

Tunasema hivyo, kwa sababu matukio ya aina hii yamekuwa yakijirudia mara nyingi katika mgodi huo na kuleta madhara makubwa yakiwamo ya vifo visivyokuwa vya lazima.

Tunamalizia kwa kusema, wananchi wa Tarime wasikilizwe, lakini wasiwe wa kwanza kuvunja sheria.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here