Mwandishi Wetu, Manyara
Wananchi wa Kijiji cha Ilkiushbour wilayani Kiteto mkoani Manyara, wamemtaka Mbunge wao, Emmanuel Papian kukanusha kauli yake kuwa hakuna Mwananchi aliyepigwa risasi wala kugongwa na gari aliyoitoa mbele ya mawaziri Nane waliofika Kijiji cha Kimotorok kutatua kero na hifadhi Kiteto.
Mawaziri hao ni Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina, Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa na  Waziri wa Ulinzi Dkt. Husein Mwinyi .
Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo Omari Mgumba, na Waziri wa Maliasili Hamis Kigwangala ambaye alitolewa taarifa kutokuwepo kwakuwa alikuwa anauguza mtoto wake
Akizungumza leo Jumanne Februari 26, Papian amewaambia mawaziri hao kuwa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Ilkiushbour, Melubo Naiganya kuwa kuna mwananchi alipigwa risasi na mwingine kugongwa na gari la pori la Akiba la Mkungunero sio kweli.
“Naomba niweke rekodi sawa, mwananchi aliyedaiwa kupigwa risasi na mwingine kugongwa na gari sio kweli, aliangukia sime na mwingine alianguka wakati akifukuzana na askari hao,”amesema.
Aidha kwa mujibu wa mwenyekiti Naiganya alisema wananchi hao baada ya Mathayo Urumjee kugongwa na gari na Atabai Kuya kupigwa risasi, waliripoti polisi na kupelekwa hospitali kwa matibabu zaidi huku mmoja wao akitolewa risasi tumboni katika hospitali ya rufaa Dodoma na aliyegongwa na gari hali yake bado ni mbaya na anahitaji msaada zaidi.
“Tunaiomba Serikali kuokoa maisha ya mwananchi huyo kwa kugharamia matibabu yake baada ya kurejea nyumbani kwa kushindwa gharama lakini pia mifugo yao ng’ombe 265 zilizochukuliwa na askari wa pori la akiba Mkungunero,”amesema.