Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Darajani uliopo Kata ya Kimanga, Jafary Batenga amejikuta katika wakati mgumu kujibu hoja za wananchi waliokuwa wanataka kujua ni lini ujenzi wa choo cha ofisi hiyo utakamilika.
Wananchi hao wamepaza sauti zao Julai 15,2024 wakati wa mkutano wa hadhara uliohitishwa na Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, kwa lengo la kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
Katika mkutano huo Bonnah alielekeza wananchi waliokuwa na kero mbalimbali kupita mbele na kusiwasilisha kisha yeye kuzijibu kwa kushirikiana na watendaji mbalimbali wa serikali.
Miongoni mwa kero iliyowasilishwa ni ya ujenzi wa choo ambapo Mkazi wa Kimanga Darajani, Augustino Tozo, alihoji kinachosababisha choo hicho kutokamilika kwa wakati.
“Wananchi wamechangia mali zao, vijana tumetumia nguvu, masinki ya vyoo yamevunjwa bila sababu za msingi na ofisi ya serikali ya mtaa haina choo mpaka sasa,” amesema Tozo.
Akijibu hoja hizo Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Darajani, Jafary Batenga, amesema awali walipokea Sh 950,000 huku mbunge akichangia Sh milioni 2 na kwamba walipata mkandarasi ambaye ameshatumia Sh milioni 1.5 katika ya Sh milioni 2.9.
Hata hivyo wananchi walionekana kutoridhika na majibu hayo ambapo Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli, amesema atafuatilia zaidi kuhakikisha ujenzi wa choo hicho unakamilika ndani ya miezi miwili.
Katika mkutano huo pia wananchi waliwasilisha kero ya urasimishaji makazi, bima ya afya, usafi wa mazingira, ubovu wa barabara, ujenzi wa soko, kukosekana kwa maji na kubambikiwa ankara za malipo ambapo Bonnah ameahidi kuzifuatilia kuhakikisha zinatatuliwa.
Awali Bonnah alifanya ziara katika mitaa ya kata hiyo kukagua miundombinu ya barabara na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kupokea kero za wananchi.
“Imepangwa mipango mbalimbali ya maendeleo katika Jimbo la Segerea ikiwemo Kata ya Kimanga, barabara ni mbovu lakini zinakwenda kutengenezwa…nitasimamia mimi mwenyewe miradi yote inayotekelezwa na tutarekebisha mapungufu yote,” amesema Bonnah.
Bonnah amesema anatumia muda wa mapumziko ya vikao vya bunge na kamati kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, kukutana na makundi ya kijamii na kusikiliza kero ambapo zingine wanazipatia majibu ana kwa ana na zingine wanazifuatilia kuhakikisha zinapatiwa ufumbuzi.