-HAI
WAKAZI wa vijiji vinane wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, wamemwomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuondoa zuio la kusitisha shughuli za uendelezaji wa eneo linalozunguka Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA) lililowekwa na Mkuu wa wilaya hiyo, Gellasius Byakanwa .
Ombi hilo limetolewa na wananchi wanaoishi pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa KIA na kampuni ya Kilimanjaro Airports Development Company (Kadco), ambao umedumu kwa takribani miaka 30.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Sanya Station, Julias Mollel, alidai kuwa mkuu wa wilaya kutoa zuio la shughuli za kimaendeleo ni kurudisha nyuma ukuaji wa kimaendeleo zilizokuwa zikiendelea katika kata hiyo.
Alisema mpaka sasa wameshindwa kuendeleza shughuli mbalimbali ikiwemo ujenzi wa shule ya Msingi Ashe Engai ambayo ilikuwa inajengwa kwa nguvu za wananchi ili kuwaondolea adha wanafunzi ambao wanatembea umbali wa zaidi ya Kilomita nane kufuata huduma hiyo katika shule ya Tindigani .
“ Tunashindwa kumwelewa mkuu wetu wa wilaya, badala afike kutambua mgogoro wetu, anakaa ofisini na kutoa maagizo ya kuzuia uendelezaji, kwanza mkuu wetu ni mgeni ni vema angefika badala ya kusikiliza upande tu wa Kadco na kutoa zuio,” alisema
Kwa upande wake, Diwani ya Kata ya Kai, Yohana Laiza, ameitaka Serikali kuangalia upya mkataba wa KIA na Kadco kutokana na kutokuwa na manufaa yoyote kwa Serikali na badala yake kuendelea kuwanufaisha watu wachache.
“Kampuni hii ni ya kitapeli na imekuja kwa ajili ya kunyanyasa wananchi kwa kutaka kuwanyang’anya ardhi yao, naiomba Serikali kupitia mkuu wa mkoa, mtoe msimamo wenu juu ya kampuni hii,” alisema.
Akizungumzia sula hilo, Diwani wa Kata ya Masama Rundugai, Elibariki Mbise, alifafanua kuwa kitendo cha Kadco kudai eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 92, kuwa ni mali yao huku wananchi wa eneo hilo wakiwa wameishi hapo kwa muda wa zaidi ya miaka 70, ni kutaka kuwadhulumu wananchi haki yao ya kumiliki ardhi.